Ummy ataka ujenzi wa shule 225 ukamilike kwa miezi sita

Muktasari:
- Serikali imetoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri nchini Tanzania kuhakikisha ujenzi wa shule za sekondari 225 unakamilika ndani ya miezi sita tangu kupokea kwa fedha na mwongozo wa ujenzi wa shule hizo.
Dodoma. Serikali imetoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri nchini Tanzania kuhakikisha ujenzi wa shule za sekondari 225 unakamilika ndani ya miezi sita tangu kupokea kwa fedha na mwongozo wa ujenzi wa shule hizo.
Pia imeagiza ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Ujenzi huo unafanywa na Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia chini ya mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) unaogharamikiwa na Serikali kwa mkopo wa Benki ya Dunia (WB) wa takribani Sh1.1 trilioni.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 3,2021 katika taarifa yake iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha ofisi hiyo, Nteghenjwa Hosseah.
“Kazi za ujenzi zinatakiwa kuanza ndani ya wiki mbili baada ya kupokea fedha na muongozo wa ujenzi na kukamilika katika kipindi cha miezi sita kwa shule za sekondari za Kata na mwaka mmoja kwa shule za sekondari za mikoa,”amesema.
Ummy amewataka kuhakikisha maeneo yaliyoteuliwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo hayana migogoro ya umiliki wa ardhi na halmashauri zenye ufinyu wa maeneo ya ujenzi kutumia ramani za ujenzi wa ghorofa.
Hata hivyo, amesema halmashauri hizo zinatakiwa kuomba kibali cha kutumia kiasi kilichotengwa na mapato ya ndani kuweza kukamilisha ujenzi wa shule husika.
Maagizo mengine ni kuzingatia taratibu za usimamizi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii husika.
Ummy amesema ofisi yake imepeleka kiasi cha Sh100.58 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari mpya 214 ambazo zitajengwa kwenye kata za majimbo yote na Sh30 bilioni zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari mpya za wasichana kwenye Mikoa 10 (shule 1 kila mkoa) Tanzania Bara.
Mradi huu wa SEQUIP unatekelezwa kwenye eneo la Elimu ya Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2020/21 – 2024/25.
Amesema gharama ya ujenzi wa shule za sekondari za kata ni Sh600 milioni kwa kila shule na kiasi kilichopelekwa katika awamu ya kwanza ni Sh470 milioni.
Aidha, kwa upande wa gharama ya ujenzi wa shule za sekondari za wasichana za mikoa ni Sh4 bilioni ambapo Sh3 bilioni kimetolewa ikiwa ni malipo ya awamu ya kwanza ya ujenzi kwa kila shule.
Amesema shule za sekondari za kata zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wasiopungua 400 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne wakati shule za wasichana za mikoa zitachukua wanafunzi wasiopungua 1,000 kwa kila shule.