Raia wa kigeni wafariki dunia ajalini Njombe

Lori lililokuwa limewabeba raia wa kigeni katika eneo la ajali
Njombe. Watu sita raia wa kigeni ambao walikuwa wanasafiri bila vibali wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wamepanda kupinduka katika Kijiji cha Iyai, Kata ya Luduga Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, John Imori wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema ajali hiyo imetokea barabara ya Makambako kuelekea Mbeya ambapo raia hao wa kigeni walikuwa wakisafirishwa kwenda nchi jirani.
Amesema ajali hiyo imetokea leo ambapo watu wengine wanane wamejeruhiwa na mpaka sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Wanging'ombe.
Amesema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu ya gari hilo kupinduka na kusababisha ajali iliyosabisha vifo vya watu hao.
"Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka dereva na utingo wa Scania ambao wamesababisha ajali hiyo iliyokuwa na raia wa kigeni ambao wanasadikika kuwa ni kutoka Ethiopia," amesema Imori.
Amesema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Scania lenye tela lililokuwa linatoka Makambako mkoani Njombe na kuelekea Zambia.
Amesema jeshi hilo baada ya kufika eneo la tukio walikuta ndani ya gari kuna mizigo mingi ambayo ni vifaa vya ujenzi pamoja na watu ambao ni raia wa kigeni ambao hawakuwa na hati zozote za kuwatambulisha.