Mkuu wa wilaya, hakimu, DAS, madiwani waburuzwa Baraza la Maadili

Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu, Sivangilwa Mwangesi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Machi 26, 2025 na Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu, Sivangilwa Mwangesi viongozi hao wanatuhumiwa kwa ukiukaji wa maadili
Dodoma. Sektarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewafikisha viongozi tisa katika Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa maadili kwa viongozi wa umma.
Viongozi hao ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Sakina Mohamed, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Kaliua, Tabora, Idefonce Arthur Columba, Hakimu Mahakama ya Mwanzo Puge(Tabora), Cleophas Mziray na Katibu Tawala Wilaya ya Arusha, Jacobo Rombo.
Wengine wanaolalamikiwa ni Msajili wa Hati Msaidizi wa Mkoa wa Tanga, Mwajuma Kihiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba katika Halmashauri ya Wilaya Korogwe, Edward Mhina, Diwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mwandei Mohamed, Diwani wa Mayomboni, Tanga, Mussa Jangwa na Eligius Adrian Mbena ambaye ni Diwani wa Kolero, Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Machi 26, 2025 na Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu, Sivangilwa Mwangesi, viongozi hao wanatuhumiwa kwa ukiukaji wa maadili kwa mujibu wa kifungu cha 6 na 12 vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995.
“Sekretarieti ya maadili na viongozi wa umma imepeleka malalamiko kwenye Baraza la Maadili kuhusu tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa maadili kwa viongozi wa umma ikiwamo kushindwa kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni kwa Kamishna wa Maadili,” anasema Mwangesi.
“Hiyo ni baada ya kuwapo kwa malalamiko kwa viongozi mbalimbali jambo linalolifanya baraza kufanya kikao cha uchunguzi wa kina wa malalamiko hayo Machi 27 na 28, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Sekretarieti ya Maadili Mtaa wa Tambukareli jijini Dodoma,” inaeleza taarifa hiyo.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni taasisi inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais na jukumu lake kubwa ni kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa.
Viongozi hao wameitwa katika sekratarieti ya maadili ikiwa ni muendelezo wa viongozi mbalimbali ikiwamo Mathew Mbaruku ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga pamoja na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, Julius Ningu.