Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Mama afunguka sakata mwanafunzi aliyedaiwa kufa kwa kipigo

Jonathan Stephano Makanyaga (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Mrupanga, enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Wakati Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, likikabidhi kwa familia mwili wa Jonathan Makanyaga(6), anayedaiwa kufa kutokana na kipigo kutoka kwa mmoja wa mwalimu tarajali wa mafunzo ya ualimu (BTP), tayari shauri hilo limepelekwa Ofisi ya DPP kwa ajili ya kulitolea maamuzi ya kisheria.

Moshi. Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, limekabidhi kwa familia mwili wa Jonathan Makanyaga (6), mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mrupanga, anayedaiwa kufa kutokana na kipigo kutoka kwa mmoja wa mwalimu tarajali wa mafunzo ya ualimu (BTP),  aliyekuwa akifundisha shuleni hapo.

Wakati huohuo jeshi hilo limesema tayari shauri hilo limepelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulitolea uamuzi ya kisheria.

Mwanafunzi huyo, alifariki dunia Machi 10, 2024 katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) alikokuwa amelazwa kwa matibabu baada ya kudaiwa  kujeruhiwa na mwalimu kwa fimbo Februari 28, 2024,  hali iliyomsababishia majeraha sehemu mbalimbali mwilini na kusababisha kuvuja damu puani na mdomoni.

Mpaka sasa, walimu tarajali wa mafunzo ya ualimu watano wanashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa mahojiano wakidaiwa kuhusika na kifo cha mwanafunzi huyo ambaye mwili wake unatarajiwa kuzikwa kesho Machi 16,  2024 kijijini kwao Kimanganuni, Kata ya Uru Kusini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi ya kidaktari (postmoterm) iliyofanyika katika hospitali ya KCMC, kwa mujibu wa taarifa ya mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Janeth Shayo, amesema familia wameambiwa kifo cha mtoto wao huyo kimetokana na changamoto ya saratani ya damu.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoani hapa, Simon Maigwa amesema uchunguzi wa tukio hilo umekamilika na  shauri limepelekwa ofisi ya Mashtaka kwa ajili ya kulitolea uamuzi wa kisheria.

"Bado tunaendelea kuwashikilia walimu tarajali watano wa mafunzo ya ualimu kwa mahojiano baada ya kuripotiwa kwa tukio hili. Inadaiwa, mwanafunzi huyo aliadhibiwa na walimu hao kwa fimbo Februari 28, mwaka huu na kisha kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC bila kutoka taarifa Polisi na huyu mwanafunzi amefariki Machi10 akiwa anapatiwa matibabu hospitalini hapo.

“Jeshi la polisi lilipopokea taarifa ya kufariki kwa mwanafunzi huyo, tulianza uchunguzi mara moja, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa walimu hao, mwili wa mwanafunzi umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi,” amesema Kamanda Maigwa.


Mama alivyopokea majibu ya postmortem

Hata hivyo, mama wa mwanafunzi huyo, Janeth Shayo ameeleza namna alivyosikitishwa na majibu ya postmortem na kusema huenda ni kutokana na umaskini wa familia yao na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuisaidia familia hiyo, ili wapate haki ya mtoto wao.

Mama afunguka sakata mwanaye aliyedaiwa kufa kwa kipigo shuleni

"Majibu yametoka nimeambiwa mtoto wangu alikuwa anaumwa saratani, sijaridhika na majibu, mtoto wangu hakuwahi kuumwa saratani na kwenye familia hakuna mtu mwenye changamoto hiyo, iweje leo wasema mwanangu amekufa kwa saratani?

“Huyu mtoto tangu nimzae hajawahi kuumwa ugonjwa wowote ule ama kulazwa naye hospitali, cha ajabu zaidi ninavyojua mtu mwenye saratani ya damu akijikata sehemu yoyote damu inaganda, mtoto wangu anaweza akakata kidole akichonga  embe ama kujikwaa damu zinatoka na anapona, angekuwa na tatizo la saratani ya damu si ingekuwa ni changamoto, iweje leo, niambie mwanangu amekufa kwa saratani?­­­"

"Mwanzoni nilipofika hospitali ya KCMC mwanangu alifanyiwa (full blood picture) na waliniambia ni ini au bandama ndio ina shida, baadaye wakaniambia hakuna shida yoyote. Hapo kwa kweli nilibaki njia panda na nilikosa cha kusema," amesema.

Ameongeza kuwa, "Natamani hii changamoto  ninayopitia imfikie Rais wangu, mama Samia Suluhu Hassan maana kama nilishuhudia mwanangu alivyoumizwa kwa fimbo mwilini na mwalimu aliyempiga mwanangu nilipofika naye shuleni  alionyesha, halafu naambiwa amekufa kwa saratani ya damu? Naumwa sana, maana mwanangu kauliwa kikatili,"

"Laiti ningekuwa na uwezo haki ya mwanangu ingepatikana, lakini kwa vile wameziona sina uwezo wala chochote ndio maana wameamua kulifunika hili tukio na kutuachia majeraha yasiyopona sisi familia," amesema na kuongeza;

"Ingekuwa mtoto wangu hajaumizwa mwalimu mkuu na msaidizi wake wasingenipa ile  Sh80,000 nimkimbize hospitali baada ya kuumizwa kwa viboko hapo shuleni?

