Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhaba wa vyoo Stendi Kuu Mbeya abiria wajisaidia kwenye ndoo

Mwonekano wa vyoo vya Stendi Kuu Mbeya.

Muktasari:

  • Stendi Kuu jijini Mbeya huingiza na kutoa mabasi kati ya 41 hadi 50 kwa siku kwa safari zinazoingiza na kutoa abiria kwa siku, ukiachilia mbali uwapo wa daladala za ndani zinazokaribia 200.

Mbeya. Licha ya jitihada mbalimbali za Serikali kuhamasisha matumizi ya vyoo bora lakini maeneo yenye mikusanyiko ya watu, hali imekuwa siyo shwari kwa Stendi Kuu jijini Mbeya.

Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na  stendi za mabasi na sehemu za biashara za vileo hali inayowalazimu kuwa na ndoo maalumu iliyotiwa maji na sabuni ya unga kwa ajili ya  kujisaidia wateja hususan wa kike.

Matumizi ya ndoo zenye sabuni inaondoa harufu mbaya pale wateja wanapotumia vifaa hivyo mbadala kufuatia kukwepa foleni kwenye choo.

Kutokana na kadhia hiyo Mwananchi ilifanya uchunguzi na kubaini kwenye kituo cha kikuu cha mabasi ya mikoani cha jijini Mbeya na kushuhudia abiria wakiwa kwenye foleni ya kujisaidia.

Stendi hiyo huingiza na kutoa mabasi kati ya 41 hadi 50 kwa siku kwa safari zinazoingiza na kutoa abiria kwa siku, ukiachilia mbali uwapo wa daladala za ndani zinazokaribia 200.

Hata hivyo, pamoja na ukubwa wa magari na abiria lakini changamoto imekuwa kubwa ya ukosefu wa vyoo vya kutosha lakini hata vilivyopo matundu saba ni vya kulipia hali inayosababisha kero hiyo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara wamebuni njia maalumu ya kutenga ndoo zenye sabuni za unga ambazo huwawezesha wateja wao kujisaidia na kumaliza haja zao.

Idadi hiyo bado haikidhi mahitaji kulingana na mwingiliano mkubwa wa watu hali ambayo imesababisha viongozi wa kituo hicho cha mabasi na abiria kupaza sauti.

Mwonekano wa vyoo vya Stendi Kuu Mbeya kwa upande wa wanawake.

Uongozi wa stendi wakiri tatizo

Akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya viongozi, John Simbeye amekiri kuwepo kwa kadhia hiyo na kwamba kimsingi hali siyo nzuri ya miundombinu ya vyoo sio rafiki licha ya kutoa taarifa kwa Jiji.

"Umeona kwa nje ndani vyoo hali ni mbaya abiria na wahudumu wanapata changamoto kubwa hali ambayo uwalazimu kujisaidia sehemu yoyote," amesema.

Amesema eneo la kituo cha mabasi ya mikoani ni kubwa kuna biashara za tofauti na kusababisha muingiliano mkubwa baada na kabla ya kufika mabasi huku kuna choo kimoja chenye matundu saba ambayo ni machache na isitoshe vimejengwa miaka mingi havina bora.

Amesema kumekuwepo na changamoto ya uchafuzi wa mazingira kwa watu kujisaidia nje ya miundombinu ya vyoo hali ambayo ina hatarisha kuhatarisha kuwepo magonjwa wa milipuko.

"Tunaomba Jiji wakae wafanye tathmini sehemu gani wajenge miundombinu rafiki ya vyoo kwani mahitaji ni makubwa lakini wanategemea choo kimoja chenye matundu saba ambayo yanatumiwa na jinsia zote," amesema.

Amesema suala hilo la changamoto hiyo waliwasilisha kwa uongozi wa Jiji na hata Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson tulifikisha kilio chetu lakini hali bado mbaya watu wazima tunapanga foleni kujisaidia," amesema.


