Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijiji vinne kunufaika na mradi wa kurejesha ikolojia Muheza

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Gilbert Kalima (katikati), akizindua Mradi wa Urejeshaji wa Mifumo ya Ikolojia na Ustahimilivu wa Jamii nchini Tanzania (Tunza). Picha na Mbonea Herman.

Muktasari:

  • Mradi huo unalenga kulinda vyanzo muhimu vya maji vya Milima ya Amani kwa kuimarisha ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa mazingira, kuongeza ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Tanga. Vijiji vinne vilivyopo katika eneo la Usambara Mashariki, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, vimeingizwa kwenye mpango wa urejeshaji wa mifumo ya ikolojia na kuimarisha ustahimilivu wa jamii nchini kutokana na umuhimu wa eneo hilo katika kuhifadhi vyanzo vya maji vinavyohudumia maelfu ya wananchi.

Mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Foundation OCP, taasisi ya Morocco iliyojikita katika kuendeleza maendeleo endelevu ya binadamu nchini humo na katika nchi nyingine za Ukanda wa Kusini.

Vijiji vilivyochaguliwa ni Kwemdimu, Amani, Kiwanda na Kwesimba, ambavyo kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa kwa kushirikiana na Serikali, vinahitaji kuongezewa nguvu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza leo Jumatano, Julai 22, 2026 wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Meneja wa Programu ya Uhifadhi wa Maeneo ya Pwani na Bahari wa IUCN, Joseph Oliva, amesema vijiji hivyo vimepewa kipaumbele kutokana na utegemezi mkubwa wa jamii kwenye kilimo cha mazao ya viungo na umuhimu wa eneo hilo katika uhifadhi wa mazingira.

Amesema shughuli za uzalishaji katika eneo hilo zinapaswa kuendana na misingi ya uhifadhi ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika bila kuharibu mifumo ya ikolojia.

"Usambara Mashariki ndiyo yalipo maeneo ya Milima ya Amani, ambayo ni chanzo kikuu cha maji yanayotegemewa katika wilaya za Muheza, Tanga, Mkinga, Korogwe na Pangani," amesema Oliva.

Amesema licha ya shughuli za uhifadhi kufanyika kwa muda mrefu katika maeneo hayo, bado zipo changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuimarisha juhudi zilizopo.

"Tathmini yetu ilionyesha kuwa vijiji hivi vinahitaji msaada zaidi ili kuimarisha shughuli za uhifadhi zinazoendelea na kuhakikisha jamii zinapata manufaa kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira," amesema.

Kwa mujibu wa Oliva, mradi huo utalenga kuwajengea uwezo wananchi kufanya shughuli za uzalishaji zinazolinda mazingira, huku ukiimarisha mifumo ya ikolojia na ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema utekelezaji wa mradi huo utazingatia maeneo manne makuu ambayo ni kuandaa mikakati na miongozo ya urejeshaji wa mifumo ya ikolojia, kujenga uwezo wa taasisi za kijamii na kamati za usimamizi wa mazingira, kushirikisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika uhifadhi, pamoja na kutumia suluhisho zinazotokana na mazingira asilia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima amesema mkoa huo una rasilimali nyingi za asili ambazo ni msingi wa uchumi na maisha ya wananchi, lakini zinaendelea kukabiliwa na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Amesema mradi huo ni mfano mzuri wa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi kupitia shughuli za kiuchumi zinazozingatia mazingira.

"Tunafurahia kuona mradi huu unatekelezwa kwa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja. Hii ndiyo njia sahihi ya kuhakikisha uhifadhi unaenda sambamba na maendeleo ya jamii," amesema Kalima.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Salimu Sechambo, amesema mradi huo utakuwa na mchango mkubwa kwa wananchi wa vijiji vinne kwa kuongeza uzalishaji na kipato huku ukilinda mazingira.

"Mradi huu ni fursa kubwa kwa wananchi wetu. Utawasaidia kufanya shughuli za uzalishaji rafiki kwa mazingira na wakati huohuo kulinda vyanzo vya maji vinavyotegemewa na maelfu ya wananchi," amesema.

Naye mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima Wahifadhi Mazingira, Twaha Mbaruku amesema wakulima wana matumaini kuwa mradi huo utawasaidia kupata mbinu bora za kilimo kinachoongeza uzalishaji bila kuathiri mazingira.

"Kupitia mradi huu wakulima watajifunza mbinu za kisasa za uzalishaji zinazolinda mazingira. Hili ni jambo muhimu kwa sababu maeneo haya ndiyo chanzo cha maji kwa wilaya nyingi za Mkoa wa Tanga," amesema.

Mradi wa Tunza unatarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika uhifadhi wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha uwezo wa wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kukuza shughuli za uzalishaji zenye tija na endelevu.