Uchimbaji mchanga holela waathiri makazi

Muktasari:
- Baada ya nyumba kubomoka, wananchi wa Mtaa wa Magomeni Kagera wameiomba Serikali kuwasaidia kunusuru makazi yao kutokana na mmomonyoko wa ardhi unaosababishwa na uchimbaji holela wa mchanga.
Mtwara. Wananchi wa Mtaa wa Magomeni Kagera katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, wameiomba Serikali kuwanusuru na mmomonyoko wa ardhi unaotokana uchimbaji holela wa mchanga.
Akizungumza na Mwananchi jana Desemba 27, 2023, Editha Petro, mkazi wa Mtaa wa Kagera B, Manispaa ya Mtwara Mikindani amesema eneo hilo kuna mtaro mdogo ambao umekuwa ukichimbwa usiku, hivyo kupanuka na kusababisha mmonyoko wa ardhi.
Amesema ameishi eneo hilo takribani miaka 20 na mtaro huo ulikuwa mdogo, lakini uchimbaji mchanga umeathiri eneo hilo.
“Wachimbaji wengi wa mchanga wamekuwa wakija kuchimba muda wa usiku kwa kuwa hatuwaoni, ndio maana tunashindwa kuwabaini. Pia tunashindwa kuwapa elimu kuhusu madhara ya uchimbaji na athari zake,” amesema.
Kwa upande wake, Majid Chikumba, mkazi wa mtaa wa Magombeni Kagera, amesema wachimbaji mchanga wamekuwa wakiwapa wakati mgumu kwa kuwa athari zimekuwa kubwa, huku mto ukiendelea kutanuka na kuwa mkubwa zaidi.
Naye Zainabu Mfaume, mkazi wa mtaa huo amesema mvua zikinyesha hali inakuwa mbaya na kusababisha wanafunzi kushindwa kwenda shuleni.
Maelezo hayo yameungwa mkono na Nicolaus Magalila, mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kagera B akisema licha ya elimu inayotolewa, kumekuwa na changamoto kwa kuwa wanaopewa elimu si wanaofanya uharibifu huo.
“Wengi wao tunawaelemisha hata tukifanya doria tunashindwa kwa kuwa wanatembea usiku, ndio maana mfereji umetanuka sana na kuleta madhara kwa wananchi pamoja na nyumba zao kuathirika,” amesema.
Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Nyange amesema baada ya kupata taarifa walikwenda eneo la tukio na kubaini uwepo wa madhara makubwa ya uharibifu wa maziringira.
“Tulitembelea eneo hilo tukiwa na wataalamu kuona namna gani tunaweza kuwasaidia wananchi hao, lakini cha kusikitisha tulipofika tuliwakuta wakiwa na michanga majumbani ambao wamechimba neo hilo. Tumewalipisha faini kwa kuchimba mchanga bila kibali,” amesema Nyange.