TFS yabeba tuzo usimamizi bora wa fedha serikalini
Arusha. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeendelea kung’ara kitaifa baada ya kutwaa tuzo ya Usimamizi Bora wa Fedha kwa Taasisi zisizo za Kibiashara 2025 katika mkutano wa wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za serikali 2025 uliofanyika jijini Arusha.
Tuzo hiyo imekabidhiwa Agosti 24, 2025 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).
Tuzo hiyo imepokewa na mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa TFS, Piensia Christopher Kiure kwa niaba ya mwenyekiti wa bodi akiwa ameambatana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa TFS, Peter Mwakosya aliyemwakilisha kamishna wa uhifadhi.
Kwa upande wake, Piensia Kiure amesema ushindi huo ni matokeo ya nidhamu ya kifedha iliyojengwa tangu kuanzishwa kwa wakala huo mwaka 2011.
“Kwa miaka 14 sasa, TFS imekuwa ikipata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku mapato yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka. Tumeboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha, kuzingatia maelekezo ya serikali, wizara na bodi ya ushauri," amesema.
Ameongeza kuwa TFS imejijengea heshima kimataifa kupitia ushirikiano na nchi kama Brazil na Russia kubadilishana uzoefu wa sekta ya misitu hatua inayoiweka kwenye viwango vya ubora wa kimataifa.
“Tuzo hii ni chachu kwetu kuendelea kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu za serikali katika shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu. Ushirikiano wetu na wananchi umeendelea kuimarika, na tunatarajia mafanikio makubwa zaidi,” amesisitiza.
Kufuatia ushindi wa TFS, Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea tuzo kutokana na kuisimamia vizuri na kutoa mchango mkubwa kwa wakala ambayo imepokewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula.
Mkutano huo wa siku tatu umehudhuriwa na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za serikali ukiwa na ajenda ya kuimarisha uwajibikaji na utawala bora katika sekta ya umma.