Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Walivyoagwa sita waliofariki ajali ya ambulensi, toyo Mafinga

Mufindi. Miili ya watu sita kati ya wanane waliopoteza maisha katika ajali iliyohusisha gari la wagonjwa (ambulensi) na pikipiki ya miguu mitatu (Guta) imeagwa leo Aprili 21, 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Upendo, iliyoko katika Halmashauri ya Mji Mafinga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Vilio na simanzi vilitawala katika viwanja hivyo huku mamia ya waombolezaji wakiwa wamegubikwa na huzuni kubwa kutokana na ajali hiyo iliyoacha pengo kubwa katika familia husika.

Vilio vyatawala miili sita waliofariki ajali ya toyo, ambulance ikiagwa

Miili hiyo iliwasili katika viwanja hivyo kuanzia saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya shughuli ya pamoja ya kuuaga, kutokana na wote kuwa wakazi wa mtaa mmoja wa Amani.

Ajali hiyo ilitokea Aprili 19, 2025 saa 12:30 asubuhi, katika eneo la Luganga, barabara ya Mafinga-Mgololo na kusababisha vifo vya watu wanane, akiwemo dereva wa Guta, huku wengine 14 wakijeruhiwa.

Miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo  na kuagwa leo ni Latifa Joseph Ngela (18), Irene Msanga (55), Siamini Lukosi, Rukia Kasavaga (52), Jenipha Msigwa (42), na Anord Mbosso.

Wengine wawili waliopoteza maisha ni Jema Mbwilo (50) na Adofu Ndanzi (27), ambapo miili yao ilichukuliwa na ndugu kwa taratibu za mazishi ya kifamilia nyumbani.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani, Melkion Ndelwa, amesema ajali hiyo ni pigo kubwa kwa mtaa huo, kwani waliofariki wote walikuwa wakazi wa eneo hilo.

“Kwa siku moja tulipoteza watu saba, na kesho yake, Jumapili, tukampoteza dereva wa Guta ambaye alikuwa akiendelea na matibabu. Hili ni jambo la kutisha,” amesema Ndelwa huku akishukuru Serikali kwa msaada wa haraka uliotolewa baada ya ajali kutokea.

Kwa upande wake, mtoto wa marehemu Rukia Kasavaga, Hawa Mvinga, amesema taarifa za kifo cha mama yao zilipokelewa kwa mshtuko na huzuni kubwa.

“Mama yetu alikuwa kila kitu kwetu. Tangu tumepoteza baba, yeye ndiye aliyekuwa nguzo ya familia. Amekuwa akijitahidi kuhakikisha tunapata maisha mazuri. Kifo chake kimetuacha kwenye huzuni kubwa sana,” amesema kwa majonzi Mvinga.

Akizungumza katika viwanja vya shule hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa amesema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wanane, akiwemo dereva wa Guta, Adofu Ndanzi, ambaye alifariki dunia akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Wengine 14 waliobaki bado wanaendelea na matibabu hospitalini.

“Guta hiyo ilikuwa imebeba watu 22, jambo ambalo si la kawaida na si salama kabisa. Watu sita walifariki dunia papo hapo, wawili walifariki dunia baadaye wakiwa hospitali akiwemo dereva wa Guta. Majeruhi wawili walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, na wengine saba walihamishiwa Hospitali ya Ipamba," amesema Dk. Salekwa.

Aidha, amekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni kwamba watu 15 wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo, akisisitiza kuwa waliothibitishwa kufariki hadi sasa ni watu wanane.

“Kama mnavyoona, hapa mbele yetu tuna miili ya watu sita, na mingine miwili ilishachukuliwa na ndugu kwa taratibu nyingine. Tunawaomba wananchi wawe na utulivu na waache kusambaza taarifa zisizo sahihi,” ameongeza Dk. Salekwa.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kuwa waangalifu na kuzingatia usalama wao wanapoelekea kwenye shughuli za kujitafutia kipato, ikiwemo kuepuka kusafiri kwenye vyombo visivyo rasmi au visivyokidhi vigezo vya usafiri salama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi, ametoa pole kwa familia zilizofiwa na kupongeza jitihada za madaktari wa Hospitali ya Mji wa Mafinga kwa juhudi walizofanya kuwaokoa majeruhi wa ajali hiyo.

“Nawashukuru pia wananchi wa Mafinga kwa namna walivyojitokeza kusaidia kwa hali na mali baada ya ajali hiyo kutokea, ikiwemo kutoa misaada ya haraka kwa majeruhi,” amesema Chumi.

Naye Diwani wa Kata ya Upendo, Michael Msite, amewashukuru wananchi kwa mshikamano waliouonyesha tangu tukio hilo kutokea.

“Nawashukuru sana kwa upendo na mshikamano mlioonyesha. Hili ni jambo zito na la kuhuzunisha sana. Kupoteza ndugu wote kwa ajali ya aina hii ni jambo la kuumiza mno,” alisema Msite huku akihimiza wananchi kuendelea kuwaombea majeruhi waliopo hospitalini.”

Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi, George Kavenuke, ameiomba Serikali kupitia vyombo vya usalama barabarani kuendelea kutoa elimu na maelekezo kwa madereva wa vyombo vya moto juu ya kuzingatia sheria za usalama barabarani.

“Tuwe na utaratibu wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva, pamoja na wamiliki wa vyombo hivi. Tukifanya hivyo, tutaepusha ajali kama hizi ambazo zinasababisha vifo vya watu wengi,” amesema Kavenuke.