Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utapeli wa ‘tuma kwenye namba hii’ unavyoshika kasi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yakiri ongezeko la asilimia 33. Majaribio yaongezeka kutoka 12,896 hadi 17,152. Mawakili wataja mwarobaini. Wananchi wataka kibano kampuni za simu.

Dar/Moshi. Nani wanasajili laini hizi kwa alama za vidole? ni swali ambalo Watanzania wengi wanajiuliza kufuatia kuongezeka kwa vitendo vya utapeli mitandaoni, huku meseji za ‘tuma kwenye namba hii,’ zikiongezeka kwa kasi.

Malalamiko ya wananchi wanaomiliki simu za kiganjani kupokea meseji za aina hiyo kila uchao yanasikika kutoka kusini hadi kaskazini mwa Tanzania na magharibi hadi mashariki, huku baadhi wakipokea meseji hadi nne kila wiki.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekiri kuwepo kwa ongezeko la asilimia 33 ya majaribio ya ulaghai wa utapeli kati ya Desemba 2024 na Machi 2025, huku mawakili na wanasheria wakidai uwepo wa ulegevu katika usajili wa laini.

Kwa mujibu wa TCRA, idadi ya laini za simu zinazotumika kwa mawasiliano hapa Tanzania imeongezeka kwa asilimia 4.1 kutoka laini milioni 86.8 Desemba 2024 hadi kufikia laini milioni 90.4 Machi 2025.

Kulingana na mamlaka hiyo yenye dhamana ya mawasiliano nchini, watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka kufikia milioni 66.5 Machi 2025 hapa Tanzania

Wananchi waliozungumza na Mwananchi wameitaka TCRA kuzibana kampuni za simu ambazo zitabainika laini zake kutumika kufanya utapeli na kutaka zipigwe faini ya hadi Sh100 milioni, wakisema hiyo itayaamsha yawe makini na usajili.

“Kwa sababu tunasajili laini kwa kutumia Nida (Kitambulisho cha Taifa) na alama za vidole, sasa hizo laini zinazotumika kwenye utapeli wamiliki wake si wanajulikana hadi picha zao? Kwanini tatizo linaendelea?” amehoji Mussa Yasin.

Yasin ambaye ni muuzaji wa vitabu mbalimbali katika Jiji la Arusha amehoji: “Halafu sawa tapeli amefanikiwa kutumiwa hela aliyolaghai, anaitoaje kwa wakala? Siamini kwa muda mfupi atatengeneza na kitambulisho kabisa. Haiwezekani.”

Usajili wa simu za mkononi unafanyika kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, ambapo awali lilifanyika kwa aina mbalimbali ya vitambulisho, lakini sasa ni kitambulisho cha Taifa.

Tangu mwaka 2018, usajili wa laini za simu Tanzania kwa njia ya kibiometria unatumia vifaa vya kielektroniki ambavyo vimeunganishwa kwenye mfumo wa vitambulisho vya Taifa unaoratibiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Jumbe fupi fupi kama “Nitumie kwenye namba hii jina litakuja (anataja), namba yangu usitume inadaiwa” na “Hongera umepokea zawadi  Sh7,000,000 kutoka Biko. Piga namba (anaitaja) upokee pesa yako,” zimeongezeka kwa kasi.

Mbali na jumbe hizo, lakini zipo jumbe za kiganga kama “Mganga wa Tiba amerudi kijijini anasaidia zindiko la biashara, cheo kazini, kurudisha mke au mume na kusafisha nyota bila kafara” na zile za “Freemason,” nazo zimeongezeka kwa kasi.

Jumbe nyingine ni “Mjukuu wangu utafutaji wako mgumu, pesa hazikai mkononi mpaka zinaisha, unasota sana, mpenzi hamuelewani. Je, utatunza siri nikusaidie pesa bila masharti magumu? Nipigie nikueleze,” zinatumwa kwa wingi.


Wananchi wapaza sauti

Mussa Yasin wa Jijini Arusha amesema matapeli hao ni wajanja na wanafahamu kila sekunde kuna miamala ya kifedha kwa simu inafanyika, hivyo wanatumia jumbe za “nitumie kwenye namba hii,” wakijua labda kwa watu 100 watampata mmoja.

“Unakuta umetoka kuongea na jamaa yako kama dakika moja au mbili tu na unahitaji kumtumia fedha. Dakika chache ukiwa na harakati unakutana na huo ujumbe, tena anakuambia ile laini inadaiwa. Usipokuwa makini unatuma,” amedai.

Yasin amedai jumbe za sasa zilizoongezewa maneno “usitume kwenye ile laini yangu inadaiwa, nitumie namba,” zimekuwa zikiwaliza wengi kutokana na watumiaji wengi wa simu kuchangamkia fursa za mikopo katika kampuni za simu.

“Wewe fuatilia, kati ya watumiaji 100, utakuta 10 hivi wana mikopo ya kifedha kwenye simu ambayo mingine inakatwa mara tu unapoweka fedha. Ndiyo maana siku hizi kabla hujamtumia pesa muulize ni laini ipi,” ameeleza Yasin.

Renalda Mbore, mkazi wa Jijini Dar es Salaam na Moshi amependekeza kampuni za simu ambazo laini zake zinasajiliwa kiholela na kuingia mikononi mwa matapeli zitozwe faini ya hadi Sh100 milioni kama njia ya kukomesha uhalifu huo.