Abiria wapaza sauti

Peter David aliyekuwa akisafiri kutoka Mbeya kwenda Iringa amesema mazingira yalivyo ni vyema Serikali kuchukua hatua kabla ya athari kubwa kujitokeza.

"Kituo cha mabasi Mbeya ni kikubwa, ni aibu hali ya vyoo kuwa mbaya huku wananchi wakilipia Sh200 kupata huduma vyoo ni vichafu ambavyo kwa wanawake ni hatari," amesema.

Kwa upande wake Hamisa Mbando amesema kuwapo kwa gharama za huduma ya choo huenda ndio inasababisha changamoto ya kukithiri kwa vinyesi katika stendi hiyo.

"Unakuta abiria amesafiri kutoka Mwanza kuja Mbeya hana pesa ya kula, kunywa wala kulala, atapataje ya kulipia choo hapo lazima ajisaidie pembeni mwa stendi na kadhia wanapata wanahudumu hapa," amesema Hamisa.

Mwonekano wa vyoo vya Stendi Kuu Mbeya kwa upande wa wanaume.

Wafanyabiashara nao

Mfanyabiashara wa vitafunwa, Rehema Nuhu, amesema serikali inapata fedha nyingi za mapato kutokana huduma zinazotolewa ufike wakati kuona na kutatua changamoto hiyo.

"Ikumbukwe Serikali hiyohiyo inafanya kampeni za ujenzi wa vyoo bora lakini kwenye maeneo ya uwekezaji wa vitega uchumi ni hatari hata ukimtaka kiongozi aingie kujisaidia hawezi," amesema.

Naye mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema wameamua kutumia mbinu maalumu ya kutenga ndoo ili kuwasaidia wateja wao.

"Tunahudumia watu wengi sasa unajiuliza inakuaje mtu mzima apange foleni chooni, unaamua umuandalie njia maalumu kumaliza haja zake, wakiongeza vyoo itasaidia," amesema.


Kauli ya Jiji

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema: “Hiyo stendi ni ya zamani tangu wakati wa uhuru, ndiyo maana imechakaa. Lakini tuna mpango wa ujenzi wa stendi nyingine ya kisasa. Hata hivyo bado tunaendelea na ukarabati wa vyoo hivyo, kila bajeti inapopatikana.”

Naye, Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema hajapokea malalamiko kuhusiana na changamoto ya vyoo bali anachofahamu ni uhamisho wa kituo hicho cha mabasi kwenda uwanja wa ndege wa zamani.

"Suala la vyoo vipo viwili vya kulipia na kawaida kwa hilo unalohoji nitafuatilia kujua uhalisia na kuchukua hatua," amesema.

Issa ambaye ni Diwani wa Isanga, amesema kwenye kituo hicho cha mabasi ya mikoani kuna mwekezaji anayesimamia, hivyo watafuatilia tukikuta hali mbaya tutachukua hatua.

Issa amesisitiza na kuonya wananchi wanaokiuka sheria kwa kujisaidia nje ya miundombinu ya vyoo watatozwa faini, huku akisisitiza wananchi wawe wavumilivu kwa sasa serikali imewekeza nguvu ujenzi wa madarasa.


Athari kiafya

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Yesaya Mwasubiri ametahadharisha jamii wanaotumia vyoo vya jumuiya kutumia maji tililika na sabuni kwa usalama na kujikinga na magonjwa ya milipuko.

"Asilimia kubwa usalama wa maji katika maeneo hayo ni mdogo kuna watu pasipo mashaka wamekuwa wakijisaidia haja ndogo ndani ya majaba wanayo hifadhia," amesema.

Dk Mwasubila ameitaka jamii kubadilika ili kuepuka magonjwa yanayoepukika hususan wanawake kuacha kutumia ndoo au makopo kujisaidia haja ndogo kwa kile alichodai kuwa kwenye hatari ya kuugua homa ya matumbo, kuhara na magonjwa ya kuambukizwa.