Wajisaidia vichochoroni stendi ya Siha ikikosa vyoo

Choo cha stendi Sanya juu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro
Muktasari:
Madereva wanaotumia stendi ya Wilaya ya Siha wamesema wananalazimika kujisaidia pembezoni mwa magari, ukuta wa vibanda vya stendi, huku wakiitaka Halmashari ya Wilaya hiyo kupitia Idara ya Mazingira wafuatilie hili kabla ya magonjwa hayajatokea.
Siha. Madereva wa magari ya abiria na mamalishe stendi ya mabasi Sanya Juu Wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro wamelazimika kujisaidia haja ndogo hovyo kutokana na choo cha stendi hiyo kujaa uchafu hali inayowaweka hatarini kupata magonjwa.
Maeneo ambayo yamekuwa yakitumiwa vibaya ni pamoja na pembezoni mwa magari ya abiria na kwenye ukuta wa majengo yaliyopo stend hapo.
Wakizungumza na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti wamesema zaidi ya miezi sita wanajisaidia sehemu hizo baada ya mhudumu kuacha kazi kutokana na kutokulipwa mshahara hivyo kuomba Halmashari kukifanyia usafi choo hicho kabla magonjwa ya mlipuko hayajatokea.
Madereva hao wamesema wananalazimika kujisaidia pembezoni mwa magari, ukuta wa vibanda vya stendi, huku wakiitaka Halmashari ya Wilaya hiyo kupitia Idara ya Mazingira wafuatilie hili kabla ya magonjwa hayajatokea.
John Kileo mmoja wa madereva hao amesema wanalipa ushuru kwenye kituo hicho cha mabasi lakini zaidi ya miezi sita wanajisaidia sehemu zisizo sahihi ikiwamo kwenye ukuta pembezoni mwa magari, kutokana na choo kujaa kinyesi na kutokuwa na mhudumu wa kukifanyia usafi.
"Mhudumu alikuwepo lakini aliacha kazi kutokana na kutolipwa mshahara wake kwa kukihudumia choo hicho hivyo kuamua kuacha kazi, tuna omba idara ya mazingira kufanya usafi ili wananchi wafanye shughuli zao kwa uhakika," amesema.
Kileo ametolea mfano dereva mwenzake aligongwa na pikipiki akitokea kujisaidia na kuvunjika mguu huku akisisitiza kama choo kingekuwepo asingekwenda kujisaidia eneo jingine na kupata tatizo hilo.
Mama lishe wa eneo hilo Anna Rubeni amesema toka choo kujaa wateja wamekuwa wakiwasumbua mara baada ya kupata huduma ya chakula huku wenye haja ndogo wakijisaidia kwenye ukuta na haja kubwa inabidi kuwaonyesha choo cha Kituo cha Polisi Sanya juu hivyo kuomba Halmashari warekebishe tatizo hilo.
"Wakati mwingine tunawaagizia watu waende choo kilichopo kituo cha Polisi Sanya, Wengine wanaogopa kwa hiyo hali sio nzuri," amesema Anna.
Mwenyekiti wa Halmashari hiyo Dancan Urasa, alipoulizwa suala hilo amesema atafika katika eneo husika na pia kumpa taarifa Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashari hiyo Upendo Mangali ili kulifanyia kazi jambo hilo.