"Hospitali zote nilizopita madaktari waliokuwa wanamhudumia wanashangaa namna mtoto alivyoumizwa kwa kipigo, lakini majibu yanatoka mepesi kwamba mwanangu ana saratani ya damu, cha kushangaza alipolazwa hapana KCMC niliambiwa ana uvimbe ndani na inatakiwa nitoe fedha Sh375,000 kwa ajili ya upasuaji, ghafla nikaambiwa nimepeleka kwenye wodi ya wagonjwa wa saratani,"

"Kwa mtu mwenye akili timamu lazima aone kuna kitu kimefanyika ambacho si sawa, ila namwachia Mungu, kibaya zaidi mpaka hivi sasa sijaona msaada wowote kutoka kwa viongozi wa Serikali hata shuleni alikokuwa anasoma mwanangu," amesema.


Ilivyokuwa

Mama wa mtoto huyo amesema Februari 28, 2024  mwanaye huyo alirudi nyumbani akiwa hana furaha na mdogo wake Jonathan alimweleza mama yake kuwa kaka yake anavuja damu mdomoni.

Amesema alipomwangalia mwanaye alibaini ni kweli anavuja damu mdomoni na puani na alipomuuliza imekuwaje alimweleza amechapwa viboko na mmoja wa walimu hao kwa madai  ya kuchelewa kushika namba asubuhi.

"Ilikuwa siku ya Jumatano Februari 28, mtoto wangu alikuwa amerudi shuleni, kuna mahali nafanya kazi akirudi shule ananipitia, lakini siku hiyo  alirudi akiwa amedhoofika, kuna mdogo wake ambaye huwa wananipitia naye  hapa kazini,  akaniuliza mama mbona Jonathan anatoka damu mdomoni? nikamuuliza Jonathan umefanyaje? nikamwambia nenda kachukue maji asukutue mdomoni ili nione alipoumia, aliposukutua damu bado zikaendelea kutoka,"

Amesema hata jioni baada ya kumpa chakula, alimtaka kwenda kupumzika, lakini mdogo wake alimfuata na kumweza kuwa Jonathan anatoka damu puani, alipokwenda kumuangalia aliziona na alipomhoji alimwambia kuwa  anaumwa kichwam, hivyo alimpa dawa ya kupunguza maumivu, akalala.

Amesema ilipofika asubuhi alimuona damu zilikuwa zimejaa mdomoni na shuka alilokuwa amewatandikia lilikuwa limelowa damu, hivyo wakati anataka kumuaandaa ili ampeleke hospitali alibaini kuwa na majeraha mwilini.

"Wakati namvua nguo nimwogeshe nikaona mgongoni kuna alama ya fimbo,  umevimba na eneo la chini ya uti wa mgongo kuna uvimbe umevilia damu na ni kweusi,  pajani  nako kuna alama ya fimbo na kumevilia  damu, kwenye mguu nako kumevimba,"

"Nilimuuliza tena umefanyaje? Akaniambia mwalimu wa 'field' kamchapa, walichelewa shuleni, wenzake walijizuia fimbo kwa mabegi ya mgongoni, lakini yeye begi lake lilikuwa juu na alishindwa kujizuia, " amesema.

Alimweleza mama yake kuwa, wakati anaendelea kuchapwa mwalimu  alimchapa na akiwa na maumivu makali alimsukuma na kumpiga tena na fimbo upande wa ubavuni,"

“Keshokutwa  yake (macho mosi) nilienda shuleni na mtoto, nilipofika nilimkuta mwalimu mkuu msaidizi, wakati huo alikuwa darasani anafundisha akaniambia nisubirie, wakati huo nilimtafuta mwalimu wake wa darasa nikamweleza mwanangu ameshindwa kuja shuleni kwa sababu amepigwa hapa shuleni na hali yake sio nzuri,"

"Mwalimu mkuu aliporudi ofisini nikamwambia nataka nimwone mwalimu aliyemchapa mwanangu. Akaniuliza mtoto anamjua mwalimu aliyemtandika fimbo kwa jina, nikamwambia hapana ila akimuona kwa sura atamjua," amesema.

Amesema mwalimu msaidizi alitoa Sh20,000 na alimpeleka zahanati ambako alipewa dawa, lakini hali yake haikukwa nzuri na alipomrudisha aliambiwa ampeleke Hospitali ya St Joseph na siku chache baadaye akashauriwa ampeleke KCMC.

"KCMC walimpokea mtoto wakamwangilia wakanambia anahitaji upasuaji, kuna kitu kama damu imevimbia ndani na niliambiwa gharama yake ni Sh375,  yule mwalimu mkuu msaidizi akapigiwa simu akaambiwa mtoto anahitaji upasuaji, amesema.

Hata hivyo, amesema baadaye daktari aliyokuwa akimhudumia mtoto alimweleza mwanaye ana changamoto ya seli sahani, hivyo anatakiwa awekwe mrija tumboni kuna damu imevujia , lakini kabla hajawekwa akafariki dunia Machi 10, 2024.