Ugonjwa usiojulikana waibuka Lindi

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Maaskofu kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika na baadhi ya viongozi katika mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) unaofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuna ugonjwa mpya umeingia katika mikoa ya Kusini ambapo baadhi ya watu wanatokwa damu puani na kuanguka.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuna ugonjwa mpya umeingia katika mikoa ya Kusini ambapo baadhi ya watu wanatokwa damu puani na kuanguka.
Rais Samia ameyasema hauo leo Jumanne Julai 12, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akihutubia Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (Amecea) unaofanyika nchini kwa siku tatu.
Amesema kuwa bado ugonjwa huo haijajulikana unasababishwa na nini lakini wataalamu wa afya wanaendelea kufanya uchunguzi.
“Kuna kila aina ya maradhi mapya yanazuka ambayo hatuyajui nilikuwa nazungumza na Waziri Mkuu, juzi ametoka ziara kule mikoa ya kusini, Lindi ameniambia ameona kuna maradhi mapya yameingia
Wanadamu wanatokwa tu damu puani na wanadondoka, hatujui ni kitu gani, wataalamu wa afya wamehamia huko wanaangalia ni kitu gani” amesema
Bila kutaja idadi ya waliogundulika kuugua ugonjwa huo, Mkuu huyo wa nchi amesema ni wengi na wanaugua mfululizo.
“Angekuwa mmoja au wawili tungesema ni presha laikini watu hao ni wengi kwa mfululizo, ni maradhi ambayo hatujawahi kuyaona” amesema
Rais Samia aliwataka viongozi wa dini kutumia nyumba zao za ibada kuhamasisha waumini umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
“Nimefurahi kuona viongozi wa dini wanaona umuhimu wa mazingira kiasi cha kukusanyika kujadili ni namna gani tunaweza kuifanya dunia yetu kuwa salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Endapo tutashirikiana kwa pamoja katika kusinamia na utunzani wa mazingira tutafanikiwa, tunaomba mawazo yenu ili tuone namna tunaweza kuyaingiza kwenye sera zetu,”. amesema Rais Samia.