Watu kadhaa wahofiwa kufariki ajalini Mbeya

Wananchi wakishuhudia gari aina ya Coaster iliyopata ajali katika maeneo ya Iwambi jijini Mbeya.
Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea leo Septemba 22 majira ya saa 12 jioni katika maeneo ya Iwambi jijini Mbeya likihusisha gari aina ya Coaster inayofanya kazi zake Nsalaga na Mbalizi.
Mbeya. Watu ambao idadi yao haijajulikana wanadaiwa kufariki dunia baada ya gari walilokuwa wamepanda kutoka Mbeya mjini kwenda mji mdogo wa Mbalizi kuacha njia na kutumbukia shimoni kwenye mteremko uliopo Iwambi mkoani Mbeya.
Mwananchi Digital imefika eneo la tukio na kushuhuhudia wananchi wakiendelea kutoa msaada wa kuondoa miili na kunyanyua gari hilo aina ya Coaster linalofanya safari zake kutoka Nsalaga kwenda Mbalizi jijini humo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha tukio hilo akisema bado hajapata undani wake kutokana na kutokuwa karibu na eneo la tukio.
"Ni kweli nimepata taarifa za ajali hiyo ila sijajua kwa undani kwa sababu muda huu natoka kwenye kikao hapa maeneo ya Nanenane, hivyo nasubiri taatifa zaidi," amesema Kuzaga.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Isack Msepa amesema gali hilo likiwa katika mteremko huo, lilisukumwa na lori ambalo lilifeli breki na kudondoka shimoni.
"Tulifika mapema na wapo ambao walipona kama watatu hivi, akiwamo mzee, mama na mtoto ila wengine tuwaombee, tumesomba miili ya kutosha," amesema Msepa.
Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yake kwa habari zaidi.