Sekretarieti ya maadili shubiri kwa vigogo Serikalini
Katibu wa Ukuzaji wa Maadili kutoka Tume ya Maadili ya viongozi wa Umma, Waziri Kipacha akiwa katika mahojiano maalum na mwandishi wa Mwananchi Habel Chidawali ofisini kwake jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Dodoma. Eti Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haina meno? Je unakumbuka kesi ya Escrow na matokeo yake?
Kwenye kesi ya Escrow yalitolewa mapendekezo ya adhabu mbalimbali Kwa baadhi ya viongozi waliotajwa na kwenye kashfa ambapo utekelezaji wa kuwashughulikia ulitajwa.
Mbali na hukumu ambazo chombo hiki huzitoa lakini baadhi ya watu wanadai kuwa hukumu zake hazina meno kwa madai kuwa waliowahi kupitia hapo waliendelea kula maisha mtaani.
Kauli hiyo inapingwa na Katibu Idara ya Ukuzaji Maadili wa Sektretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha huku akisema chombo hicho ni mwiba kwa wanaokiuka sheria.
“Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa chombo mwiba kwa watumishi wanaokiuka maadili katika utumishi wao lakini haina ubaya na wenye kufuata misingi ya utumishi,”anasema Kipacha.
Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa namna vigogo wanavyopishana katika vyumba vya Baraza la Maadili kwa tuhuma za ukiukwaji maadili ya utumishi na baadhi yao wanasema kufika mbele ya baraza hilo shubiri yake ngumu kuliko Mahakama Kuu.
Tukio la hivi karibuni kwa chombo hicho lilikuwa ni kuwahoji Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Dk Julius Ningu (59), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mathew Mbaruku kwa tuhuma za ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.
Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti zilizopo jijini Dodoma, Kipacha alieleza kazi zinazofanywa na chombo hicho na changamoto zake.
“Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa ibara ya 132 ya Katiba ya nchi na ilianza kazi rasmi Julai 1996 lengo ni kusimamia maadili ya viongozi wa umma,” anasema Kipacha.
Kipacha anataja majukumu ya chombo hicho ni kupokea taarifa za mali na madeni zinazohitajika kutolewa na viongozi wa umma kwa mujibu wa sheria laini tunapokea malalamiko na tuhuma kuhusu ukiukwaji wa sheria ya maadili na kufanya uchunguzi.
Anasema taarifa zinazopokewa na chombo hicho pia huhakikiwa na inapobidi lazima wajiridhishe kwa kuhoji na kuziona mali kwa wahusika popote zilipo.
Tofauti ya Sekretarieti na Baraza la Maadili
“Baraza ni chombo kinachoundwa kwa mujibu wa sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (sura 398) ambao kazi yake ni kushughulikia ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na mgongano wa kimaslahikatika shughuli za umma,” anasema.
Kwa mujibu wa Kipacha, baraza linalojukumu kubwa katika kushughulika na wavunjifu wa maadili pale linaokaa kama mahakama kwa lengo la kuwahoji watuhumiwa waliokiuka maadili ya viongozi wa umma.
Kwa sasa Baraza linangozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu, Rose Teemba ambaye ni mteule wa Rais akisaidiwa na wajumbe wawili ambao ni Peter Ilomo na Suzan Mlawi.
Jinsi ya kuendesha kesi
Kama ilivyo kwa mahakama katika uendeshaji wa mashauri, muundo wa baraza hili linapoketi katika kesi zake huwepo mawakili na waendesha mashtaka na mashahidi huitwa kama itabidi.
“Kesi ya pale siyo lelemama, watu wanapewa nafasi ya kujitetea na kujieleza mbele ya mwenyekiti wa baraza hadi kijasho kinawatoka, shughuli yake siyo mchezo,” anasema Kipacha.
Kama ilivyo kwa mahakama za kawaida, mashtaka hutolewa na Wakili wa Serikali, na uendeshaji wake huzingatia taratibu zote za kisheria ikiwemo kupeleka mashahidi wa pande zote.
Hata hivyo, anaeleza namna ambavyo baadhi ya kesi huendeshwa kwa njia ya usiri mkubwa kutokana na unyeti wa taarifa wanazotuhumia nazo.
