Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ofisi ya Msajili yageuzwa kimbilio wanachama wenye migogoro

Muktasari:

  • Hata hivyo, makada hao wamesema hatua ya kwenda kwa Msajili ni kutafuta haki waliokosa, sambamba na kuijulisha ofisi hiyo kuhusu kinachoendelea ndani ya Chadema.



Dar es Salaam. Mfululizo wa wanachama wa vyama vya siasa kufikisha malalamiko yao kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa umeibua mjadala kuhusu mipaka ya ofisi hiyo na umuhimu wa kufuata taratibu za ndani za vyama husika.

Jana, Jumanne, Julai 21, 2026, waliokuwa viongozi wa Chadema Wilaya ya Muheza, Kilindi na Mkoa wa Morogoro walifika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakipinga hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi yao, wakidai zimekiuka Katiba na kanuni za chama.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria wamewataka wanachama na viongozi wa vyama vya siasa kufuata kwanza taratibu za ndani za vyama vyao wanapokumbana na migogoro, badala ya kukimbilia moja kwa moja kwa msajili.

Kwa mujibu wa wanasheria hao, katiba za vyama zinaeleza namna ya kushughulikia malalamiko kuanzia ngazi za chini hadi vikao vya juu vya maamuzi kabla ya kutafuta msaada nje ya chama.

Alipoulizwa kuhusu hatua ya makada au viongozi wa vyama vya siasa kukimbilia katika ofisi yake, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema mtu anapopeleka jambo katika taasisi hiyo huwa na sababu zake.

“Sheria haikatazi kuleta kwa Msajili. Hakuna sheria inayosema kwamba lazima umalize matatizo yako ndani ya chama. Mtu anaona sehemu bora ambayo haki yake itapatikana ndipo anapopeleka matatizo yake.

“Mbona kuna wengine kina Zitto (Kabwe) na Hamad Rashid walikimbilia mahakamani walipopata changamoto kwenye vyama vya Chadema na CUF?” amehoji Nyahoza.

Nyahoza amesema si lazima mtu asubiri kila kitu ndani ya chama, anaweza kutafuta njia nyingine ya kutatua suala hilo, ikiwamo mahakamani au kwa Msajili.

“Ni haki yao, ilimradi aangalie anapopeleka jambo lake, sheria inamruhusu,” ameeleza.

Katika miaka ya karibuni, baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa wamekuwa wakifikisha malalamiko yao kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakipinga maamuzi ya vyama vyao.

Miongoni mwao ni Mchungaji Dk Godfrey Malisa, aliyewasilisha malalamiko akipinga uamuzi wa CCM wa kumfukuza uanachama baada ya chama hicho kutangaza hatua hiyo Februari 2025.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, aliyekuwa Katibu wa Uenezi Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala, aliwasilisha malalamiko akipinga uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho, Luhaga Mpina, na baadaye kupinga kuvuliwa uanachama, akidai hatua hiyo ilikiuka Katiba ya chama na sheria za nchi.

Kwa CUF, baadhi ya wanachama waliwasilisha malalamiko wakipinga taratibu za uchaguzi wa ndani. Mwaka huu pia walifanya maandamano katika Ofisi ya Msajili jijini Dar es Salaam wakitaka mrejesho wa malalamiko yao, wakidai kulikuwa na kasoro katika uchaguzi uliomwingiza madarakani Mwenyekiti mpya, Yusuf Mirambo.


Wasemavyo wadau

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano, Julai 22, 2026, wakili Alyoce Komba amesema mwanachama au kiongozi anayepata changamoto ndani ya chama anapaswa kwanza kurejea Katiba na kanuni za chama husika ili kuona utaratibu wa kushughulikia malalamiko yake.

Komba amesema endapo mwanachama anaona haki yake imekiukwa, anatakiwa kutumia mifumo ya ndani ya chama kuanzia ngazi za chini hadi vikao vya juu vya maamuzi kabla ya kutafuta msaada nje ya chama.

