Kamera za barabarani kumaliza ajali nchini

Dar es Salaam. Kutokana na kuwepo kwa vitendo vya madereva kukimbizana wakati wa safari, Serikali iko katika mchakato wa kutafuta wakala wa kuleta kamera zitakazofungwa barabarani ili kufuatilia na kubaini mwenendo mzima wa uendeshaji nchini.
Wakati Serikali ikiwa kwenye mchakato huo, wadau wamepongeza hatua hiyo na kusema itasaidia kupunguza au kutibu tatizo kwa kiwango kwa fulani japo halitakuwa suluhisho.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, Ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha ajali zimepungua kutoka 2,924 mwaka 2019 hadi 1,864 mwaka 2021 na ajali 1,933 ziliripotiwa mwaka 2020. Ajali zinazosababisha vifo zimeongezeka kutoka 1,031 mwaka 2020 hadi 1,038 mwaka 2021.
Vifo vilivyoripotiwa kusababishwa na ajali mwaka 2021 vilikuwa 1,368 sawa na wastani wa kila ajali ilisababisha kifo cha mtu mmoja. Pia, majeruhi waliotokana na ajali za barabarani waliongezeka kutoka 2,362 mwaka 2020 hadi 2,452 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 3.8.
Machi 29 mwaka huu, Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO) mkoa wa Iringa, Mosi Ndozero aliwanasa madereva wa mabasi wa matatu baada ya kuweka mtego, wakiendesha kwa mwendo kasi huku wakikimbizana.
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Meloe Buzama akizungumza mwishoni mwa wiki wakati akipokea vifaa hivyo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri Ardhini (Latra) ambavyo ni kompyuta na runinga zitakazowekwa Makao Makuu ya Polisi nchini na nyingine eneo la Msamvu, mkoani Morogoro, alisemasasa Serikali inatafuta mawakala wa ndani au nje kuleta vifaa vitakvyotumika na vitafanyiwa majaribio kuona utendaji wake.
“Tukimpata tunaanza kufunga, mpango huu mpya wa kamera utasaidia kuonyesha namna dereva anvyoendesha, ili anapofanya kosa achukuliwe hatua,”alisema Meloe.
Akizungumzia vifaa walivyokabidhiwa, alisema ni msaada mkubwa kwao kwa kuwa vitasaidia kuongeza ufanisi wa kazi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Latra, Profesa Ahmed Mohamed Ame alisema mpango huo mpya wa kamera katika maneno mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia magari yote na kubaini mwenendo mzima wa uendeshaji barabarani kwal engo la kupunguza ajali.
Alibainisha mfumo huo utaoanishwa na mfumo wa ufwatiliaji mwenendo wa mabasi (VTS) unaosimamiwa na Latra kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
“Mchakato wa kutekeleza mfumo huo mpya ambao ni kamera za barabarani na utafanya kazi na mfumo wa VTS utawezesha kuongeza usalama kutokana na ajali za barabarani kuwa nyingi kutokana na ukiukwaji wa sheria,” alisema Profesa Ame.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Latra, Habibu Suluo alisema mfumo wa VTS una uwezo wa kuona basi lilipo na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Alisema mfumo huo unapunguza ajali barabarani na unaokoa maisha ya watu wengi, na kulitaka Jeshi la Polisi kutumia vema vifaa hivyo kwani vimenunuliwa na wananchi.
Walichosema wadau
Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani alisema, “hata uko Ulaya ambako hizo kamera zimefungwa sehemu zote kuna watu wanavunja sheria kusudi, kwetu itasaidia umakini utaongezeka hawatajisahau wakijua watarekodiwa.”
Alisema zikifungwa nchi nzima itakuwa faraja si kwa madereva wa malori pekee, bali wote hata wa mabasi na hata kwa madereva walevi wataacha tabia hiyo.
“Kamera hizo zitafichua ukweli kwa sababu wakati mwingine madereva hawasababishi ajali, isipokuwa bodaboda na magari madogo na baiskeli wakiona kamera watakuwa wanaongeza umakini wakiingia barabarani,”alisema.
Mkurugenzi wa habari Chama Cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema pamoja na hatua hiyo nzuri, muundo mzima wa upatikanaji wa madereva unapaswa kufumuliwa.
“Inapofikia mtu unataka kuendesha gari ni muhimu kuingia darasani na si mtu kuingia darasani wiki mbili hususani masafa marefu lazima kuwepo madereva maalumu wanaoweza kuendesha,”alisema
Kaimu Katibu Mtendaji wa Latra CCC, Leo Ngowi aliyedai hatua hiyo inaenda kubadilisha tabia ya madereva na ni mfumo ambao unatumiwa na mataifa mengi hasa yaliyoendelea huku akiwaomba wananchi kuunga mkono juhudi hizo.
Mitazamo hiyo ilitofautiana na Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa madereva (TADWU) Shubert Mbakizao, aliyedai ajali nchini hawezi kupungua kwa kufungwa kamera isipokuwa wasimamizi wa sheria wanapaswa kuingia lawamani.
“Kulegalega kwao kusimamia sheria ndipo ajali zinajitokeza na Bibilia inasema rushwa upofusha macho, sasa kama maaskari wana vinasaba na rushwa na wanakula mipango na wamiliki wa mabasi ajali haziwezi kuisha,” alisema.