TMA yatahadharisha mvua kubwa siku mbili Dar

Muktasari:
- Wakati vipindi vya mvua vikiendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri kunyesha kwa mvua kubwa katika mikoa mitatu nchini.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewaonya wakazi wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari kwani kutashuhudiwa vipindi vikubwa vya mvua.
Kulingana na taarifa iliyololewa leo Aprili 21, 2023 TMA mikoa hiyo mitatu ni Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar.
TMA imefafanua kuwa vipindi hivyo vya mvua vitashuhudiwa kwa siku mbili mfufulizo katika Jiji la Da es Salaam, mikoa ya pembezoni na mkoani Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladislaus Chang'a amesema wanaoishi mabondeni wanapaswa kuchukua tahadhari
Amesema mvua zinazoendelea sasa ni utabiri uliofanyika Februari 22, mwaka huu ambapo TMA ilitabiri Dar es Salaam, Pwani, Zanzibar na Mororgoro zingepata mvua za juu kuliko kawaida.
"Wakazi wanapaswa kujitayarisha kwa baadhi ya siku za mvua za juu ya kawaida, ambazo zinaweza kuwa na athari kwa usafiri na maji pia kuna uwezekano wa kutokea kwa hali mbaya ya hali ya hewa ambayo inatarajiwa kuathiri usafiri na miundombinu," amesema.
Kulingana kiongozi huyo, baadhi ya maeneo yatatarajiwa kuzungukwa na maji, uharibifu wa miundombinu ambayo inaweza kuathiri shughuli za kiuchumi.
Dk Chan’ga amesema wataendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa kwa wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari.