Tija ya ziara, safari za Samia 2022

Rais Samia Suluhu Hassa, akizungumza na wananchi katika moja ya ziara zake alizofanya katika maeneo mbalimbali nchini. Picha ya Maktaba
Muktasari:
- Urais huenda ukawa ndio wadhifa unaobeba majukumu mengi zaidi ukilinganisha na nyingine zote nchini na hivyo kumfanya mtu anayeshika nafasi hiyo kugubikwa na shughuli lukuki.
Dar es Salaam. Urais huenda ukawa ndio wadhifa unaobeba majukumu mengi zaidi ukilinganisha na nyingine zote nchini na hivyo kumfanya mtu anayeshika nafasi hiyo kugubikwa na shughuli lukuki.
Ushahidi wa hili ni wingi wa shughuli zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha mwaka 2022, zikiwemo zile alizoonekana hadharani, kadhalika alizofanya akiwa ofisini kwa kuketi vikao mbalimbali na wateule na wageni.
Kwa ujumla tangu uanze mwaka 2022 mpaka sasa, Rais Samia amefanya ziara 16 za nje ya nchi katika mataifa kadhaa yakiwemo Senegal, Marekani, Ubelgiji na Msumbiji.
Januari
Pazia la majukumu ya Rais Samia hadharani alilifungua Januari 5, kwa kupokea taarifa ya mpango wa awamu ya kwanza wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19, Ikulu ya Dar es Salaam.
Shughuli hiyo ilifuatiwa na uapisho wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, kadhalika viongozi wengine aliowateua. Hiyo ilikuwa Januari 10 Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.
Safari ya kwenda Zanzibar alipokutana na Rais wa Visiwa hivyo, Dk Hussein Ali Mwinyi ni shughuli aliyoifanya Januari 11, ambako huko alifungua kiwanda cha nguo cha Basra Textile Mills Ltd na Januari 12, alihudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya mapinduzi ya Zanzibar.
Mbali na Dodoma na Dar es Salaam, kwa Tanzania Bara Rais Samia alisafiri kwenda mkoani Kilimanjaro Januari 22, lilikofanyika tamasha la kwanza la utamaduni, siku ambayo alisimikwa uchifu na kupewa cheo cha Chifu Hangaya.
Januari 24 alishiriki sherehe za mwaka mpya kwa mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini, ilifanyika Dar es Salaam na kesho yake Januari 25 alizungumza na viongozi wa machinga Ikulu ya Dar es Salaam.
Safari ya kwanza ya Rais Samia kwenda nje ya nchi mwaka huu ilikuwa Januari 28, aliposafiri kwenda Msumbiji kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na Rais wa nchi hiyo, Phillip Nyusi.
Februari
Kutoka nchini Msumbiji, Rais Samia aliporejea nchini Februari 2 alishiriki kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria jijini Dodoma, kisha Februari 4 alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa International Finance Cooperation (IFC) Makhtar Sop Diop Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Februari 6 alitembelea Hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Mara, alikoendelea na ziara hadi Februari 7.
Ziara ya pili ya Rais Samia nje ya Tanzania aliifanya Februari 9 aliposafiri kwenda Ufaransa kwa siku tano kisha Ubelgiji Februari 15 kwa siku tano hadi Februari 20 aliporejea nchini.
Februari 22 alikwenda mkoani Geita kuhudhuria sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya utumishi wa Kiaskofu na Februari 26 alisafiri kwenda Dubai kwa ajili ya kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji na alirejea Februari 28.
Machi
Machi 3, Mkuu huyo wa nchi alikutana na viongozi wa dini Ikulu jijini Dar es Salaam na Februari 4 alikutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe baada ya kutoka rumande alikokaa kwa miezi tisa kwa tuhuma za ugaidi.
Rais Samia alitimiza ahadi yake ya kutembelea shule ya Sekondari Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Machi 7 na siku mbili baadaye alisafiri kwenda visiwani Zanzibar kuwajulia hali wagonjwa na kuzungumza na Wazee wa Kusini Unguja Machi 10 na Machi 14 aliunda kikosi kazi kuimarisha demokrasia.
Machi 22 alikutana na kikosi kazi hicho na kesho yake alihutubia kilele cha wiki ya maji, ratiba iliyofuatiwa na uzinduzi wa nyumba za Magomeni Kota.
Aprili
Aprili 5, alifungua mkutano wa maridhiano, haki na amani ulioratibiwa na taasisi ya demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dodoma na siku mbili baadaye alishiriki maadhimisho ya siku ya Karume.
Aprili 10 alihutubia mdahalo wa miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere na Aprili 19 alisafiri kwenda nchini Marekani kwa ajili ya uzinduzi wa filamu ya Royal Tour na alifanya hivyo Aprili 28 nchini Tanzania.
