Ulinzi waimarishwa huku kesi ya Lissu ikiendelea Mahakama Kuu

Dar es Salaam. Wakati kesi ya maombi ya mapitio iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ikiendelea katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salam, ulinzi katika eneo lote la mahakama umeimarishwa.
Kuanzia getini hadi ndani ya mahakama ulinzi umeimarishwa kwa kuwepo askari polisi waliovalia sare na wengine askari wasio na sare.

Baadhi ya maaskari wa jesh la polisi wakiwa nje ya mahakama kuu wakimarisha ulinzi katika kesi ya Lissu inayoendelea jijini Dar es Salaama leo.Picha na Sunday George
Unapoingia ndani ya viunga vya mahakama hiyo, lazima upite ujiandikishe katika daftari lililopo mapokezi na kisha unaonyesha kitambulisho na baada ya hapo unakaguliwa ndio unaruhusiwa kuingia Mahakama.
Japo utaratibu huo upo kila siku, lakini leo, unaongozwa na askari Polisi ambao hawajavaa sare za jeshi hilo, huku getini kukiwa na askari zaidi ya watatu nje na ndani ya geti waliovalia kofia ngumu wakiwa na silaha.
Ndani ya ukumbi wa mahakama namba mbili ambapo kesi hiyo inasikilizwa askari magereza zaidi ya nane waliovalia sare za jeshi pamoja na askari polisi wapo ndani ya ukumbi huo kuimarisha usalama.

Mbali na ulinzi kuimarishwa, wafuasi wa chama hicho, nao wamekaa kwa utulivu kwa kufuata utaratibu maalumu ambao wametakiwa kukaa katika mabechi yaliyopo ndani hapo na iwapo mtu atakosa sehemu ya kukaa anatakiwa kutoka nje ya ukumbi wa mahakama badala ya kusimama ndani ya ukumbi huo.
Lissu amewasilisha ombi mahakamani hapo akiomba Mahakama Kuu iitishe jalada la kesi ya kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi , Kisutu ili kujiridhisha na mwenendo wa kesi hiyo wa Juni 2, 2025.
Katika maombi hayo ambayo Serikali iliwasilisha Mahakama ya Kisutu walikuwa wanaiomba mahakama hiyo ikubali ombi la kuwalinda mashahidi katika kesi hiyo.
Serikali baada ya kuwasilisha ombi hilo, mahakama hiyo ilikubalina na maombi hayo.
Baada ya maombi hayo kukubaliwa, Lissu alikwenda mbele Mahakama Kuu, kuomba Mahakama hiyo iitishe jalada la kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu ili kujiridhisha na mwenendo wa kesi hiyo wa Juni 2, 2025.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu ambapo kwa sasa mawakili wa pande zote mbili wapo mahakama ya hapo wanaendelea kuchuana kuhusiana na maombi hayo ambapo Serikali imemuwekea pingamizi Lissu ikitaka maombi yake yasisikilizwe kwa hoja kwamba yanakiuka masharti ya kisheria na kwamba Mahakama hiyo haina amlaka ya kuyasikiliza kutoka na kasoro za kisheria.
Endelea kifuatilia mitandao ya kijamii