Viongozi wa dini Dar, wasisitiza amani kuelekea uchaguzi mkuu
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamati hiyo imeeleza wananchi na viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kulinda amani sambamba na kuimarisha umoja na mshikamano.
Dar es Salaam. Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, imesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini wananchi wa mkoa huo, kulinda na kuitunza amani hasa katika kipindi ambacho, Taifa linajiandaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye.
Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo imeeleza wananchi na viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kulinda amani sambamba na kuimarisha umoja na mshikamano uliopo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar amesema amani ni tunu adhimu inayopaswa kulindwa kwa nguvu zote wananchi na viongozi wa dini pamoja wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuzuia viashiria vya uvunjifu.
Sheikh Walid amesema katika kongamano la Amani kwa viongozi wa dini wa mkoa wa Dar es Salaam kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Lengo la mkutano huo, kujadili nafasi ya viongozi wa katika kulinda na kutetea amani ya nchi.
Mwenyekiti huyo, amesema ni wajibu wa kila kiongozi wa kiroho kuhakikisha ujumbe wao unaleta mshikamano na si mgawanyiko katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, akisisitiza umakini unahitaji.
Katibu Mkuu wa Kanisa la Methodist, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Kamati ya Amani wilayani Kinondoni, Askofu Allen Siso amesema ni vyema viongozi wakasalia katika kuhubiri amani akisema ni wajibu wao wa msingi.
“Viongozi wa dini tuna nafasi ya kipekee na dhamana kubwa katika dunia ya leo, sisi ni taa ya maadili, walimu na sauti ya matumaini kwa waliovunjika moyo. Kiongozi wa dini anapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si sehemu ya tatizo,” amesema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam Tanzania (Juwakita), Shamimu Khan amewataka wanasiasa kutumia lugha za staha katika kampeni zao na kujiepusha na matusi au maneno ya chuki.
“Lugha nzuri huleta upendo na mshikamano, siasa zetu zinapaswa kujengwa katika misingi ya heshima. Nimewahi kuwa mbunge wa kuchaguliwa jmbo la Morogoro Mjini niliongoza vyema, nawahamasisha wanawake,” amesema Khan.