Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulega awakomalia makandarasi wanaochelewesha miradi ya ujenzi

Muktasari:

  • Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema Serikali haitaongeza hata siku moja kwa atakayeshindwa kukamilisha mradi wa ujenzi kwa sababu za uzembe.

Lindi. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amezidi kuwa mwiba kwa wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, akisema Serikali haitaongeza hata siku moja kwa atakayeshindwa kukamilisha mradi wa ujenzi kwa sababu za uzembe.

Ulega alitoa msimamo huo jana Mei 25 mkoani Lindi, akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa ukarabati wa miundombinu ya ujenzi katika mikoa ya kusini, baada ya mvua zilizonyesha mwaka huu kuharibu barabara na madaraja.

Kwa nyakati tofauti, Ulega amekuwa akitumia majukwaa mbalimbali kuwaonya wakandarasi, mathalan Mei 15 wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya ujenzi, aliwataka kutekeleza kazi zao kwa kuzingatia mikataba, masilahi ya wananchi na Taifa.

Siku iliyofuata yake (Mei 16), waziri huyo alitangaza mpango wa kuitisha uchunguzi dhidi ya mshauri elekezi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) awamu ya nne–Lot 4(1), unaohusisha kipande cha barabara cha Posta hadi Daraja la Kijazi, kufuatia ucheleweshaji wa utekelezaji na uchimbaji usio na mpangilio unaondelea katika maeneo mbalimbali.

Baada ya wiki moja, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ulitangaza kufanya mabadiliko ya baadhi ya watendaji wa BRT, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Ulega.

Jana katika ziara hiyo, Ulega aliwaambia wakandarasi hao, kuwa hivi sasa ni wakati mzuri wa kumaliza kazi zao kabla ya kuanza kwa mvua za vuli, akisema hatarajii kuona wananchi kuteseka kwa sababu ya uzembe wa waliopewa kazi za kujenga barabara na madaraja.

“Serikali imewaamini na kuwapa kazi ya ujenzi wa barabara na madaraja ya kudumu, hakikisheni mnakamilisha kwa ubora na wakati. Hatutakubali kuona wananchi wakiteseka kama ilivyotokea mwaka jana na mwaka huu,” alisisitiza Ulega.

Waziri huyo aliwataka makandarasi wanaojenga madaraja na barabara unganishi mkoani Lindi kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili ikamilike Septemba kabla ya kuanza kwa mvua za vuli.

Hivi sasa ujenzi unaoendelea katika barabara inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini baada ya athari za mvua za El Nino na kimbunga Hidaya, ambavyo vilisababisha kukatika kwa barabara za Marendego–Nangurukuru–Lindi–Mingoyo, Kiranjeranje–Namichiga, Tingi–Kipatimo, Nangurukuru–Liwale na Liwale–Nachingwea.

Ili kuhakikisha kazi ya ujenzi inakwenda kwa kasi, Ulega amewataka wakandarasi kuongeza idadi ya wafanyakazi na muda wa kufanya kazi bila kujali usiku na mchana, ili kazi iende kwa kasi na pia kusaidia vijana kupata riziki.

Waziri Ulega alikagua na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi wa madaraja ya Somanga Mtama (m60), Mikereng’ende (m40), Njega II Matandu (m60), Miguruwe (m39), Zinga (m 18).

Kuhusu barabara ya Nangurukuru–Liwale, Ulega alisema wizara kupitia (Tanroads) imetenga zaidi ya Sh9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa tuta la barabara hiyo yenye maeneo korofi ya Njinjo na Ngea na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Lindi, Emil Zengo, alisema ujenzi wa daraja la Somanga Mtama (m60) nguzo 41 zimekamilika kati ya 43 zinazotaakiwa kulibeba.

“Mradi umefika asilimia 42, ujenzi wa daraja la Kipwata (m40) una nguzo 34 na zote zimekamilika kujengwa na mradi umefikia asilimia 40.9,” alisema Zengo.