Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti: Dawa za Corticosteroids zinapunguza uwezekano watoto njiti kufariki

Mhitimu anayetarajiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (Cuhas) Dk Stanley Mwita akiwasilisha taarifa ya utafiti wake aliyoufanya kuhusu uwezekano wa dawa za Corticosteroids kwenye kupunguza uwezekano vifo vitokanavyo na tatizo la kupumua kwa shida kwa watoto njiti. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Utafiti wa matumizi ya dawa za Corticosteroids wakati wa ujauzito umeonyesha matumizi ya dawa hizo yanasaidia kunusuru maisha ya watoto njiti kwa kuwaongezea ufanisi wa kukabiliana na changamoto ya upumuaji wanapozaliwa.

Mwanza. Utafiti wa matumizi ya dawa za Corticosteroids wakati wa ujauzito umeonyesha matumizi ya dawa hizo yanasaidia kunusuru maisha ya watoto njiti kwa kuwaongezea ufanisi wa kukabiliana na changamoto ya upumuaji wanapozaliwa.

  

Utafiti huo umefanywa na Mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (Cuhas)Dk Stanley Mwita, anayetarajiwa kutunukiwa shahada hiyo katika mahafali ya chuo hicho yatakayofanyika Jumamosi Novemba 12, 2022.


Dk Stanley Mwita ni mmoja wa watakaotunukiwa PhD hiyo akiwa na mwenzake, Dk Karol Marwa ambaye amefanya utafiti wenye lengo la kutambua 'Athari za aina ya vinasaba vya Cytochrome P450, Protini za merozoiti na viwango vya dawa za mchanganyiko wa Artemisin Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.


Akizungumza leo Jumatatu Novemba 7, 2022, Dk Mwita amesema kupitia utafiti wake aliyoufanya kati ya Julai 2019 hadi Februari 2020 amebaini katika kipindi hicho wanawake 1,008 walijifungua watoto njiti 1,125 katika hospitali ya Bugando, Sekouture, Nyamagana na Sengerema mkoani Mwanza huku watoto 230 kati yao wakiwa mapacha.


"Dawa jamii ya Corticosteroids zinazopendekezwa na Shirika la Afya duniani, kupewa wanawake wanaotarajiwa kujifungua kabla ya wakati ndani ya siku saba ili kuwaepusha watoto wao dhidi ya hatari ya kupatwa tatizo la kupumua kwa shida ni sindano ya Dexamethasone au Betamethasone," amesema Dk Mwita


Dk Mwita amesema watoto njiti 259 waliozaliwa walikuwa na tatizo la kupumua kwa shida huku akiwataka wataalam kutoa dawa hizo kwa wajawazito walioko hatarini kujifungua watoto hao.


"Utafiti huu umebaini iwapo mjamzito akipewa dawa hizi kwa kipindi tajwa kuna uwezekano mkubwa wa kumfanya mtoto atakayezaliwa akiwa njiti aishi kwa sababu hatakumbana na ugonjwa wa kupumua kwa shida ambao umekuwa kisababishi kikuu cha watoto hawa kufariki," ameongeza


Amewashauri wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara nne kabla ya kujifungua ili kutambua iwapo wanauwezekano wa kujufungua mtoto njiti na kupatiwa dawa hizo zitakazoleta ufanisi wa kupambana tatizo la kupumua kwa shida kwa watoto wanaozaliwa na tatizo hilo.


Katika hatua nyingine, Kaimu Naibu Mkuu wa CUHAS (Taaluma, Utafiti na Ushauri), Profesa Peter Rambau amesema katika mahafali hayo ya 15 wahitimu 790 wanatarajiwa kutunukiwa vyeti kwenye kada mbalimbali za afya huku wawili kati yao wakitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD).


Profesa Rambau amesema wahitimu 32 watatunukiwa shahada ya Uzamili katika Utabibu, 394 watatunukiwa shahada ya kwanza katika uuguzi, maabara ya afya, ufamasia, udaktari, afya ya jamii, uuguzi wa watoto na 361 wakitunukiwa Stashahada katika kada ya mionzi, maabara na famasia.


"Mwaka huu zaidi ya asilimia 90 ya watu waliodahiliwa watahitimu hii inaonyesha ni kwa kiasi gani wanafunzi wamepikwa katika kada zote za afya. Lengo ni kuhakikisha tunazalisha watalaam watakaokuwa mwarobaini wa changamoto za kiafya zinazoikumba jamii," amesema Profesa Rambau


Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo cha Uuguzi Cuhas, Profesa Rose Laizer amesema chuo hicho kimewekeza nguvu kinaendelea kuandaa watalaam wake kwa vitendo ili kuwawezesha kufanya tafiti zitakazoleta utatuzi wa magonjwa na changamoto zinazoikumba jamii.