UVCCM wataka sheria kali kuwabana wabadhirifu

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere
Unguja. Wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ikionyesha madudu na ubadhirifu wa fedha katika miradi na taasisi za serikali, Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) imetaka wachukuliwe hatua wahusika huku zikitungwa sheria kali za kuwabana wabadhirifu hao.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 9, 2023 na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Kawaida wakati akizungumza na waandishi wa habari na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho makao makuu ya Jumuiya hiyo Gymkhana Zanzibar.
“Serikali irejeshe kanuni ya utumishi bungeni ili itungwe sheria kali zitakazowabana wabadhirifu wasio na nia njema ya Tanzania maana wanachofanya wanahujumu taifa na sisi hatupo tayari kuona hili linaendelea,” alisema Kawaida
Alisema jumuiya hiyo inawajibu wa kuwasemea vijana na kwamba katika ripoti hiyo ya CAG imeonyesha kutokurejeshwa Sh88.4 bilioni zilizotolewa mkopo kwenye vikundi vya vijana huku kukiwa na vikundi hewa vya vijana vilivyopewa Sh895.9 milioni.
Pia kuna mikopo inayodaiwa kwenye vikundi vilivyositisha shughuli za biashara Sh2.2 bilioni huku mamlaka za serikali za mtaa zikionyesha kutochangia Sh5 bilioni kwenye mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Sambamba na hilo, kwa mujibu wa Kawaida aliyedai kaisoma ripoti yote yenye kurasa zaidi ya 250, kuna mikopo ya Sh147.2 milioni imetolewa kwa watu wenye ajira rasmi.
Pia amesema kumebainika kasoro za kutoshirikishwa kwa wataalamu katika utoaji na urejeshaji wa mikopo “hivyo sisi jumuiya ya umoja wa vijana tunaunga mkono kwamba fedha za vijana zianze kutolewa katika mabenki kuepusha mianya hiyo ya upigaji.