Vita vyashika kasi nchini Ukraine

Muktasari:
- Mambo magumu Ukraine. Vikosi vya Russia vimesonga mbele karibu na mji mkuu kutokea upande wa kaskazini, magharibi na kaskazini mashariki.
Kyiv, Ukraine. Mashambulizi ya Russia yameendelea katika maeneo mbalimbali nchini Ukraine na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa. Pamoja na maeneo mengine, majeshi hayi ya Russia yameharibu uwanja wa ndege kusini mwa mji wa Vasylkiv.
Mykhailo Podolyak, mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema tayari Kyiv “imezingirwa” huku jeshi na watu wa kujitolea wakijiandaa kulitetea jiji hilo, mtaa kwa mtaa.
Janga Mariupol
Viongozi wa Ufaransa na Ujerumani wanamsihi Rais wa Russia Vladimir Putin kukomesha kuzingirwa kwa mji wa Mariupol, ambapo wakazi wamekwama kwa kukosa maji na umeme kwa siku 11 na kuna ripoti za watu kufa kutokana na njaa na baridi.
Meya wa Mariupol, Vadym Boichenko amesema zaidi ya raia 1,500 wameuawa katika mji huo. Maiti zimelala mitaani bila kuchukuliwa.
Maofisa wa Ukraine na Russia wameelezea hali ya kibinadamu inayozidi kuwa mbaya kama “janga”.
Ukraine inadai msikiti mmoja ambapo takriban raia 80 walikuwa wamejihifadhi ulipigwa makombora lakini mtu anayekaa katika eneo hilo alikanusha taarifa hizo akisema kombora hilo lilianguka umbali wa mita 700 kutoka kwenye msikiti huo.
Marekani yaidhinisha msaada
Rais wa Marekani Joe Biden ameidhinisha dola 200 milioni za ziada kwa jeshi la Ukraine. Marekani tayari imeidhinisha dola milioni 350 kwa ajili ya vifaa vya kijeshi, fedha ambazo ni nyingi zaidi katika historia ya Marekani.
Ukraine yalalamika
Ukraine imedai kuwa wanajeshi wa Russia wamelifyatulia risasi kundi la wanawake na watoto waliokuwa wakitoka katika kijiji karibu na Kyiv na kuua saba, mmoja wao mtoto, idara ya kijasusi ya kijeshi ya Ukraine imesema.
Vilevile, imesema njia tisa kati ya 14 za misaada ya kibinadamu zilizofunguliwa zimefanikiwa, naibu waziri mkuu wa Ukraine amesema, huku takriban watu 13,000 wakifanikiwa kuhama Jumamosi kupitia njia hizo.
Wanajeshi 1,300 wauawa
Takriban wanajeshi 1,300 wa Ukraine wameuawa tangu kuanza kwa uvamizi huo, Rais Zelensky amesema, ikiwa ni mara yake ya kwanza kutoa takwimu za vifo vya wanajeshi wa Ukraine vilivyotokana na vita hivyo. Machi 2 Russia ilisema imepoteza wanajeshi 498, lakini Zelensky anasema ni karibu 12,000.
Umoja wa Mataifa unasema Takriban raia 579 wa Ukraine wameuawa, ukisisitiza kwamba takwimu zake pengine zilikuwa chini kuliko takwimu halisi.
Uchumi wayumba
Waziri Mkuu Denys Shmyhal amesema itakuwa muhimu kurekebisha uchumi wa Ukraine kutokana na ukosefu wa vifaa, na kuwataka watu katika maeneo ambayo hayana vita kurejea kazini.
Rais Zelensky amesema mbinu inayotumiwa na Russia ni tofauti na mazungumzo ya awali ambapo Moscow “ilitoa matamshi” tu na kwamba “anafurahi kupata ishara kutoka Russia” baada ya Putin kusema aliona “mabadiliko chanya” katika mazungumzo yao.
Kiwanda cha nyuklia
Wahandisi wa Russia wamewasili kupima mionzi katika kinu cha nyuklia cha Ukraine huko Zaporizhzhia na kukamatwa kwa kinu hicho kumezua hofu ya kimataifa, maafisa wamesema.
Hospitali yashambuliwa
Hospitali ya matibabu ya saratani na kliniki ya macho zimeharibiwa kutokana na mashambulizi ya mabomu ya jiji la Mykolaiv, karibu na bandari ya kimkakati ya Odessa katika Bahari Nyeusi, hii ni siku chache baada ya hospitali ya uzazi huko Mariupol kupigwa makombora.
Umoja wa Mataifa kukutana
Wanadiplomasia wanasema Umoja wa Mataifa utakutana wiki hii kuhusu vita vya Russia nchini Ukraine, ingawa haijafahamika iwapo mkutano huo utasaidia kusitishwa kwa mapigano.
Silaha za kibayolojia
Nchi za Magharibi zimekataa madai ya Russia kwamba Marekani na Ukraine zilitafiti kwa kutumia popo kufanya vita vya kibaolojia. Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa anasema madai hayo ni “upuuzi mtupu”.
Kanisa lagawanyika
Makasisi wa Kanisa la Orthodox la Russia katika mji wa Uholanzi wa Amsterdam wametangaza kujitenga na Kanisa la Moscow kwa sababu ya vitisho kwao kutokana na uvamizi wa nchi hiyo kwa Ukraine.
Milioni 2.6 walikimbia
Takriban watu milioni 2.6 wamekimbia “vita visivyo na maana” nchini Ukraine, Umoja wa Mataifa unasema. Zaidi ya nusu ya hao wamehamia Poland.
Msururu wa makombora
Msururu wa makombora ulikishambulia kituo cha mafunzo ya kijeshi magharibi mwa Ukraine, takriban maili 15 kutoka mpaka wa mwanachama wa Nato, Poland, maafisa walisema jana Jumapili.
Kituo cha Kimataifa cha Ulinzi wa amani na usalama, kati ya Lviv na mpaka wa Poland, kwa miaka mingi kimekuwa kikitumiwa na Marekani na nchi nyingine za Nato kwa mazoezi ya pamoja na Ukraine.
Shambulio hilo la anga lilikuja siku moja baada ya Kremlin kuonya kwamba inaona shehena za silaha za Magharibi kama “shabaha halali” kwa wao kuishambulia.
Ukraine imeonya kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu wakati vita inaingia siku ya 18.