Vurugu Mtwara: Wabunge waangua vilio

Nyumba ya Mbunge wa Jimbo la Masasi,Mariam Masembe ambayo ilichomwa moto na watu wenye hasira. Vitu mbalimbali viliharibiwa.

Muktasari:

Vitu vingine vilivyoteketezwa ni Ofisi ya Maliasili ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo Lisekese, Ofisi ya Ukaguzi, Shule ya Msingi, Ununuzi na Ugavi na magari sita ya halmashauri ya wilaya.Mzuki alisema mbali na uharibifu huo, watu 4 wameuwa na 11 kujeruhiwa.

WABUNGE waliochomewa nyumba na mali zao katika vurugu zilizotokea Mtwara juzi; Anna Abdallah na Mariam Kasembe, jana waliangulia vilio walipotakiwa na gazeti hili kuzungumzia tukio hilo.

Nyumba za wabunge hao wa Viti Maalumu na mali zingine kadhaa za taasisi mbalimbali, ni miongoni mwa vitu vilivyoharibiwa katika vurugu hizo ambazo pia zilisababisha vifo vya watu wanne wilayani Masasi.

Akizungumza kwa huzuni,  Anna alisema hajui sababu za uharibifu huo, hasa ikizingatiwa mwenyewe amekuwa huko kwa karibu siku tatu na hakuona dalili za uhasama wowote dhidi yake.

Anna ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho alisema: “Nina siku ya tatu hapa Masasi na nimeshiriki mkutano wa halmashauri kwa mwaliko na wakati wote, sikuhisi chochote hivyo siwezi kujua sababu ya chuki iliyofanya nyumba yangu ichomwe moto,” alisema.

Alipotakiwa aeleze hali ilivyokuwa, alisema, “Wavamizi hao walipora kila kitu nyumbani kwangu yakiwamo mapazia, kabla ya kumwaga petroli kila chumba na kuwasha moto.”

Aliendelea kueleza,” Kila kitu kiliteketea. Inatia uchungu kwani nyumba hiyo niliijenga kwa kudunduliza fedha kidogo kidogo nikiwa mkuu wa mkoa.”
Anna alisema, kundi hilo la vijana lilivamia nyumbani kwake saa 4:00 asubuhi na kuanza kupora mali kwa kupita chumba kimoja baada ya kingine.

“Hali si nzuri. Kila kitu kimeibwa na nyumba imechomwa moto, hakuna kilichobaki. Walichukua kila kitu na itanichukua muda mwingi kujua thamani halisi ya hasara iliyopatikana,” alisema.

Kauli ya Kasembe
Naye Kasembe alipokea simu ya mwandishi wa habari hii kwa kilio na kuikata huku akisema, “Jamani niacheni… Mwenzenu naumia…!”
Alipopigiwa tena baadaye, alisema anashangazwa na tukio hilo ambalo limemfika bila kutarajia na kumtia hasara kubwa.

“Wamepora kila kitu katika nyumba na kuichoma moto, sijui atakuwa nani huyu, kwani sina tatizo na wapiga kura wangu na sina mgogoro na mtu yeyote. Nashindwa hata kuhisi nani kafanya uchochezi,” alisema Kasembe.

Alisema wakati wa vurugu hizo, ndugu zake akiwamo mama yake, walikimbia na kwenda kujihifadhi hotelini, lakini mpaka sasa hawajui wataishi vipi baada ya nyumba hiyo kuteketezwa kwa moto.

“Jana wanafamilia walilala hotelini na leo tupo nje ya gofu la nyumba yangu ambayo imeteketea kabisa kwa moto, tunasubiri majaaliwa mengine, lakini nimechanganyikiwa kwa kweli na sijui ni kitu gani hiki, siamini,”alisema.

Polisi waeleza uharibifu
Watu 44 wanashikiliwa na polisi wilayani Masasi kufuatia vurugu hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Mtwara, Maria Mzuki alisema watu hao wamekamatwa kwa wakituhumiwa kujihusisha na vurugu hizo zilizosababisha uhalibifu mkubwa mali.

Mbali na nyumba za wabunge hao, Mzuki alitaja mali zingine zilizoharibiwa katika vurugu hizo kuwa ni ofisi za CCM Wilaya, Mahakama ya Mwanzo Masasi na magari matano katika ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.

Vitu vingine vilivyoteketezwa ni Ofisi ya Maliasili ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo Lisekese, Ofisi ya Ukaguzi, Shule ya Msingi, Ununuzi na Ugavi na magari sita ya halmashauri ya wilaya.Mzuki alisema mbali na uharibifu huo, watu 4 wameuwa na 11 kujeruhiwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, Beatrice Dominick, alisema halmashauri yake imepata hasara kubwa kwa kupoteza kumbukumbu mbalimbali hasa katika Idara ya Ununuzi na Ugavi. Dominick alisema gari 11 zimechomwa moto

Chagonja azungumza
Katika hatua nyingine, Kamishna wa Mafunzo na Oparesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja yuko mkoani Mtwara kufuatilia vurugu zinazoendelea huko na kusababisha uharibifu wa mali.
Akizungumza gazeti hili jana Kamishna Chagonja alisema, moja ya kazi iliyompeleka mkoani humo ni kurejesha amani ili hali ya usalama irejea na wananchi waendelee na shughuli zao.

“Hali ni shwari sasa na tunaendelea na upelelezi kuwabaini waliosababisha vurugu hizo. Kwa wale tunaowashikilia tunakamilisha upelelezi na siku yoyote tutawafikisha mahakamani ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe,” alisema.

Nchimbi, Mwema, Mwamunyange watua Mtwara
Habari zilizolikifia gazeti hili jana wakati tunaenda mitamboni zimeeleza kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani  Dk Emmanuel Nchimbi ameenda mkoani Mtwara, kufuatilia vurugu hizo.

Habari hizo zimesema kuwa Nchimbi  katika ziara hiyo ameambatana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, (IGP) Said Mwema.
Jana watendaji hao walikuwa na mkutano wa ndani na viongozi wa serikali mkoani  Mtwara na taarifa kutoka ndani  ya vikao hivyo zimedokeza kuwa wamepanga kuzungumza na wananchi leo.

Wamkataa Mkuchika
Wakazi wa Wilaya ya Newala wamemkataa Mbunge wao, George Mkuchika kwa maelezo kuwa ni msaliti kwa kuridhia gesi asilia inayochimbwa Msimbati kupelekwa Dar es Salaam kwa njia ya bomba bila ridhaa yao.

Wananchi hao waliyasema hayo jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo mjini Newala, baada ya kuulizwa na Katibu wa CUF Wilaya ya Mtwara, Saidi Kulaga iwapo walishirikishwa katika mchakato wa kuridhia gesi kupelekwa Dar es Salaam.

Katibu huyo aliwauliza wananchi “Huyu ni Mbunge wenu? Anawakilisha mawazo ya nani?”…. “Siyo mbunge wetuuu…Ametusalitiii…Anawakilisha njaa zakeee” walijibu wananchi hao kwa sauti za juu.

Kabla ya mkutano huo kuanza, Tanesco walikata umeme uwanjani hapo hali iliyoibua tena vurugu baada ya wananchi kuvunja vioo vya magari kwa mawe na ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba, Newala.  Kutokana na vurugu hizo, polisi walilazimika kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Habari hii imeandikwa na Ibrahim Yamola, Joseph Zablon, Abdallah Bakari, Newala, Mwanja Ibadi Masasi