Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanane wapewa Sh1.048 bilioni kujenga vituo vya mafuta vijijini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafut, Dk James Mataragio akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikopo kwa wafanyabiashara nane kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini iliyoratibiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) chini ya  Benki ya Azania.

Muktasari:

  • Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga angalau asilimia 70 ya uwekezaji katika miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza nishati utoke sekta binafsi, hatua ambayo itaongeza kasi ya uwekezaji na upatikanaji wa huduma za nishati kwa wananchi.

Dar es Salaam. Wakati wafanyabiashara wanane wakipatiwa mkopo wenye jumla ya Sh1.048 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini, Serikali imetaka kuangaliwa uwezekano wa kuanzisha mpango kama huo kwa ajili ya vituo vya kujaza gesi vijijini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio leo Alhamisi Julai 23, 2026 wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo iliyoratibiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kwa ushirikiano na Benki ya Azania.

Dk Mataragio amesema mradi wa mikopo nafuu kwa ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini utarahisisha upatikanaji wa bidhaa za petroli, dizeli na mafuta ya taa katika maeneo ambayo kwa muda mrefu wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kuzifuata au kuzinunua kwa gharama kubwa.

Amesema hatua hiyo itapunguza gharama za usafiri na bei ya mafuta kwa wananchi wa vijijini, ambako mara nyingi bidhaa hizo huuzwa kwa bei kubwa zaidi kuliko mijini kutokana na gharama za usafirishaji.

Pia mradi huo pia utaongeza usalama kwa kuondoa utaratibu wa wananchi kuhifadhi mafuta kwenye nyumba na vyombo visivyo salama, hali ambayo imekuwa ikisababisha ajali za moto na kupoteza maisha.

“Ujenzi wa vituo vinavyokidhi viwango vya usalama utasaidia kulinda maisha na mali za wananchi huku ukiimarisha ubora wa huduma za mafuta vijijini,” amesema.

Amesema ni wakati sasa wa kupanua wigo wa uwezeshaji kwa sekta ya gesi katika magari ambayo imekuwa mbadala wenye gharama nafuu kwa watumiaji wengi wa usafiri.

Ametaka maeneo yenye miundombinu ya gesi kupewa kipaumbele ili kuwasaidia wawekezaji wadogo kuanzisha vituo vya kujaza CNG kupitia mikopo yenye masharti nafuu.

“Ili haya yote yafanikiwe nawaomba Benki ya Azania kuweka masharti rafiki zaidi na kuendelea kutoa elimu kwa waombaji ili kuvutia wawekezaji wengi na Ewura shirikianeni kwa karibu na wawekezaji hao kwa kuwapa elimu na mwongozo wa kutimiza viwango vya usalama na ubora,” amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia kufanikisha lengo la Serikali la kusogeza huduma za nishati karibu na wananchi na kuongeza uwekezaji katika maeneo ya vijijini.


Ili kuongeza wanufaika zaidi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Hassan Said amesema wakala huo unalenga kuwa na mikataba zaidi ya 200 ya ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mafuta kwa wananchi na kupunguza umbali na gharama wanazozikabili kufuata bidhaa hizo.

“Mikataba hii nane iliyosainiwa leo yenye thamani ya Sh1.048 bilioni ni mwanzo tu wa utekelezaji wa mpango hui, kiwango hiki bado hakijafikia hata asilimia 20 ya lengo la Rea la kuwezesha ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini,” amesema.

Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki ya kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa nishati kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) na maboresho ya mfumo wa kisheria na udhibiti.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga angalau asilimia 70 ya uwekezaji katika miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza nishati utoke sekta binafsi, hatua ambayo itaongeza kasi ya uwekezaji na upatikanaji wa huduma za nishati kwa wananchi,” amesema.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia na Teknolojia Mbadala kutoka Rea, Dk Advera Mwijage amesema ili mtu apate mkopo huo huangukiwa usalama wa eneo la mradi, umbali kutoka barabara kuu, umiliki halali wa ardhi kupitia hati ya kimila au hati ya serikali.

“Hili huenda sambamba na kuangalia vigezo vingine vya kiufundi vinavyohakikisha kituo kinaweza kujengwa na kuendeshwa kwa kuzingatia sheria na usalama wa watumiaji,” amesema.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania, Yahya Mbanka amesema benki hiyo itasimamia utekelezaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia weledi, uwazi na ufanisi kwa kushirikiana Rea.

Amesema Azania, iliyochaguliwa kupitia mchakato wa zabuni kuwa msimamizi wa kifedha wa mpango huo itahakikisha huduma zote za kifedha zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi zinapatikana na kusimamiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

“Pia tutatoa elimu ya fedha kwa wanufaika kabla ya kupokea mikopo wakati wa utekelezaji wa miradi na hata baada ya kuanza shughuli zao ili kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha na kuendesha biashara kwa ufanisi,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mikopo hiyo, Boaz Nyakeke amesema watatumia fedha hizo kama walivyoelekezwa ili lengo la mkopo huo lifanikiwe.

“Kupitua mradi huu utafanya sasa bei za mafuta kuuzwa kwa kufuata bei kikomo zilizowekwa na Mamlaka ya maji safi na majitaka (Ewura) hivyo kupunguza mzigo kwa wananchi,” amesema.