VIDEO: Serikali yafumua masharti saba bima ya afya kwa wote
Muktasari:
- Miaka 16 ya mchakato wa maandalizi ya Bima ya Afya kwa Wote (UHC) huenda ukahitimishwa katika Bunge litakaloanza mwishoni mwa mwezi ujao Wizara ya Afya itakaposoma muswada wake kwa mara ya pili.
Dar es Salaam. Miaka 16 ya mchakato wa maandalizi ya Bima ya Afya kwa Wote (UHC) huenda ukahitimishwa katika Bunge litakaloanza mwishoni mwa mwezi ujao Wizara ya Afya itakaposoma muswada wake kwa mara ya pili.
Muswada huo utasomwa tena bungeni baada ya kutojadiliwa na kupitishwa katika mkutano wa tisa uliofanyika mwezi uliopita kwa kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa chanzo cha fedha kitakachouwezesha utaratibu huo kuwa endelevu.
Swali kubwa lililozusha mjadala ndani na nje ya Bunge ni namna gani wasio na uwezo watakavyohudumiwa na mfuko huo lakini taarifa ilizozipata Mwananchi zinaeleza kuwa unakuja na mabadiliko makubwa ikiwamo kuondolewa kwa baadhi ya huduma zilizokuwa zimefungamanishwa nayo ikiwamo pasi ya kusafiria, namba ya mlipakodi (TIN), usajili wa laini za simu na kitambulisho cha Taifa.
Maboresho mengine ni kuwapo kwa bima mbili, moja itakayomwezesha mtu kutibiwa katika hospitali za Serikali na binafsi popote alipo na bima ya kitita cha huduma za msingi itakayomwezesha kutibiwa katika zahanati, kituo cha afya au hospitali ya wilaya popote nchini ikigharamu kati ya Sh50,000 mpaka Sh60,000.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema safari ilikuwa ngumu kwa kuwa inahitaji kushirikisha wadau sambamba na chanzo cha uhakika cha fedha za kuifanikisha.
Alifafanua kuwa wameshayafanyia kazi maoni ya wadau hivyo wanarudi tena bungeni kwa ajili ya kwenda mbele na muswada ili sheria ipitishwe.
“Tulikwama lakini tunarudi bungeni Januari, katika muswada ule wa sheria ile tunapendekeza ianze kufanya kazi kuanzia Julai mosi mwaka 2023,” alisema.
Alifafanua kuwa Serikali imepanga kwenda hatua kwa hatua. “Yaani siyo tukianza tu basi hupati huduma zilizofungamanishwa, tunaenda kuangalia makundi maalumu na kwenye hii bima tunataka kupunguza watu wanaojiunga mmoja mmoja lengo wajiunge kama kaya ili hawa sita waweze kumgharamia yeyote atakayeumwa ndani ya familia,” alisema Waziri Ummy.
Ummy alisema suala hilo lazima likamilike mwaka 2023 kwani lipo katika vipaumbele vikuu viwili vya wizara yake ikiwamo kuhakikisha ubora wa huduma.
“Kipaumbele chetu kwa mwaka 2023 kitajikita katika maeneo makuu mawili, ubora wa huduma na ugharimiaji wa huduma za afya kwa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha kwa kuhakikisha bima ya afya kwa wote inakuwepo,” alisema.
Kusuasua
Waziri Ummy alisema safari ya kusaka bima ya afya kwa wote Tanzania ilianza takriban miaka 16 iliyopita lakini mchakato ulipata kasi wakati wa kutengeneza Maendeleo Endelevu (SDG) kupitia lengo namba tatu.
Alisema wakati wa kutengeneza malengo hayo kulikuwa na vipaumbele na sekta ya afya ilikuwa ni lazima kila nchi kuhakikisha wananchi wake wote wanapata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha na vituo vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma stahiki.

Waziri wa Afya, UmmyMwalimuakizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi wakati wa mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam. Picha na Ericky Boniphace
“Mchakato ulishika kasi mwaka 2016 na kuliandaliwa nyaraka kwa sababu mchakato wa kutengeneza sheria nchini unataka kuwe na waraka wa baraza la mawaziri ambao unapitia kwa wataalamu kwa kushirikisha wadau na baada ya hapo kamati ya makatibu wakuu wa wizara zote wanaosimamiwa na katibu mkuu kiongozi. Waraka ulifanikiwa kufika kwenye baraza la mawaziri mwaka 2021 kwa mara ya kwanza lakini kwa muda mrefu ulikuwa unakwama huku chini,” alisema Ummy.
