Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Simulizi ya tabibu aliyevuka mto yaacha gumzo mtandaoni

Dodoma. Upo msemo wa Kiswahili unaosema, “bora punda afe lakini mzigo ufike,” ukimaanisha ni lazima jambo lifanikiwe kwa njia yoyote.

Usemi huo unashabihiana na picha jongefu iliyokuwa ikimuonyesha Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mpendo, wilayani Chemba Mkoa wa Dodoma, Hassan Ahmadi akivuka Mto Bubu.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mpendo Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma, Hassan Ahmadi aliyevuka Mto Bubu na sanduku la chanjo.

Mganga mfawidhi huyo alikuwa amebeba sanduku la chanjo ya surua na rubella, akitokea Kijiji cha Mpendo kuelekea Kijiji cha Hamai.

Picha hiyo iliyosambaa katika mitandao ya jamii ilimuibua Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu baada ya kuambatanishwa (tag) na aliyekuwa Rais wa Chama cha Madaktari (MAT) mwaka 2020, Dk Elisha Osati katika mtandao wa X, zamani twitter.

Dk Osati aliweka picha hiyo na kuandika, “Vyovyote vile chanjo lazima ifike, surua na rubella.”

Akionyesha kuguswa, Waziri Ummy aliandika katika mtandao huo, “sijui ni halmashauri gani hii, hakika mtumishi huyu anapaswa kupongezwa. Katibu Mkuu wa Afya wamtafute. Lakini pia, viongozi tunapaswa kufanya kitu ili kuboresha mawasiliano kuwezesha wananchi kupata huduma za afya.”

Kutokana na tukio hilo, Mwananchi ilimtafuta mganga mfawidhi huyo, anayehudumia vijiji vya Hamai, Mpendo, Kubi na Mwagungu, ambaye anasema alianza kufanya kazi Kituo cha Afya Jogolo, wilayani Chemba mwaka 2018.
Anasema alifanya kazi kwa mwaka mmoja katika kituo hicho kabla ya kuomba uhamisho wa hiari kwenda katika Zahanati ya Mpendo.

Anasema alifanya uamuzi huo baada ya kuona Kijiji cha Jogolo kilikuwa na watu wachache kuliko Mpendo, kilichokuwa na idadi kubwa ya watu lakini kilikuwa hakina daktari wala tabibu.

Ahmadi, ambaye pia ni tabibu, anasema katika zahanati hiyo wako watumishi wanne wanaohudumia, tabibu akiwa peke yake wengine ni wahudumu wa afya.

Anasema Serikali ilitangaza kampeni ya chanjo ya surua na rubella iliyoanza Februari 15, 2024 na walijipanga kuchanja maeneo yote wanayoyahudumia, kwa sababu katika baadhi ya maeneo kulianza kulipuka ugonjwa wa surua, hasa Kijiji cha Hamia.

SIMULIZI YA TABIBU ALIYEVUKA MTO NA SANDUKU KUPELEKA CHANJO KIJIJINI

“Baada ya kushauriana na timu yangu tukakubaliana kutengeneza mkakati utakaohakikisha watoto wote wanapata chanjo. Tuliona kampeni hii ni fursa ya kila mtoto mwenye umri wa kupata chanjo, anaipata kwa muda stahiki,” anasema.

Anasema watumishi wengine walikwenda maeneo mengine, lakini yeye alikwenda Hamai, ndipo ilipomlazimu kuvuka Mto Bubu ili kukifikia kijiji hicho.


Ahmadi anasema ilimlazimu kuvuka mto huo kwa sababu hiyo ilikuwa ni kampeni na mazingira ya maeneo mengi sio mazuri.

“Hawa watu wa Hamai hawana watu wengine pale wanaoweza kuwapatia chanjo, sisi ndio tunaowahudumia, kwa hiyo ililazimika kutumia nguvu zozote kuhakikisha hawa wanapata huduma,” anasema Ahmadi, aliyefanya kazi hiyo kwa siku mbili katika Kijiji cha Hamai kuanzia Februari 15 hadi 16, 2024. Anasema alipofika katika mto huo, kwanza alivusha nguo zake kisha kurudia sanduku la chanjo.

Ahmadi anasema kuna hatari angeweza kukutana nazo wakati anavuka mto, lakini kwa mtumishi wa afya yapo mazingira hatari mengine wanayokabiliana nayo.

Anatoa mfano waliokwenda kuwahudumia wagonjwa wa Ebola au wanaohudumia wenye kipindupindu, wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira hatarishi.

“Watu wasione kupita kwenye mto ni risk (hatarishi), zipo nyingi sana kwa sisi watoa huduma za afya…Tusitengeneze mazingira fulani ili kukwepa kutimiza wajibu wetu, hapana. Wewe kama Mungu hajakupangia utakufa kwa tatizo hilo haliwezi kukupata,” anasema tabibu huyo.Anasema haikuwa mara ya kwanza kuvuka mto huo, bali hata kwa mwaka 2020 alifanya hivyo kwa kumvusha mjamzito aliyekuwa na uzazi pingamizi.

Ahmadi anasema mbali na changamoto hiyo, wamekuwa wakikutana na tembo wakati wa kiangazi wanapokwenda kutoa huduma.

