Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujumbe wa Pasaka KKKT wabeba mzito

Muktasari:

  • Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametuma salamu za Pasaka kwa mwaka 2022 zilizobeba ujumbe wa mambo makuu manane, yakiwamo mvutano na msuguano wa kisiasa kuhusu Katiba mpya, mivutano ndani ya kanisa hilo, vita ya Russia na Ukraine, kupanda bei kwa bidhaa na kutotabirika kwa mvua.

  

Moshi. Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametuma salamu za Pasaka kwa mwaka 2022 zilizobeba ujumbe wa mambo makuu manane, yakiwamo mvutano na msuguano wa kisiasa kuhusu Katiba mpya, mivutano ndani ya kanisa hilo, vita ya Russia na Ukraine, kupanda bei kwa bidhaa na kutotabirika kwa mvua.

Maaskofu wa makanisa mbalimbali nchini wamekuwa na utamaduni wa kutuma salamu za Pasaka kwa waumini wao kuashiria kufufuka kwa Yesu Kristo na kushinda kwake kifo.

Mambo mengine yaliyogusiwa kwenye salamu hizo ni umuhimu wa maridhiano ya Watanzania na athari za Uviko-19.

Kuhusu mchakato wa uandikaji wa Katiba uliokwama mwaka 2014 ukiwa katika hatua ya kupigiwa kura kwa Katiba inayopendekezwa, hivi sasa umeibua mjadala na mvutano, maaskofu wametaka kuwapo kwa maridhiano ya kulitekeleza jambo hilo katika njia itakayowafanya Watanzania waendelee kuwa wamoja

Mvutano uliopo nchini kwa sasa ni mchakato wa kuandika Katiba mpya uendelee au usubiri hadi mwaka 2025, misuguano na mivutano ndani ya KKKT na athari zitokanazo na ugonjwa wa Uviko-19.

Migogoro ndani ya KKKT

Kuhusu migogoro ndani ya Kanisa hilo, Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, Chediel Sendoro alisema ni ukweli mchungu migogoro inayoendelea katika maeneo tofauti inalitia doa kanisa.

“Ninajua hali hii inatuumiza wanakanisa wengi na tunatamani hali hii ifikie mwisho. Tumuombe Mungu sana atusaidie sisi sote ili tuweze kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro hii kwa kushika nafasi zetu, hasa kwa maombi.

“Maombi yatasaidia ili hatimaye tuweze kuuona mwisho wa hali hii ndani ya Kanisa. Tuliombee Kanisa la Mungu ili Yesu aliyefufuka na kututangulia kwenda Galilaya, atushindie katika hili pia na atutangulie katika kufikia utatuzi wa amani.

“Tunatamani kubaki kuwa chumvi ya ulimwengu na mfano mwema kwa ulimwengu wote,” alisema Askofu Sendoro, kauli ambayo haitofautiani na ya Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga.

Katika salamu zake za Pasaka, Askofu Munga aligusia suala la migogoro ndani ya kanisa hilo, akidokeza uwepo wa mivutano na misuguano ndani ya Kanisa hilo la KKKT, akisema hayo na mengine yanasababisha maisha kuonekana giza nene.

“Misuguano na mivutano iliyomo ndani ya Kanisa, mivutano na misuguano iliyopo kisiasa kama juu ya ama au la kuanzishwa mchakato wa kukamilisha Katiba mpya, Uviko-19 na vita ya Russia na Ukraine ni magumu, lakini yatapita,” alisema.

“Wakati tunapambana na janga la Uviko-19, ulimwengu umeingiliwa na vita vibaya vya Russia kuivamia Ukraine. Vita hivi vimekuwa na athari kubwa, ikiwamo vifo vya watu, uharibifu wa mali na makundi ya wakimbizi,” alisema.

“Pasaka ni kielelezo na mfano wa tumaini la kufikia maisha bora yenye furaha. Pasaka ni msingi wa tumaini la kufufuka kwetu,” alisema.

Katika siku za karibuni, waumini wa Kanisa hilo wameshuhudia kanisa likitikiswa na migogoro ya kiuongozi na mgogoro wa siku za karibuni kabisa ni wa Dayosisi ya Konde, ulioshuhudiwa Askofu wake, Dk Edward Mwaikali akiondolewa.
Hata hivyo, Askofu Mwaikali na baadhi ya maaskofu wa Dayosisi za Kanisa hilo wamepinga maamuzi ya kumuondoa Askofu Mwaikali, wakidai mkutano ulikuwa ni batili, wajumbe walipatikana kwa njia batili na Katiba ya Konde ilikiukwa.

Maridhiano na uhasama

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza alisema yanahitajika maridhiano katika ngazi tofauti, akisema dhuluma iliruhusiwa kuleta uhasama katika taifa na kutenganisha watu na taasisi mbalimbali.

“Uhasama umeota mizizi hata katika nyumba za ibada. Waliopakwa mafuta kupatanisha waliofarakana, hivi sasa wanakimbilia kupatanishwa mahakamani na kwa Kaisari. Nuru imezimika na chumvi imekosa ladha,” alisema Askofu Bagonza.

“Watumishi wa Mungu wanatumia njia za dunia kumaliza migogoro. Damu isiyo na hatia ifufue moyo wa kuachilia na kuleta maelewano tena. Tishio la vita ya tatu ya dunia haliwezi kuishinda damu ya Kristo mfalme wa amani,” alisisitiza.

Vita ya Russia na Ukraine

Askofu wa Dayosisi ya Mwanga ya kanisa hilo, Chediel Sendoro alitaja mambo matano, likiwamo janga la vita kati ya Russia na Ukraine, akisema vita hiyo ina athari kubwa katika ulimwengu mzima, hususan katika masuala ya uchumi.

“Athari hizi zimeshatufikia hata sisi hapa Tanzania, sote tunashuhudia kupanda kwa bei za mafuta ya petroli na dizeli, kunaathiri bei za vitu vingine vyote. Tunaishukuru Serikali inajitahidi kupunguza makali,” alisema.

“Tutambue kuwa janga hili linaweza kuwa nje ya uwezo wao. Badala ya kunyoosheana vidole pale mambo yanapokuwa magumu, tuzidi kuiombea Serikali yetu ili Mungu aipe hekima na maarifa ya kushughulikia jambo hili,” alisisitiza.

Walichosema kuhusu Uviko-19

Kuhusu Uviko-19, Askofu Sendoro alisema pamoja na kwamba jamii imerudi kwenye taratibu zetu za kawaida katika ibada na mambo mengine ya maisha ya kila siku, Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kwa ugonjwa huo.

“Ugonjwa wa Uviko-19 bado upo, tunaishi nao na unaua. Tusiupuuzie. Kwa wale ambao bado hawajapata chanjo, ninashauri waendelee kufuatilia utaratibu wa chanjo ili kujilinda na ugonjwa huu hatari,” alisisitiza askofu huyo.


Kuchelewa kwa mvua

Askofu Sendoro katika salamu zake za Pasaka, alisema hali ya hewa sio nzuri kwa kilimo kwa baadhi ya maeneo nchini, ikizingatiwa wakulima wanategemea zaidi mvua kutekeleza kilimo.

“Kwa ujumla hatujapata mvua za kutosha kuweza kukidhi mahitaji yetu ya kilimo. Lakini tunamshukuru Mungu kwa yote,” alisema.


Niwaombe Wakristo na wanajamii wote, tutunze vyakula tulivyonavyo ili kuweza kukidhi mahitaji yetu,” alisema.