“Wakati mwingine wananchi wanalalamika kuwa kesi zinaendeshwa kwa usiri, ni kweli kuna mazingira lazima itokee hivyo kutokana na tuhuma za mtu au mashahidi wanaotakiwa kufika mbele ya baraza, na hii mbona ipo hata katika mahakama zingine kuwa wanaendesha kesi kwa usiri inapobidi,” amesema Kipacha.
Wajumbe wa baraza
Baraza linandwa na wajumbe watatu wanaoteuliwa na Rais ambapo mwenyekiti wake lazima atokane na jaji aliyehudumu kwa muda mrefu Mahakama Kuu,
Mahakama ya Rufani
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, wajumbe wengine wawili hutokana na pendekezo la Kamishna na watatu hao wanafanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa.
Wanaripoti kwa nani
“Baada ya kumaliza kesi, kamati huandaa taarifa ambayo hupelekwa kwa Kamishna wa maadili, yeye anawasilisha kwa Rais, Spika wa Bunge, taasisi ambayo mhusika anafanyia kazi na nakala kwa mtuhumiwa mwenyewe,” anasema Kipacha.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kamati inatoa mapendekezo ya moja kwa moja kwa mhusika kama afukuzwe kazi, ajiuzulu, abadirishwe, onyo kali au kuwajibishwa na ama adhabu nyingine inyofanana na hizo kulingana na uzito wa tukio.
Je imeshatokea
“Ndiyo, tena ni zaidi ya mara tano hivi nikikumbuka na kama nilivyokutajia kwenye kesi za Escrow ambapo mapendekezo yake yalifanyiwa kazi kwa sehemu kubwa na wahusika wakashughulikiwa,” anasema.
Hata hivyo anabainisha kuwa, hawezi kutaja ni akina nani waliowahi kupitia kwenye mkumbo huo kutokana na kuwa msemaji wa adhabu hizo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Changamoto
Palipo na mafanikio hapakosi changamoto, Sekretarieti ya Maadili ya Viongoni wa Umma inakutana na baadhi ya changamoto ikiwemo ujazaji fomu za madeni na mali kutokuwa sahihi.
Mengine ni malalamiko ya matumizi mabaya ya madaraka kutoka kwa viongozi waliopewa dhamana na ukiukwaji wa maadili kwenye viapo vya watumishi.
Changamoto nyingine ni kwa wanaotumbuliwa a kutoka katika utumishi ambao wanashindwa kutimiza takwa la kisheria la kutakiwa wajaze mali na madeni ndani ya siku 90 kabla ya kukoma utumishi lakini sekretarieti inakosa nguvu ya kuwafuatilia kutokana na kukoma ghafla utumishi.
Kuhusu mali kwa viongozi
“Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haimzuii kiongozi kuwa na mali ilimradi kuwe na uwazi alizipataje, lakini kwamba viongozi kumiliki mali, siyo kosa kabisa na haiwezi kuwa kosa,” anafafanua.
Kauli hiyo inaondoa sintofahamu ya siku nyingi miongoni mwa watu kuwa, viongozi wenye mali nyingi huwa wametenda makosa.
Katibu anasema kiongozi anayefanya shughuli zake kihalali na kwa uwazi mbele ya jamii anaweza kuwa na mali nyingi na isiwe tatizo lakini ikatokea mwenye mali kidogo kukawepo shida kama itathibitika kuna ujanjaujanja katika kuzitafuta.
Nini matamanio
Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma inataja matamanio yake kuwa, viongozi wangekuwa na misingi ya kiutumizi unaozingatia haki, ingesaidia kwa kiasi kikubwa Taifa kusonga mbele hata kiuchumi.
Wanasema kuwa, jamii ingejifunza ulipaji wa kodi bila shuruti kwa sababu kila jambo lingeongozwa na viongozi lakini kinyume cha hapo hakuna anayeweza kuamini kitu au mtu ikiwa hayupo kwenye orodha ya wanaoaminika.
Kingine alisema Watanzania wanaweza kuamini na kujenga tumaini kwa kiongozi ambaye wanaona yupo karibu na wananchi na anawasilisha lakini hali huwa tofauti kwa wasiofuata maadili kwani siku zote ni maadui wa watu.