“Siku moja tulikimbia wote na kuacha pikipiki barabarani baada ya kukutana na tembo wakikatiza. Kutoka Mpendo kwenda Kijiji cha Mangungu; wakati wa kiangazi tembo wanapita sana. Ukikutana nao inabidi utulie tembo wapite ili uendelee na safari.” Anasema kampeni hiyo ilifanikiwa kwa sababu walipewa lengo la kuchanja watoto wenye umri wa kati ya miezi tisa hadi miaka mitano 1,940, lakini waliwachanja watoto 2,404.


Ugumu kufika Kijiji cha Mpendo

Ahmadi anasema vipindi viwili vya kiangazi na mvua ndivyo vinaamua utafikaje kwenye kijiji hicho.

Anasema kipindi cha kiangazi unaweza kukatisha Mto Bubu kwa kuwa maji yanakuwa yamekauka, lakini wakati wa mvua inakulazimu kupitia Manyoni mkoani Singida kama unataka kwenda makao makuu ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

“Kama unatokea Mpendo kwenda Makao Makuu ya Wilaya Chemba, inakupasa kwenda hadi Manyoni, unakuja Bahi (Dodoma), halafu Dodoma Mjini halafu Chamwino na kisha Chemba,” anasema.

Anasema mvua zikinyesha hakuna gari inayoweza kupita, hivyo inawalazimu kusafiri kwa bodaboda umbali wa kilomita 35 kutoka Kijiji cha Mpendo hadi Kintinku (wilayani Manyoni) ili kupata gari za kwenda Dodoma Mjini.

Anasema gharama za kukodisha bodaboda huwa ni kati ya Sh18,000 hadi Sh25,000, huku nauli ya kutoka Manyoni hadi Dodoma Mjini ikiwa ni Sh4,000 na Dodoma Mjini hadi Chemba ni Sh7,000.

Ahmadi anasema wagonjwa wanaowahudumia wanapatiwa rufaa za kwenda Kituo cha Afya Kintinku kilichopo Manyoni chenye umbali wa kilomita 35 kutoka Mpendo. Anasema kituo hicho kipo karibu ukilinganisha na kile cha Mtoro kilichopo Wilaya ya Chemba ambacho umbali ni kilometa 60 kutoka zahanati anayoisimamia.

Hata hivyo, wakati wa mvua mara nyingi njia hazipitiki, hivyo kulazimika kutumia bodaboda.

Anaishukuru Serikali kujenga madaraja katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitiririsha maji mengi wakati wa mvua, lakini hata hivyo anasema bado kuna maeneo hayapitiki, hivyo kuwalazimu kuwabeba wagonjwa.


Aliwahi kupewa tuzo

Julai 14, 2022, Taasisi ya Benjamin Mkapa ilimpatia cheti cha kutambua mchango wake wa kuhudumia jamii kwenye vijiji anavyofanyia kazi.
Cheti hicho alikabidhiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Kongamano la Kumbukizi ya Hayati Benjamin William Mkapa, lililofanyika Zanzibar.

Alipoulizwa ni nini kilifanya kutunukiwa cheti hiyo, Ahmadi anasema alipoingia katika kijiji hicho mwaka 2019, alikutana na changamoto za afya.
Anasema idadi kubwa ya wajawazito walijifungulia nyumbani kutokana na kutokuwepo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Changamoto nyingine anasema ni uelewa hafifu wa elimu ya afya kwenye jamii na wananchi kutembea umbali mrefu, takribani kilomita 18 kufuata kituo cha kutolea huduma.

Anasema hatua alizochukua yeye akiwa msimamizi na wahudumu wengine ya afya ni kutoa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

“Tulishirikiana pia na kamati ya huduma za jamii pamoja na Serikali ya kijiji kuhakikisha kila mjamzito anajifungulia kwenye kituo cha kutolea huduma,” anasema tabibu huyo.

Anasema kupitia mikakati hiyo, kuliongeza wajawazito wanaojifungulia kituoni na mwaka 2020 baada ya mafunzo ya wahudumu ngazi ya jamii idadi ya waliojifungulia kituoni ilifikia 337 mwaka 2020 kutoka 182 kwa mwaka.

Anasema kwa hatua hiyo, walipata nafasi ya kwanza kiwilaya kwa zahanati zote za Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.

Ahmadi anasema idadi ya wanaojifungulia kituoni imeendelea kuongezeka na mwaka 2021 walifikia 401, ukilinganisha na lengo la wanawake 312.
 

Ombi kwa Serikali

Ahmadi anaiomba Serikali kuboresha barabara inayotoka Kijiji cha Mpendo kwenda Kintinku ili wananchi waweze kupata huduma wakati wa kiangazi na mvua.

Pia, anaomba ijenge kituo cha afya katika kijiji hicho kilichopo Kata ya Mpendo ili wananchi wapate huduma hiyo karibu.

Pia, anaiomba Serikali ijenge daraja katika Mto Bubu ili njia hiyo inaowaunganisha na makao makuu ya Wilaya ya Chemba ipitike wakati wote badala ya kuzungukia mkoani Singida.