Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Wananchi wapewa mbinu kukabiliana na polisi wanaokamata watu ‘kihuni’

Muktasari:

  • RPC Safia Jongo amesema kumekuwa na matukio ya utekaji yanayodaiwa kufanywa na watu waliovaa sare za polisi wakiwa kwenye magari yanayodaiwa kuwa ya Serikali, lakini hawatoi uthibitisho wowote kwa wananchi, jambo linalotia hofu na kuathiri imani kwa vyombo vya dola.

Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita limetoa wito kwa wananchi kutokubali kukamatwa na mtu yeyote anayejitambulisha kama askari polisi bila kuonyesha kitambulisho cha utumishi na kueleza kituo cha polisi alichotoka.

Jeshi hilo limesema kitendo cha kutokuonyesha kitambulisho au kituo cha kazi ni kinyume cha sheria na kinaweza kutumika kama mbinu ya kuficha vitendo vya kihalifu.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Safia Jongo ametoa kauli hiyo Aprili 8, 2025, wakati wa mafunzo ya ulinzi shirikishi na polisi jamii yaliyotolewa kwa viongozi wa vijini, kata na tarafa.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa lengo la kuimarisha usalama wa wananchi.

Kamanda Jongo amesema kumekuwa na matukio ya utekaji yanayodaiwa kufanywa na watu waliovaa sare za polisi na kutumia magari yanayodaiwa kuwa ya Serikali, lakini bila kutoa uthibitisho wowote kwa wananchi.

Polisi watoa mbinu za kukabiliana na wasiojulikana

Hali hii inatia hofu na inaathiri imani ya wananchi kwa vyombo vya dola.

"Askari wa kweli anapokwenda kukamata mtu, lazima ajitambulishe kwa jina, awe na kitambulisho cha kazi na aseme anatoka kituo gani. Kama hana hivyo, huyo si askari ni mtu wa kawaida ambaye anaweza kuwa jambazi au mhalifu," amesema Kamanda Jongo.

Amesema wananchi wana haki ya kuuliza na kudai uthibitisho kabla ya kukubali kuchukuliwa au kupekuliwa na mtu anayedai kuwa askari.

Kamanda Jongo amesisitiza kuwa mtu yeyote anayeshindwa kujitambulisha hana mamlaka ya kumkamata raia.

Aidha, Kamanda Jongo ameeleza kuwa sheria inamtaka polisi anayeendesha upekuzi kwa mtu kuwa na mtu mzima wa kushuhudia, ingawa si lazima awe mwenyekiti au mtendaji wa kijiji, kutokana na kwamba kuna wakati ambapo mtu anayekamatwa ni ndugu wa mtuhumiwa.

Hivyo, askari anapaswa kuwa na mtu mzima anayeweza kujitambulisha, na pia lazima aonyeshe kitambulisho chake na hati ya upekuzi.

Akizungumzia dhana ya ulinzi shirikishi, Kamanda Jongo amesema ilianzishwa na Jeshi la Polisi ili kuwajengea uwezo wananchi kujilinda wenyewe, kwa sababu usalama wa mtu huanza na mtu mwenyewe.

Kamanda huyo amesema licha ya nia njema ya Jeshi la Polisi kuanzisha mfumo wa polisi jamii, wapo baadhi ya watu wanaokwenda kinyume na malengo hayo kwa kufanya vitendo viovu, ikiwemo kutumia nguvu kukamata watu, kudai rushwa, na wakati mwingine kuwafungia watu kwenye vituo vya polisi visivyo rasmi, kinyume na sheria.

Kamanda Jongo amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, watendaji wa kata na vikundi vya polisi jamii wanajengewa uwezo wa kuelewa misingi ya polisi jamii pamoja na mipaka ya majukumu yao.

Wakati huohuo, Kamanda Jongo amepiga marufuku watendaji wa kata au vijiji kufungua vituo bubu vya polisi kwenye ofisi zao na kuwakamata wahalifu, kuwaweka mahabusu kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Maelezo ya Kamanda Jongo yameungwa mkono na Dk Ezekiel Kyogo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kitengo cha ushirikishwaji wa jamii, ambaye amesema elimu inayotolewa inalenga kuwasaidia wananchi kuelewa wajibu wao na haki zao.

“Tunalenga kuwaelimisha wananchi kuwa ulinzi unaanzia kwao wenyewe. Polisi jamii au vikundi vya ulinzi wanapaswa kushirikiana kwa kufuata sheria, si kutumia nguvu wala kuwapiga watu,” amesema Dk Kyogo.

Ameongeza kuwa baadhi ya polisi jamii wamekuwa wakitumia vibaya nafasi zao kwa kupiga watu, kuwatisha, na hata kuwatoza fedha.

Dk Kyogo amesisitiza kuwa tabia hizo zinaharibu dhamira njema ya Jeshi la Polisi kuanzisha utaratibu wa ulinzi shirikishi.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Wilfred Willa pia kutoka Makao Makuu ya Jeshi, kitengo cha Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, amesema mafunzo hayo pia yanagusa uelewa kuhusu ukatili wa mtandaoni.

Ameeleza kuwa watu wengi wamekuwa wakifanya makosa bila kujua, kwa kuchapisha au kusambaza taarifa zinazodhalilisha wengine.

“Ipo tabia ya wazazi kuchapisha  picha za watoto wao mtandaoni wakiwa na nia njema, lakini wanasahau kuwa mtoto atakua na wadhifa wake tofauti na picha hiyo, na kwa sababu picha hiyo itakuwa inaishi mtandaoni, mwisho wa siku inaweza kumletea maudhi. Hivyo, unakuwa umemfanyia ukatili wa kijinsia,” alisema.

Pia, amewataka wananchi kuacha tabia ya kupiga picha hovyo na kuzituma kwenye mitandao ya kijamii bila ridhaa ya wahusika.

Martin Matiba, mmoja wa watendaji wa kata, amesema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha watendaji kupata uelewa mpana wa namna ya kushirikisha jamii katika masuala ya ulinzi bila kuvunja sheria.

Pia, alisema wanatakiwa kuhamasisha wananchi kuachana na tabia ya kujichukulia sheria mkononi.