Umeme jua yarejesha matumaini kwa wanafunzi Kigoma

Mwakilishi wa Shirika la Chakula duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson(wa tatu kushoto), Balozi wa China nchini, Chen Mingjian (aliyevaa blauzi nyeupe) wakiwaongoza wenzao kukata utepe kuashria uzinduzi wa mradi wa umeme jua katika shule ya msingi Kigadye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma. Picha Happiness Tesha.
Muktasari:
Wanafunzi zaidi ya 800 wa Shule ya msingi Kigadye iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, walio katika mpango wa elimu kwa waliokosa (MEMKWA) wamepewa msaada wa umeme jua kuwawezesha kujisomea nyakati za usiku.
Kasulu. Wanafunzi zaidi ya 800 wa Shule ya msingi Kigadye iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, walio katika mpango wa elimu kwa waliokosa (MEMKWA) wamepewa msaada wa umeme jua kuwawezesha kujisomea nyakati za usiku.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo wa umeme jua uliofadhiliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na Serikali ya China, Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Amir Mohhammed amesema umeme huo siyo tu utawawezesha wanafunzi kujisomea usiku, bali pia utawaondolea adha ya kuchota maji kutoka nje ya eneo la shule kwa matumizi yao na kumwagilia bustani ya mbogamboga.
‘’Kwa kupata umeme huu wa uhakika sasa tutakuwa na uwezo wa kuvuta maji na kusukuma maji kutoka kwenye kisima kwenda kwenye matanki kwa matumizi ya jumuiya ya shule,’’ amesema Mwalimu Amir
Amesema shule hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukosa fursa hiyo kutokana hamasa kubwa ya jamii kupitia viongozi wa Serikali za Mitaa waliokuwa wanapita nyumba kwa nyumba kuhimiza wazazi wenye watoto waliokatisha masomo kuwarejesha shuleni.
Mwakilishi wa Shirika la WFP Tanzania, Sarah Gordon-Gibson amesema kupitia uwekezaji kwenye nishati endelevu, shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wengine tayari wamewesha zaidi ya watu 2000 kupata nishati ya kujisomea na kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii kupitia umeme jua.
“Kwa Kigoma, WFP tunasaidia shule 30 katika Wilaya ya Kasulu, Kibondo na Kigoma kubadilisha mifumo yake ya ufanyaji kazi ikiwemo kuwapa uhakika wa nishati ya umeme kupitia umeme jua,’’ amesema Gibson
Balozi wa China nchini, Chen Mingjian amesema mradi huo ni mfano ni moja ya mifano hai ya ushirikiano kati ya Serikali ya China na Tanzania katika juhudi za kuboresha huduma na maisha ya jamii.
Amesema kupitia mikakati hiyo, Serikali ya China imetenga dola za bilioni 4 za Kimarekani kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo teknolojia na uwekezaji kwenye nishati safi kufikia mwaka 20230 kulingana na malengo ya Umoja wa Mataifa.