Uhaba walimu watajwa chanzo kuporomoka ufaulu la saba

Muktasari:
Wakati ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kupata wastani wa daraja A hadi C ukishuka kwa miaka mitatu mfululizo, takwimu zinaonyesha ufaulu wa masomo matatu nao umeshuka kati ya mwaka 2021 na mwaka 2022.
Dar es Salaam. Wakati ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kupata wastani wa daraja A hadi C ukishuka kwa miaka mitatu mfululizo, takwimu zinaonyesha ufaulu wa masomo matatu nao umeshuka kati ya mwaka 2021 na mwaka 2022.
Wakati masomo hayo yakishuka katika ufaulu, somo la maarifa ya jamii na stadi za maisha ufaulu ulibakia kuwa katika kiwango kile kile ndani ya miaka hiyo huku uraia na maadili na Kiswahili wanafunzi wakifanya vizuri.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na Baraza la mitihani la Tanzania (Necta) kati ya mwaka 2020, 2021 na 2022, ufaulu ulishuka kutoka asilimia 82.68, asilimia 81.97 hadi asilimia 79.62 katika mtiririko wa awali.
Haya yanatokea wakati uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ukiendelea kuzorota na kufikia mwalimu mmoja kwa wanafunzi 65 kwa shule za umma mwaka 2022 ukilinganisha na wanafunzi 62 mwaka 2021, Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- Tamisemi).
Takwimu hizi zinabainisha kuwa shule 61 zina uwiano wa mwalimu mmoja akifundisha angalau wanafunzi 200 darasani. Shule 2,152 zikiwa na uwiano wa angalau wanafunzi 100 na zaidi ya nusu ya shule zote (Shule 11,282) zikiwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa angalau wanafunzi 50.
Taratibu zinataka mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wasiozidi 40.
Walimu watajwa
Hali hiyo inatajwa na wadau kuwa inatokana na kupungua kwa idadi ya walimu, kupungua ari ya walimu katika kujituma na kutokuwapo kwa umahiri kwa walimu.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi na Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi, Kiingereza ndiyo somo linaloongoza kwa kuporomoka katika ufaulu kutoka asilimia 48.02 pekee ya watahiniwa wote waliopata daraja A hadi C mwaka jana na kufikia asilimia 29.39 mwaka huu.
Sayansi na teknolojia ilifikia ufaulu wa asilimia 70.96 ya watahiniwa ambao walipata daraja A hadi C, ikiwa ni pungufu kutoka asilimia 83.23 iliyokuwapo mwaka 2021.
Somo la hisabati, asilimia 52.29 ya watahiniwa walipata daraja A hadi C mwaka 2022 ikiwa imeshuka kutoka asilimia 57.63 mwaka 2021.
Maarifa ya jamii na stadi za maisha, ufaulu wake ulibakia kuwa ule wa asilimia 71.2 katika miaka hiyo miwili.
Kiswahili, uraia na maadili ndiyo masomo ambayo wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri kwa miaka hii miwili ambapo ufaulu ulifikia asilimia 89.5 kutoka 88.5 mwaka 2021, huku uraia ukitoka asilimia 77.61 hadi asilimia 81.88.
“Ndiyo matokeo tunayostahili kuyapata,” alisema Jimson Sanga, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa
Alisema matokeo hayo yamepatikana huenda kutokana na kubadilishwa kwa mfumo wa uamuzi na usimamizi ambapo badala ya kuwatumia walimu wa shule ya msingi wenyewe, asilimia kubwa ya wasimamizi na wasahihishaji wa mitihani hiyo walikuwa wa sekondari.
“Hii inaweza kuwa sababu lakini ni lazima tuangalie namna ya kuongeza idadi ya walimu, ili kukidhi haja ya wanafunzi waliopo kwa kuweka uwiano sawa ili kuboresha ufundishaji,” alisema Sanga.
Aliongeza: “Tuendelee kuajiri, wapo wengi mtaani waliomaliza vyuo, hawana kazi, wangeajiriwa kulingana na matakwa ya wanafunzi bila kuzingatia kipaumbele cha masomo kwani masomo yote ni sawa.
Agosti mwaka huu, gazeti hili liliripoti kuwa zaidi ya walimu 63,221 wanahitajika katika shule za msingi nchini ili kuweka sawa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi uliowekwa na Serikali ikilinganishwa na wanafunzi zaidi ya 10.86 waliosajiliwa mwaka huu katika shule hizo.
Idadi hiyo ni baada ya kuajiriwa kwa walimu 5,000 wa shule hizo mapema mwaka huu kwani hadi Januari, kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za elimu msingi ( Best 2022), kulikuwa na walimu 173,270.
Mdau wa elimu, Catherine Sekwao alisema upungufu wa walimu si tatizo pekee bali umahiri ni sababu nyingine inayofanya ufaulu kushuka.
‘‘Pia hakuna usimamizi mzuri wa ufundishaji kwa walimu wa shule za umma kama ilivyo kwa shule binafsi , alisema.jambo ambalo linafanya arii ya kujali kazi kushuka kwa kiasi kikubwa.
“Unakuta mwalimu anakaa Gairo anakaa Mtumbatu anafika kazini saa ngapi, anakuwa amechoka anafundishaje.
Kuhusu kupungua kwa ufaulu katika somo la kiingereza alisema wakati mwingine msingi mbovu unatokana na walimu wa somo husika.
“Angalia kiingereza cha mwalimu, angalia kiingereza cha viongozi wetu, wakiongea hadi unasema nini hiki. Kama mwalimu hana msingi mzuri wa kiingereza unategemea afundishe nini.
Alisema ili kuondokana na hilo ni vyema kuwapo kwa walimu maalumu waliofundishwa lugha ya kiingereza kwa ajili ya kufundisha somo hilo kwa kile alichoeleza kuwa waliopo sasa hawajui lugha.
“Lakini pia kiingereza kiwe medium of instruction kuanzia darasa la tano, kufanya hivyo tutaongeza ari ya wanafunzi kujua lugha kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Endapo hayo hayatafanyika alisema mfumo wa elimu wa sasa utaendelea kutengeneza matabaka kwa kuandaa watawala na watawaliwa.
‘Hii ni kwa sababu wale waliosoma shule za kiingereza wataweza kuwa viongozi na kupata fursa za ajira katika mashirika ya kigeni tofauti na wale waliosoma katika shule za kawaida.
Kuhusu somo la hisabati na sayansi na teknolojia alisema kinachopaswa kufanyika ni kuongeza walimu wa kutosha.