Waziri pia alisema baada ya baraza la mawaziri kuupitia lilitoa maoni yaliyofanyiwa kazi kabla ya waraka kurudi tena kwa mara ya pili Septemba 2022.
“Tukaruhusiwa kuendelea, ndipo tukatengeneza muswada wa sheria Septemba na katika mkutano wa Novemba tukaenda nao bungeni na kamati ikajadili. Kamati iliita wataalamu tukapata maoni na michango yao mbalimbali,” alisema.
Waziri alifafanua kuwa wakati wanataka kuusoma kwa mara ya pili, kutokana na maoni yaliyopatikana, Serikali iliamua kuuondoa.
“Nafurahi kusema kwamba tumeshayafanyia kazi maoni ya wadau kwa hiyo tunarudi tena bungeni Januari tukitaraji kwenda mbele na muswada huu,” alisema.
Ugumu uliokuwapo
Katika mahojiano hayo maalumu, Waziri wa Afya alieleza ugumu uliokuwepo kufika walipo wanapoamini mambo yanaelekea kuwa sawa.
“Hata ukifuatilia uchaguzi wa Marekani au Uingereza, watu wanabishana kuhusu bima ya afya kwa wote. Hili si jambo rahisi, lakini limethibitishwa pasi na shaka kwamba ili wananchi wapate huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha ni muhimu kuwa na huu utaratibu wa bima ya afya ila mnaifanya vipi ndiyo kilikuwa kikwazo,” alisema.
Kuwapata watu wasio wagonjwa kuchangia huduma alisema ilikuwa kati ya changamoto zilizoibuliwa lakini kupitia uzoefu wa kuendesha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ni lazima kwa watumishi wote wa umma uliwasaidia kupata majibu ya uhakika.
Katika kuhakikisha bima ya afya kwa wote inaridhiwa, alisema Serikali iliamua kubadilisha Sheria ya NHIF iliyokuwa bima ya afya ya watumishi wa umma kwa kuwa inao wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata matibabu hata kama hawana fedha.
“Ndipo Serikali ikaweka utaratibu wa watu kuchangia kwa hiyari lakini kwa bahati mbaya Tanzania wanaojiunga kwa hiyari asilimia 90 ni wagonjwa, tunaona mtu anachangia Sh100 lakini anatumia mpaka Sh300,” alisema.
Kilichosababisha mchakato huo kuchelewa, alisema ni mashauriano ya ndani yaliyokuwapo kati ya Serikali na wadau.
“Wataalamu wakaona wanaoumwa na wasioumwa wote wajiunge ndiyo maana kwenye muswada mkaona ukitaka leseni ya udereva uwe na bima ya afya, pasi ya kusafiria, leseni ya biashara, kitambulisho cha uraia, namba ya mlipa kodi hivi vyote tukavifungamanisha kwa kujifunza kwa nchi zilizofanikiwa. Lakini baada ya kupata maoni na ushauri wa wananchi tumepunguza baadhi ya masharti na kuondoa huduma kadhaa zilizofungamanishwa kikiwamo kitambulisho cha Taifa, pasipoti, leseni ya biashara, kusajili namba ya simu ambavyo vilikuwa na malalamiko mengi,” alisema Ummy.
Alifafanua kuwa wameondoa namba ya mlipakodi inayomwezesha mtu kulipa kodi hivyo waliona itakuwa kikwazo kwa Serikali kukusanya mapato mengi. Hata ulazima kwa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha tano kujiandikisha ilionekana sharti hilo litakwaza wanafunzi kusajiliwa.
“Hilo lilikuwepo hasa vyuoni lazima alipe ada ya matibabu na mara nyingi hazitumiki ipasavyo, tumebakisha leseni ya biashara, usajili vyombo vya moto na kusajili wanafunzi vyuoni. Ni hivyo vitu vichache tu,” alisema.
Maoni yaliyotikisa
Waziri Ummy alitaja maoni yaliyotikisa zaidi muswada huo na kusababisha ukaahirishwa kuwa ni ulazima na utaratibu wa wasio na uwezo kupata huduma.
