Tisa wafariki dunia, 23 wakijeruhiwa ajalini Mbeya

Wananchi wakishuhudia gari aina ya Coaster iliyopata ajali katika maeneo ya Iwambi jijini Mbeya.
Muktasari:
- Ajali hiyo ilitokea jana katika mlima wa Iwambi, ambapo gari aina ya Howo Kampuni ya Afric Motors Ltd ya Zambia liliigonga gari aina ya Mitsubishi likitokea Mbeya Mjini kwenda Mbalizi.
Mbeya. Watu tisa wamefariki dunia huku 23 wakijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea jana Septemba 22, 2023 katika mteremko wa Iwambi, Wilaya ya Mbeya vijijini mkoani Mbeya ikihusisha magari mawili.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamini Kuzaga imeeleza kuwa katika ajali hiyo watu tisa walipoteza maisha na kati ya hao, wanaume ni watano na wanawake wanne.
Amesema watu 23 walijeruhiwa, ambapo wanaume ni 13 huku wanawake wakiwa 10, majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali teule ya Ifisi iliyopo mji mdogo wa Mbalizi.
“Miili ya marehemu pia imehifadhiwa kwenye hospitali hiyo na marehemu saba tayari wametambuliwa, huku miili miwili bado haijatambuliwa,” amesema.
“Chanzo cha ajali ni dereva wa lori Mohamed Abilah (47) raia wa Zambia kushindwa kulimudu gari lake kwenye mteremko mkali na kwenda kuligonga kwa nyuma gari ya abilia. Dereva huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika,” amesema Kuzaga.
Kamanda huyo ametoa wito kwa madereva wanaotumia barabara hiyo kuhakikisha wanakagua magari yao kabla ya safari huku wamiliki wakitakiwa kutowapa madereva wasiozingatia sheria ili kuepusha ajali.