Ulikuwa uamuzi mgumu ujenzi daraja la Ubungo
Muktasari:
- Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji) ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesimulia namna uamuzi mgumu wa Rais wa Tanzania, John Magufuli yalivyokamilisha ujenzi wa daraja la juu la Ubungo ‘Kijazi Interchange’.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji) ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesimulia namna uamuzi mgumu wa Rais wa Tanzania, John Magufuli yalivyokamilisha ujenzi wa daraja la juu la Ubungo ‘Kijazi Interchange’.
Profesa Mkumbo ameyasema hayo leo Jumatano Februari 24, 2020 mbele ya Rais Magufuli aliyezindua daraja hilo katika ziara yake ya siku tatu jijini Dar es Salaam.
“Mradi huu unanigusa sana kwa sababu mwaka 2018 nikiwa Kahama saa 4 usiku nilipokea wito kwamba Rais Magufuli anatuita kesho yake Ikulu saa 4 asubuhi, nikiwa na wasaidizi wangu nilitafuta gari mpaka Mwanza asubuhi tulipanda ndege Mwanza mpaka jijini Dar es Salaam na saa 4 asubuhi tukawasili.”
“Ulituambia jambo moja tu kwamba naona nyie kubomoa jengo la wizara ya maji na jengo la Tanesco imewashinda sasa nimewaita kuwaambieni kwamba katika masaa sita yajayo, kama hamjabomoa basi nitakuja kubomoa kwa mikono yangu,” amesema Profesa Mkumbo ambaye wakati wa kuanza ujenzi wa daraja hilo alikuwa katibu mkuu Wizara ya Maji ambayo majengo yake yalikuwa jirani na lilipo daraja hilo.
Huku akizungumza kwa umakini Profesa Mkumbo amesema, “ nakumbuka tulikuwa na Mfugale (Patrick- mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania Tanroads). Tukaangaliana tukaondoka pale tukaitana pembeni tunaulizana tufanyeje? Mfugale akasema tukabomoe basi tukaitana na mzee Kamwelwe (Isack) siku mbili tukayabomoa.”
Profesa Mkumbo amesema Rais Magufuli alisema haiwezekani Serikali imechukua uamuzi mgumu kubomoa nyumba za wananchi halafu majengo ya Serikali hayabomolewi.
“Sifa yako kubwa mheshimiwa Rais ni kusimamia maamuzi yako na ndiyo maana leo tunaona majengo haya yamesimama,” amesema.