Vifo vitokanavyo na Ebola vyavuka 1,000, mlipuko ukienea kwa kasi
Muktasari:
- Watu 1,000 wamefariki kutokana na Ebola nchini DRC huku maambukizi yakiongezeka kwa kasi. Uhaba wa chanjo, migogoro, upinzani wa jamii na changamoto za huduma za afya vinachochea mlipuko huo.
Kinshasa. Zaidi ya watu 1,000 wamefariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku mamlaka za afya barani Afrika zikionya hali kuwa mbaya zaidi iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dk Jean Kaseya, amesema hadi sasa vifo 1,031 vimethibitishwa katika mlipuko huo, ambao unaenea kwa kasi zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya ugonjwa huo.
Leo Alhamisi, Julai 23, 2025 Shirika la Habari la AP, limemnukuu Dk Kaseya kutoka Ghana akisema uhaba wa chanjo, dawa na fedha za kukabiliana na ugonjwa huo unachangia kuendelea kuongezeka kwa maambukizi na vifo.
"Hawa ni watu wanaopoteza maisha. Wanakufa kwa sababu hatuna chanjo, hatuna dawa na hatuna rasilimali za kutosha," amesema.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya DRC, hadi Jumatatu jumla ya wagonjwa 2,473 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa Ebola huku wasiopungua 737 wakiwa wamewekwa katika vituo vya kutengwa au kupatiwa matibabu hospitalini.
Mlipuko huo ulitangazwa rasmi Mei 15 mwaka huu na unatofautiana na milipuko mingine ya Ebola kutokana na kusababishwa na kirusi aina ya Bundibugyo, ambacho hadi sasa hakina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa.
WHO yaonya idadi kuongezeka
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya idadi halisi ya maambukizi inaweza kuwa mara mbili hadi nne zaidi ya takwimu rasmi kutokana na maeneo mengi ya mashariki mwa DRC kutofikika kirahisi kwa sababu ya mapigano yanayohusisha makundi ya waasi.
Maofisa wa afya pia wameeleza asilimia 80 ya maambukizi mapya yanatokea nje ya mnyororo unaojulikana wa maambukizi, jambo linaloashiria kuwa virusi vinaenea kwa kasi kuliko uwezo wa mamlaka za afya kufuatilia wagonjwa na watu waliokaribiana nao.
Jitihada za kudhibiti ugonjwa huo zimeendelea kukumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya jamii zinazokataa taratibu salama za mazishi na badala yake kuendelea na mila za jadi, hali inayoongeza hatari ya maambukizi.
Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Raia katika Jimbo la Ituri, Robert Ndjalonga, amesema changamoto kubwa ni baadhi ya wananchi kukataa kushirikiana na timu za afya.
Kutokana na hali hiyo, wakati mwingine timu za mazishi hulazimika kupewa ulinzi na vikosi vya usalama ili kuhakikisha mazishi yanafanyika kwa usalama bila vurugu.
Aidha, vituo vya afya na wahudumu wa mstari wa mbele wamekuwa wakishambuliwa, huku baadhi ya watumishi wakigoma wakidai kutolipwa mishahara tangu mlipuko huo uanze.
Wiki iliyopita, mfanyakazi mmoja wa timu ya mazishi salama alijeruhiwa baada ya watu wasiojulikana kurusha mawe kwenye gari lao mjini Bunia.
CDC imeeleza chini ya asilimia tisa ya watu waliokutana na wagonjwa waliothibitishwa kuugua Ebola ndiyo wanaofuatiliwa kwa sasa, kiwango ambacho ni cha chini sana kwa kudhibiti mlipuko huo.
Taasisi hiyo pia imebainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya vifo vinatokea katika jamii kabla wagonjwa hawajafikishwa kwenye vituo vya afya kwa ajili ya matibabu.
Msimamizi wa operesheni za kukabiliana na Ebola Taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma ya DRC, Pierre Akilimali, amesema idadi kubwa ya vifo vinavyotokea majumbani inaonyesha wagonjwa wengi hawagunduliwi mapema wala kutengwa kwa wakati, jambo linaloruhusu virusi kuendelea kuenea.
Onyo la wataalamu
Dk Kaseya ameonya bila kuongeza kasi ya hatua za kudhibiti ugonjwa huo, mlipuko wa sasa unaweza kuwa miongoni mwa milipuko mibaya zaidi ya Ebola kuwahi kurekodiwa duniani.