Vifo vya mafuriko Hanang vyafikia 47, majeruhi 85

Baadhi ya askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji wa Mkoa wa Manyara, wakiwa juu ya paa za nyumba wakijaribu kuokoa watu kwenye maafa yaliyosababisha vifo 47 na majeruhi 85 kwenye kata za Gendabi na Katesh wilayani Hanang. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Vifo hivyo vimesababishwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Jumapili Desemba 3, 2023
Hanang. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema hadi kufikia saa 10 jioni leo Desemba 3, 2023 watu 47 wamefariki dunia na wengine 85 kujeruhiwa wilayani Hanang kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo.
Mvua hiyo ilisababisha sehemu ya Mlima Hanang kumomonyoka na kusababisha kutiririka kwa tope katika maeneo ya Katesh na Gendabi.
Sendiga amesema watu wengine wanahofiwa kufukiwa na tope baada ya nyumba na makazi yao kusombwa na mafuriko ya maporomoko ya udongo huo kutoka Mlima Hanang.
Akizungumza na waandishi wa habari amesema eneo kubwa lililoathiriwa na mafuriko hayo ni Kata ya Gendabi na katikati ya Mji wa Katesh ambayo ni makao makuu ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
"Nyumba za watu zimezingirwa na mafuriko na miti iliyosombwa na mafuriko kutoka sehemu ya mlima Hanang yamesababisha barabara ya Katesh kwenda Singida kushindwa kupitika," amesema Sendiga.
Mmoja kati ya wakazi wa Hanang, Stephen Samo amesema Serikali inapaswa kufanya marekebisho ya haraka ya miundombinu iliyoharibika.
"Barabara, nyumba zimeharibika pamoja na misaada mbalimbali ya makazi na vyakula kwa watu waliofikwa na janga hili," amesema Samo.
Mapema mchana leo, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko Dubai anakoshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ametoa pole kwa wananchi na waathirika wa mafuriko hayo huku akiagiza nguvu zote za Serikali zielekezwe katika eneo hilo kwa ajili ya uokozi na kuzuia maafa zaidi.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa kuhusu mvua kubwa iliyonyesha mkoani Manyara na kuleta madhara Katesh. Tunatoa pole kwa waathirika wa tukio hilo.
“Nimelekeza nguvu zote za Serikali zielekezwe katika uokozi ili kuzuia maafa mengi, sisi tulioko huku (Dubai) kushiriki mkutano wa mazingira tumesikitishwa na tukio hili, lakini ndio mipango ya Mungu inavyokwenda, tunatoa pole,” amesema Rais Samia.