Mei
Mei Mosi, Mkuu huyo wa nchi alishiriki maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani na Mei 10 alikwenda nchini Uganda kwa ziara ya kikazi.
Siku tatu baadaye, Rais Samia alishiriki maadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mei 17 alianza ziara mkoani Tabora na Mei 22 alipokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.
Juni
Juni 3 alifungua mkutano wa tisa wa chama cha makatibu muhtasi na Juni 7 alifungua mkutano wa baraza la taifa la biashara jijini Dodoma, ratiba mbayo ilifuatiwa na ziara ya kikazi mkoani Kagera Juni 9.
Mkuu huyo wa nchi alisafiri kwenda Oman kwa ziara ya kikazi na alirejea nchini Juni 16 na Juni 28 alihutubia wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya mfuko wa fursa sawa kwa wote, siku ambayo alimuapisha Mkuu mpya wa Majeshi, Jacob Mkunda.
Julai
Julai 5 Mkuu huyo wa nchi alishuhudia uwekaji saini mkataba wa ujenzi wa kipande cha reli ya kisasa cha kutoka Tabora hadi Isaka na Julai 7 alifungua jengo la afya ya mama na mtoto la hospitali ya CCBRT.
Julai 8 alikutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Uendeshaji wa Benki ya Dunia (IDA) Axel van Trotsenburg, Dakar, nchini Senegal alikokwenda kwa ziara ya kikazi.
Baadaye Julai 12, Mkuu huyo wa nchi alikutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Victoria Kwakwa na Julai 16 alikutana na kuzungumza na wazee wa Kusini Pemba.
Agosti
Agosti 2 Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema alizuru nchini na pamoja na mambo mengine alikutana na Rais Samia kwa mazungumzo kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Agosti 5, Rais Samia alianza ziara ya kikazi mkoani Mbeya, kisha Njombe na Iringa aliyoihitimisha Agosti 13.
Agosti 18, Rais Samia alianza ziara ya kikazi ya siku moja nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo na alikutana na Rais wa nchi hiyo, Felix Tsishekedi.
Septemba
Rais Samia alifungua kikao kazi cha maofisa wakuu waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi-Moshi Kilimanjaro Agosti 30.
Septemba 2, Rais Samia alizindua miradi mbalimbali ya Kizimkazi visiwani Zanzibar na kurejea Dar es Salaam Septemba 5, kisha alikutana na kuzungumza na Waziri wa Norway anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Masuala ya Nordic, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Oktoba
Oktoba 3, Mkuu huyo wa nchi aliwaapisha viongozi aliowateua na kesho yake alikwenda nchini Qatar na kuhutubia mkutano mkutano wa ubunifu wa afya duniani (WISH).
Oktoba 10 Rais Samia alikutana na kuzungumza na Katibu Mkuu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Women) Ikulu jijini Dar es Salaam na kuanza ziara yake mkoani Manyara.
Novemba
Novemba 3 Rais Samia alikutana na Rais wa Jamhuri ya China, Xi Jinping baada ya kuchaguliwa tena kuliongoza taifa hilo na Novemba 9, alikwenda nchini Misri kwa ajili ya kushiriki mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP27).
Novemba 11, Mkuu huyo wa nchi alizindua mradi wa maji wa Kigamboni na Novemba 17 alipokea hatia za utambulisho wa mabalozi sita.
Novemba 19 alishiriki Jubilee ya maadhimisho ya miaka Miaka 50 ya Kazi ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista wa Sabato na Novemba 22 alianza ziara ya kikazi mkoani Manyara.
Desemba
Desemba Mosi, alitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima ikiwa ni Shahada ya Udaktari wa Juu katika Humanitia na Sayansi Jamii na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dk Jakaya Mrisho Kikwete katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya chuo hicho katika ukumbi wa Mlimani City.
Desemba 13 alisafiri kwenda nchini Marekani kushiriki mkutano wa Agra uliowahusisha viongozi Wakuu wa Nchi za Afrika.
Wanachosema wachambuzi
Dk Richard Mbunda ni Mhadhiri wa Sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema suala sio wingi wa shughuli pekee, bali tija iliyopatikana.
Katika kipindi hicho, alieleza Mkuu huyo wa nchi amefanya shughuli nyingi zilizozaa matunda kwa maslahi ya nchi na wananchi.
“Utalii ndiyo alianza nao kwenye mambo ya Royal Tour, shughuli zake alizozifanya nchini kwa kiasi kikubwa zimechochea utekelezaji wa vipaumbele alivyoweka.
“Kwa maana nyingine hakuwa anahangaika bure bali aliyafanya aliyotafanya na tija imeonekana,” alisema.
Mbali na Dk Mbunda, Mhadhiri wa Diplomasia wa Chuo cha Diplomasia, Godwin Amani alisema katika kipindi hicho Rais Samia amebadilisha mtazamo wa kimataifa juu ya Tanzania.