“Kama kuna tatizo, atafungua shauri kwa mujibu wa Katiba ya chama chake. Katiba za vyama zinaeleza utaratibu wa kupeleka malalamiko kuanzia ngazi za chini hadi juu, ikiwamo Kamati Kuu, Mkutano Mkuu au Halmashauri Kuu,” amesema.

Aidha, Komba amesema kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kunapaswa kuwa hatua ya mwisho baada ya taratibu zote za ndani kushindikana.

“Msajili hawezi kurukia suala la mwanachama moja kwa moja kwa sababu kuna taratibu za ndani za chama ambazo zinapaswa kufuatwa,” amesema.

Kwa upande wake, wakili Peter Madeleka amesema Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuwa juu ya Katiba za vyama vya siasa vilivyosajiliwa, ambavyo vinaendesha shughuli kwa mujibu wa katiba zao.

Madeleka amesema mwanachama anayepinga uamuzi wa chama chake anatakiwa kutumia njia zilizowekwa ndani ya chama kuanzia ngazi ya tawi, kata, wilaya au mkoa kabla ya kufikia hatua nyingine.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina mamlaka ya kuingilia michakato ya uendeshaji wa shughuli za chama kwa sababu mwanachama ameenda kulalamika ofisini kwake,” amesema.

Madeleka amesema uanachama unatokana na chama husika na si Ofisi ya Msajili, hivyo changamoto za ndani zinapaswa kuanza kutatuliwa ndani ya mfumo wa chama.

“Ulipoingia ndipo utakapotokea, ulipoingia ndipo utakapotatua matatizo yako. Si kinyume na hivyo,” amesema.

Hata hivyo, Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, inampa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya kufuatilia mwenendo wa vyama ili kuhakikisha vinafuata sheria, kanuni na masharti ya usajili.

Mjadala kuhusu mipaka ya mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa uliwahi kufika katika Mahakama ya Afrika Mashariki. Machi 25, 2022, mahakama hiyo ilitoa uamuzi uliowapa ushindi Freeman Mbowe na wenzake, akiwamo Seif Sharif Hamad (marehemu), Zitto Kabwe, Hashim Rungwe, Salum Mwalimu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC).

Katika kesi hiyo iliyohusu mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa, mahakama hiyo ilisema baadhi ya vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa vinakiuka Mkataba wa EAC.

Waliosimamishwa Chadema wafunguka

Wakati wanasheria wakieleza hayo, jana Julai 21, 2026, waliokuwa viongozi wa Chadema Wilaya ya Muheza, Kilindi na Mkoa wa Morogoro waliokwenda Ofisi ya Msajili kulalamika kuwa hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi yao zimekiuka Katiba na kanuni za chama.

Mmoja wao, Barnaba Okola, amekiri kukata rufaa katika Kamati Kuu ya Chadema kupinga hatua iliyochukuliwa na uongozi wa Kanda ya Kati ya chama hicho ya kumsimamisha ukatibu wa Mkoa wa Morogoro.

“Nimekata rufaa, Kamati Kuu bado haijasikiliza, lakini tulichokifanya ni kumpa taarifa ya ujumla Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kinachoendelea Chadema,” amesema.

Kwa upande wake, Cosmas amesema hajaridhika na uamuzi uliofanywa na uongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini, ndiyo maana amekimbilia Ofisi ya Msajili ili kupata haki zake.

“Kilichofanyika ndani ya Chadema si sahihi, ndiyo maana tumeenda kwa Msajili. Ofisi ya Msajili ni mlezi wa vyama vya siasa, ndiyo maana tukimbilia kwake,” amesisitiza.

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya, amesema taratibu za kuwasimamisha uongozi Cosmas na Mwakidasi zilifuatwa, sambamba na kuwapa siku 14 za kujieleza ambazo bado hazijaisha.