“Kwa kuwa laini ni mali ya kampuni na sio mali binafsi ya mtu, kampuni zote za simu zinapaswa kudhibiti laini zote zinazosajiliwa kiholela mitaani. Hizi kampuni zinajua ni mfanyakazi wake yupi amesajili au wakala gani. Wawajibike,” amesema.

“Akikamatwa mtu mmoja anatumia laini iliyosajiliwa na Nida ya mtu mwingine na huyo mtu wala hajui kama kuna mtu anatumia usajili wake, basi mashtaka yake yawe chini ya kampuni husika ya simu. Tukifanya hivi hizi tabia zitakoma.”

“Binafsi nahisi kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu ambao si waaminifu. Haiwezekani pesa iingie kwenye simu au ufanye miamala mikubwa, na hapo hapo upigiwe simu ya mtu kukosea muamala,” amesema.

“Mwizi anapiga simu kampuni ya simu, anajitambulisha ndiye mmiliki na hadi namba ya siri, na kuiba. Mimi lilinitokea hilo Februari 13, 2025, niliibiwa simu na fedha zikatolewa, hawakunipa msaada wowote ule,” ameeleza Renalda.

Mjasiriamali anayejihusisha na uuzaji wa viatu na raba za mitumba mjini Moshi, Salome Salvatory, amehoji: “Hivi si tuliambiwa huu utaratibu wa kusajili kwa alama za vidole ndio unakwenda kukomesha huu utapeli? Mbona mambo ni yale yale?

“Kwa mwezi mie naweza kupokea meseji tatu hadi nne za ‘tuma kwenye namba hii,’ mara mimi mganga sijui wa kufanya nini. Yaani ni shida. Ukiwa ni mtu wa ushirikina unajikuta unajiingiza kichwa kichwa kwa hawa matapeli,” ameeleza Salome.


Walichokisema TCRA

Ripoti ya TCRA ya Desemba 2024 hadi Machi 2025 inaonyesha kumekuwa na ongezeko la matukio ya majaribio ya ulaghai kutoka 12,896 hadi kufikia 17,152 Machi mwaka huu.

Ongezeko hilo limeshuhudiwa kwa kila mtoa huduma wa mawasiliano ndani ya kipindi husika, huku TTCL ikiwa na ongezeko kuliko wengine kwa asilimia 64.

Mkoa wa Rukwa ndiyo unaoongoza kwa kuwa na matukio mengi nchini, uliorekodi matukio 7,385 ukifuatiwa na Morogoro 5,227.

Mikoa mingine iliyo katika tano bora ni Dar es Salaam (1,069), Mbeya (1,000) na Songwe (352).

Mikoa hiyo pekee inabeba asilimia 87.4 ya matukio yote ya majaribio ya ulaghai yaliyotokea katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Kwa upande wa matukio yaliyozuiliwa kimtandao, kampuni ya Airtel ilirekodi matukio 5,879, TTCL (3,925), Vodacom (3,143), Yas (Tigo zamani) (2,484), na Halotel (1,724).

Akizungumzia suala hili, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Bakari Jabir amesema ukuaji wa sekta ya mawasiliano umekuja na fursa mbalimbali na changamoto zake.

“Kampeni za ‘Ni rahisi na sitapeliki ni moja ya kampeni zinazowafanya watu wengi kuanza kuripoti matukio hayo na kurekodiwa kwa wingi,” amesema.


Mawakili waeleza kiini

Mawakili waliohojiwa kuhusu kwa nini makosa ya utapeli kupitia simu yanaongezeka licha ya sheria kali, walinyooshea kidole mamlaka zenye dhamana.

Wakili Peter Madeleka amesema: “Nadhani ongezeko la uhalifu kwa mitandao ya simu linasababishwa na mamlaka husika kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

“Pili, uhalifu unapiga hatua za kimaendeleo katika mbinu za ufanyikaji wake, wakati walinda sheria bado wana mbinu za kizamani za kukabiliana nao.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema tatizo kubwa ni ukosefu wa msingi wa uwajibikaji.

Amesema utekelezaji wa sheria umekuwa wa kusuasua, hasa kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika kwa haraka, isipokuwa pale wanapogusa viongozi wakubwa wa kisiasa.

Ameongeza kuwa baadhi ya watoa huduma huweka mbele maslahi ya kibiashara kuliko usalama wa watumiaji, huku akipendekeza kuwepo kwa mfumo wa kiotomatiki unaogundua namba za utapeli na kuzizuia mapema.

Pia amependekeza kuboreshwa kwa sheria na kanuni na kuweka mfumo rafiki wa kuziwajibisha kampuni za simu kisheria pale inapobainika hizo hazijachukua hatua stahiki pale laini zake ilizozitoa na kuzisajili ndizo zinatumika kwa utapeli.

Kwa upand wake, Wakili Jullius Semali amesema: “Polisi wangewezeshwa kimafunzo na kupatiwa vifaa vya kupeleleza kitaalamu zaidi na kwa haraka kuhusu makosa ya kimtandao.

Wakili David Shillatu amesema: “Sheria na kanuni zipo wazi, adhabu pia zipo wazi. Kinachopaswa kufanyika ni utekelezaji wa sheria hizo kwa ufanisi.”

“Alama za vidole ni za kipekee. Inakuwaje mtu anasajili laini kwa jina la mtu mwingine?” amehoji.