Mwarobaini mafuriko Barabara Morogoro - Dodoma wapatikana

Magari yakiwa yamekwama kwenye barabara ya Moro -Dodoma eneo la Mtanana baada ya maji kukatiza kwenye barabara hiyo. Picha na maktaba
Muktasari:
- Wakati magari yakikwama kwenye eneo la Mtanana katika Barabara ya Morogoro kwenda Dodoma kutokana na mafuriko, Serikali imeshaaza mkakati wa kuiboresha barabara hiyo ili ipitike wakati wote.
Kongwa. Kufuatia kero ya mafuriko yanayosababisha kufungwa kwa Barabara ya Morogoro -Dodoma eneo la Mtanana Kibaigwa wilayani Kongwa kila mvua inaponyesha, Serikali imeanza kuchukua hatua ya kujenga upya eneo hilo.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ujenzi, Balozi Aisha Amour aliyetembelea eneo hilo leo Januari 30,2024 akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri.
“Tuliifunga barabara hii kwa saa tatu ili kujiridhisha na uimara wake kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hili na mikoa ya jirani na kusababisha maji kupita juu ya barabara”, amesema Balozi Amour.
Akieleza hatua zilizochukuliwa, Balozi Amour amesema tayari mkandarasi amepatikana, fedha zimetengwa na vifaa kwa ajili ya kujenga barabara na madaraja makubwa katika eneo la Mtanana- Kibaigwa yenye urefu wa kilomita sita baada ya mvua kwisha.
“Tumedhamiria kumaliza tatizo hili kwa kujenga hizi kilomita sita kati ya Mtanana hadi Kibaigwa kwa kuweka madaraja makubwa na kuongeza upana wa barabara ili kudhibiti changamoto ya kila mwaka katika eneo hili,” amesisitiza Balozi Amour.
Amesema kazi inayoendelea kwa sasa ni kuimarisha kingo za barabara ili mafuriko yanayotokea sasa yasibomoe barabara na kuhatarisha huduma ya usafiri katika eneo hilo.
Amemtaka Meneja wa Tarnroads Mkoa wa Dodoma kushirikiana na wananchi na viongozi ili eneo hilo lipitike mchana na usiku, na kuzuia kwa muda huduma za usafirihaji pale maji yanapozidi ili kulinda usalama wa watu na mali zao.
Mweri amesema Serikali itajenga mabwawa katika eneo hilo ili kuhakikisha maji yote yanayopita katika yanavunwa na kutumiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo katika kipindi chote cha mwaka.
“Tutahakikisha mabwawa haya yanajengwa kwa haraka ili kuwawezesha wananchi wa eneo hili kunufaika na uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara katika kipindi chote cha mwaka, na hivyo kukuza uchumi wao,” amesisitiza.
Ukaguzi wa makatibu wakuu hao katika eneo unafuatia ziara ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa katika eneo hilo ambapo alisisitiza umuhimu wa makatibu wakuu wa Wizara za Kilimo na Ujenzi kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa eneo hilo.
Barabara hiyo licha ya kutumiwa na magari yanayofanya safari zake kanda ya kati, ziwa na nje ya nchi, mapema leo asubuhi vyombo hivyo vya usafiri vililazimika kuegeshwa kupisha mafuriko yanayotokana na mvua zilionyesha Januari 30, 2024.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wasafiri wanaotumia barabara hiyo, Isacky Raphael amesema ingawa alifika Kibaigwa magari yakiwa yameruhusiwa saa 7:00 mchana, alilazimika kusubiri kwa saa mbili kuruhusiwa kupita kutokana na foleni.
"Hapa watu wanatumia barabara upande mmoja tu, kwa hiyo ilitupasa kusubiri kwanza wapite waliokuwa mbele yetu ili nasi tuweze kupita," amesema Raphael.