Uchimbaji mchanga wahatarisha mazingira Kisiwa cha Uzi

Muktasari:
- Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed amesema wamejipanga kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Kisiwa cha Uzi kilichopo mkoani Kusini Unguja kimeathiriwa na uchimbaji mchanga holela kwa ajili ya biashara ya matofali.
Kiongozi wa kamati ya kupambana na uharibifu wa mazingira katika eneo hilo, Ali Rashid Ali amesema utafiti walioufanya umebaini nusu ya kisiwa hicho tayari imeathiriwa na uchimbwaji mchanga holela.
Amesema hali hiyo imesababisha nguvu ya maji ya bahari kuingia katika baadhi ya maeneo ya kisiwa hicho na kuleta athari katika kilimo na makazi ya wananchi.
“Zaidi ya mashimo 47 yenye upana wa futi 20 na kuendelea yanayotokana na uchimbaji mchanga yamo katika kisiwa chetu hali inayoweza kuleta madhara kwa jamii,” amesema.
Ali amesema katika utafiti wao wamebaini wachimbaji wa mchanga wamekuwa wakiusafirisha nje ya kisiwa hicho na wengine wakianzisha biashara ya matofali.
Mlinzi katika eneo hilo, Ali Abdalla amesema jitihada za kudhibiti uchimbaji mchanga hukwama kutokana na kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Serikali.
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed amesema wamejipanga kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira.
Amesema kikosi cha utafiti kutoka wizarani kimeandaliwa kwa lengo la kuangalia uharibifu wa mazingira na kutoa miongozo ya kukinusuru kisiwa hicho.
Waziri Hamad amesema hali ilivyo haiwezi kufumbiwa macho kwa kuwa Serikali imeshatenga maeneo maalumu ya kuchimbwa mchanga.
Amesema wanashirikiana na vikosi vya askari wa Serikali kufanya doria ili kuhakikisha uharibifu wa mazingira hauendelei.
Kisiwa cha Uzi kina njia maalumu ya kuingilia kwa watembea kwa miguu na magari wakati maji yanapokupwa na yanapojaa haitumiki.