“Unaposema ni lazima kwa mujibu wa sheria za kimataifa ni muhimu tuwaingize wasio na uwezo na jambo husika ambalo Wizara ya Afya peke yake tulikuwa hatuwezi kulifanya zaidi ya kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mipango kwani kwa mujibu wa takwimu inaonyesha asilimia 26 wanaishi chini ya dola moja na tulikuwa tunatumia takwimu za sensa ya mwaka 2012. Ukisema ni lazima kunaweza kufanyika upotoshaji kwamba Serikali inaanzisha tozo nyingine wakati ni manufaa ya mtu mwingine kwa hiyo tulikuwa hatujatoa elimu ya kutosha kwa wananchi,” alisema waziri.
Ummy alisema vyombo vya habari vimesaidia kuibua mjadala zaidi kwani mpaka wanasiasa wa vyama vya upinzani waliiweka kama moja ya sera zao ingawa ilikuwapo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Wananchi wameonyesha kuuhitaji huu mfumo. Maoni mengi yakiwamo ya wabunge yalijielekeza sehemu kubwa mbili, kwanza ni ulazima. Unaposema lazima tunafanyaje wengine walisema ifungamanishe mpaka vyeti vya ndoa, mnaona tumeondoa maeneo mengi ambayo labda wengine wanadhani tungeweza kupata wananchi wengi wasio wagonjwa. Tumeangalia bima ya afya ni mchakato, kwa mfano wenzetu Marekani imewachukua miaka 100 kujadili bima ya afya kwa hiyo sisi tumeona bora tuanze huko mbele jinsi itakavyopokelewa na utekelezaji utakavyofanyika,” alisema.
Waziri Ummy alitaja eneo la pili ni la wasio na uwezo. Kwamba kuwe na utaratibu wa kuchukua kadi za msamaha lakini kwa maoni ya wabunge basi Serikali ianzishe mfuko kwa kuangalia vyanzo mbalimbali kama kodi za makosa ya pombe, sukari au sigara kuwagharamia wasio na uwezo.
Aliitolea mfano Ghana ambayo asilimia 2.5 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inaingia kwenye mfuko huo hata Rwanda waliofanikiwa zaidi.
Maoni mengine ilikuwa ni kiwango cha uchangiaji ambacho walitumia uzoefu wa NHIF ambayo imekuwa ikitoa huduma kwa wanufaika milioni 4.8 lakini haikuwa sahihi kupanga kiwango kabla ya kukubaliana kwenye misingi.
“Kwenye hili maoni yalitolewa kuwa huenda Watanzania watashindwa kumudu gharama katika hospitali za umma hata binafsi, ikaja hoja kwamba utaratibu wa bima ya afya ya jamii uwepo. Wanufaika watachagua, ukitaka bima kwa ajili ya huduma zinazotolewa kwenye hospitali za Serikali au binafsi, utalipia kiwango fulani. Pia, tutakuja na utaratibu wa bima ya afya ya kitita cha huduma za msingi mtu atapata huduma katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya na hospitali ya halmashauri au wilaya kwa Sh60,000 tu,” alisema.
Alifafanua kuwa suala la huduma za jamii ndilo lililoleta maoni mengi zaidi lakini mwisho walikubaliana kuanza mchakato na baada ya miaka mitatu mpaka mitano wataona namna gani wanaweza kurekebisha mapungufu yatakayokuwa yamejitokeza.
Waziri Ummy alisisitiza kuwa haitokuwa jinai kwa mtu kutokuwa na bima ya afya.
“Wengine wamesema itakuwa lazima na usipokuwa nayo ni jinai na unaadhibiwa, sisi tumeona tutajaza watu kwenye magereza ndiyo maana tumekuja na hii kuifungamanisha na baadhi ya huduma zitakazokutaka uwe na bima lakini zaidi tutatoa elimu,” alisema.
Alisema katika hilo ni muhimu kwa wananchi wenyewe kujitathmini kama ni lazima kutumia fedha nyingi kujitibu wakiumwa au kulipia bima ya afya mapema.
“Lazima Watanzania tubadili tabia na kujenga utamaduni wa kuwa na bima ya afya, matibabu hivi sasa yanahitaji fedha nyingi lakini kuwa na bima ya afya, wasioumwa wanakuwa wamemchangia anayeumwa kupata huduma bora anazostahili tena kwa wakati,” alisema Ummy.