VIDEO: Aliyekuwa RC Simiyu kizimbani kwa tuhuma za ulawiti

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda (aliyevaa kofia) akiwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza leo Julai 9, 2024.
Muktasari:
- Upande wa mashtaka umesema uchunguzi wa kesi hiyo tayari umekamilika
Mwanza. Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza na kusomewa shtaka moja la kulawiti.
Dk Nawanda amepandishwa kizimbani leo Jumanne Julai 9, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Erick Marley na kusomewa shtaka hilo na waendesha mashtaka wa Serikali, Magreth Mwaseba na Martha Mtiti.
Kwa mujibu wa Mwaseba, mshtakiwa (Nawanda) alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.
"Mshtakiwa, Yahaya Nawanda, Mkazi wa Nyamata wilayani Bariadi mkoani Simiyu unashtakiwa kwa kosa la kumwingilia kinyume na maumbile 'kumlawiti' Tumsime Ngemela, kosa ulilolitenda Juni 2, 2024 eneo la maegesho ya magari, lililoko Rock City Mall wilayani Ilemela mkoani Mwanza," amesema Mwaseba.
Baada ya kumsomea shtaka hilo ambalo amelikana, Mwaseba ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.
Baada ya kukana shtaka, Dk Nawanda anayewakilishwa na Wakili, Constantine Mutalemwa ameomba dhamana kwa kuwa kosa hilo linadhaminika.
Baada ya kusikiliza ya pande zote, Hakimu Marley amesema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili, mmoja awe mtumishi wa umma na mwingine wa sekta binafsi na bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua Sh5 milioni.
"Dhamana itakoma endapo mshtakiwa atavunja sharti lolote ikiwemo kutofika mahakamani," amesema Hakimu Marley.
Mshtakiwa ametimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana na shauri hilo limeahirishwa hadi Julai 16, 2024, kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali na kesi kuanza kusikilizwa.