Prime
AfCHPR yaipa miezi sita Tanzania kufuta viboko

Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu (AfCHPR), imetoa miezi sita kwa Tanzania kuondoa adhabu ya viboko kwa wanaotiwa hatiani kwa makosa mbalimbali kwa kuwa adhabu hiyo ni utesaji, udhalilishaji na unyama.
Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo katika kesi iliyokuwa imefunguliwa na Mtanzania, Yassin Rashid Maige aliyehukumiwa mwaka 2003 kutumikia kifungo cha miaka 30 na viboko 12 kwa wizi wa kutumia silaha mkoani Tabora.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imetupa maombi ya Maige kuachiwa huru kutokana na upungufu wa kisheria aliyoeleza katika shtaka hilo ikiwepo kukosa uwakilishi wa kisheria.
Mahakama hiyo imeitaka Serikali kumlipa fidia ya Sh300,000 Maige kutokana na kudhalilishwa na adhabu aliyopewa.
Wakisoma Hukumu hiyo Septemba 5 mwaka huu, Majaji wa Mahakama hiyo wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Dibo Sacko walipinga hoja za mawakili wa Serikali za kutaka shauri hilo kutokana na upungufu ya kisheria
Majaji wengine walishiriki katika Hukumu hiyo ni Ben Kioko, Rafaa Ben, Suzanne Mengine, Tulilane Chizumila, Chafika Bensaoula, Blaise Tchikaya, Stella Anukam, Dumisa Ntsebezana na Dennis Adjei.
Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud hakushiriki kusoma hukumu hiyo kwa kuwa Serikali ya Tanzania ndio ilikuwa inalalamikiwa ni ya Tanzania. wa mujibu wa Kanuni ya 9(2) ya Mahakama .
Mlalamikaji Yassin Rashid Maige hakuwa na mwakilishi Mahakamani hapo kwani bado anatumikia kifungo ambapo Serikali ilikuwa imewakilishwa na wanasheria wa Serikali, Dk Boniphace Luhende, Nkasori Sarakikya na Pauline Mdendemi.
Majaji hao wa AfCHPR wameiamuru Tanzania kufuta hukumu ya viboko na kufuata makubaliano ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu unaokataza hukumu za utesaji, ukatili, unyama na udhalilishaji.
Jopo la Majaji hao pia limeagiza Mamlaka kuwasilisha ripoti kuhusu utekelezaji wa amri hiyo kila baada ya miezi sita hadi pale Mahakama itakaporidhishwa na utekelezaji wake.
Katika kesi Maige, alidai Mahakama za ndani zilizoamua kesi yake zilikiuka haki zake chini ya Vifungu 2. 3, 5, na 7(1) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu .
Maige aliiomba Mahakama hiyo, irejeshe haki zake zilizopuuzwa, ifute makosa yote mawili kuhukumiwa kifungu Cha miaka30 na kuamuru aachiliwe kutoka gerezani.
Maige pia aliomba mahakama hiyo, kutoa amri nyingine yoyote ambayo inaweza kuwa sahihi na kuamuru serikali kumlipa fidia.
Mawakili wa Serikali walipinga mamlaka ya Mahakama hiyo ya AfCHPR kutoa msamaha wa kuachilia huru.
Hata hivyo, Majaji wa Mahakama hiyo walieza Mahakama hiyo ina mamlaka ya kutoa aina tofauti za fidia, ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kutoka gerezani, kama kuna ukiukaji unaodaiwa umefanyika.
Mahakama hiyo iliona Maige aendelee kutiwa hatiani na kutumikia kifungo kwani taratibu za Mahakama za ndani zilifuatwa.
Mahakama hiyo ilieleza madai ya ukiukaji wa haki zake inaweza kuzingatiwa.
Mahakama ilieleza kugundua kuwepo kwa sheria zinazoidhinisha adhabu ya viboko ni kinyume cha sheria Mikataba ya kimataifa.
Katika mazingira hayo, Mahakama ilisema adhabu ya Maige kuchapwa viboko 12 ilikiuka haki yake ya utu kama ilivyoelezwa chini ya Kifungu cha 5 cha Mkataba.
Mahakama hiyo pia ilieleza kugundua kuwa haki za Maige kukosa uwakilishi wa kisheria na haki yake ya heshima, vilikiukwa na iliamuru kulipwa kiasi cha Sh300,000.
Mahakama pia iliamuru Serikali ya Tanzania kuondoa adhabu ya viboko kutoka kwenye sheria zake na kanuni ya adhabu.