Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi wamsaka mwalimu anayedaiwa kumuua mwanafunzi

Muktasari:

  • Jeshi la polisi Kilimanjaro latumia mitandao ya kijamii kumsaka mwalimu anayedaiwa kumuua mwanafunzi.

Moshi. Zikiwa zimepita siku 16 tangu mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Samanga wilayani Rombo, Sixtus Kimario (7) afariki dunia kwa madai ya kuchapwa viboko na mwalimu na kumsababishia umauti, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limeamua kumsaka mwalimu huyo, James Urassa kwa kutumia mitandao ya kijamii baada ya kutorokea kusikojulikana.

Mwalimu huyo anatuhumiwa kumsababishia kifo mwanafunzi huyo, Julai 17, mwaka huu baada ya kumchapa viboko katika sehemu mbalimbali za mwili wake kwa madai ya kupiga kelele darasani ambapo mwalimu huyo baada ya kubaini mwanafunzi huyo amefariki dunia, alitoroka shuleni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Julai 17, mwaka huu ambapo alisema baada ya mwalimu huyo kutoa adhabu hiyo kwa mwanafunzi huyo, alitoroka kusikojulikana baada ya kubaini mwanafunzi huyo amefariki dunia.

Katika uchunguzi wa kitabibu ambao ulifanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC Julai 19, ndugu wa marehemu, Odilo Shayo amesema kuwa baada ya daktari kufanya uchunguzi wa kina ilibainika kuwa mwanafunzi huyo alifariki dunia baada ya kuumia sehemu ya ubongo wa nyuma ambao ulisababisha damu kuvujia kwenye ubongo.

Hata hivyo leo, Agosti 2, mwaka huu kulisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kutoka Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro ikieleza yeyote atakayemwona mwalimu huyo atoe taarifa polisi ili aweze kukamatwa.

"Mtajwa hapo juu anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kumuua mwanafunzi wa darasa la kwanza aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Samanga iliyopo wilayani Rombo Julai 17, 2023, popote pale atakapoonekana tafadhali toa taarifa ili aweze kukamatwa," amesema.