Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Teknolojia yakwamisha hukumu ya Waziri mstaafu

Waziri mstaafu, Edgar Maokola Majogo.

Muktasari:

  • Edgar Maokola Majogo, aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, amemshitaki mpangaji wake kwa kukiuka masharti ya mkataba wa upangaji wa miaka 70, kuhusu ujenzi wa jengo alilopanga.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeshindwa kusoma hukumu ya kesi ya madai iliyofunguliwa na Waziri mstaafu, Edgar Maokola Majogo dhidi ya mpangaji wake, kampuni ya Catic International Engineering Tanzania Ltd, kutokana na tatizo la mfumo wa kimahakama.

Hukumu hiyo ilikuwa imepangwa kusomwa jana, Ijumaa, Mei 2, 2025, na Jaji Lusungu Hemed, aliyesikiliza kesi hiyo, lakini haikusomwa kutokana na changamoto ya mfumo wa kimahakama wa uendeshaji mashauri kimtandao.

Jaji Hemed amesema kuwa kutokana na tatizo hilo la kimfumo, ameshindwa kuona jalada la kesi hiyo pamoja na kesi nyingine zilizokuwa zimepangwa kusikilizwa leo, na hivyo kuziahirisha hadi tarehe nyingine ambayo wadaawa watajulishwa.

"Kutokana na changamoto hii, ninaahirisha mashauri haya mpaka tarehe nyingine, na pande zote zitajulishwa," amesema Jaji Hemed, akiahirisha kesi hiyo pamoja na nyingine zilizokuwa zimeitwa.

Majogo, aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na hayati Benjamin Mkapa, alifungua kesi dhidi ya kampuni ya Catic International Engineering Tanzania Ltd, ambayo ni mpangaji wa jengo lake lililoko katika Kiwanja Na. 7, Oysterbay, Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, Majogo aliyewakilishwa na Wakili Peter Madeleka, amedai kuwa kampuni hiyo ilikiuka masharti ya msingi ya mkataba wa upangaji walioingia mwaka 2008.

Kutokana na madai hayo, Majogo ameomba mahakama iamuru kampuni hiyo imlipe fidia ya jumla ya Dola milioni 3 za Marekani kwa kukiuka masharti ya mkataba huo, Dola milioni 2.88 kwa kuvunja sharti la kifungu cha 2(a), na Dola 120,000 kwa kuvunja sharti la msingi la kifungu cha 1(b) cha mkataba huo.

Kwa mujibu wa hati ya madai pamoja na ushahidi wa upande wa mdai uliowasilishwa mahakamani, Machi 1, 2008, pande hizo mbili ziliingia mkataba wa upangaji kuhusiana na Kiwanja Na. 7 kilichopo Oysterbay, Dar es Salaam, chenye Hati Na. 100376.

Katika mkataba huo, Majogo alitambuliwa kama mmiliki wa kiwanja na mpangishaji, huku kampuni ya Catic International Engineering Tanzania Ltd ikiwa mpangaji.

Mkataba huo uliweka sharti la msingi chini ya kifungu cha 2(a) kwamba mdaiwa (Catic) atajenga jengo la ghorofa tatu lenye vyumba vya makazi 24, pamoja na sakafu ya chini ya ardhi (basement), kwenye kiwanja hicho kwa gharama zake mwenyewe.

Chini ya kifungu cha 4(f) cha mkataba huo, pande zote mbili ziliruhusiwa, kwa njia ya mazungumzo na makubaliano ya pamoja, kufanya marekebisho au kuongeza kiambatisho chochote katika mkataba, ambacho kingekuwa sehemu rasmi ya mkataba huo.

Pia, kifungu hicho kiliruhusu kusitishwa kwa mkataba iwapo kutakuwa na makubaliano kati ya pande hizo.

Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, kampuni ya Catic ilitakiwa kuwa mpangaji wa jengo hilo kwa kipindi cha miaka 70, kuanzia Machi mosi, 2008 hadi Februari 28, 2078, huku ikilipa kodi ya pango ya kila mwezi kwa mujibu wa mkataba.

Kwa mujibu wa mkataba huo, katika kipindi cha miezi 12 ya mwanzo, mpangaji alitakiwa kumlipa mpangishaji (Majogo) kodi ya pango ya Dola 3,500 kwa mwezi, kuanzia tarehe ya kusaini mkataba.

Kuanzia mwaka wa pili mpaka mwaka wa 25 wa kipindi cha mkataba wa upangaji mpangaji huyo alipaswa kumlipa mpangishaji kodi ya pango ya Dola 5,000 kila mwezi, huku kuanzia mwaka wa 26 paka wa 50 alipaswa kulipa Dola 7,500, kila mwezi.

Kuanzia mwaka 51 mpaka wa 70 wa kipindi cha mkataba wa upangaji, mpangaji alipaswa kumlipa mpangishaji kodi ya pango ya Dola 10,000, kwa mwezi.

Hata hivyo, katika hati ya madai ya kesi hiyo na katika ushahidi wake, Majogo anadai kuwa mdaiwa (mpangaji), kinyume na kifungu cha 4(f) cha mkataba huo, alijenga jengo hilo bila basement, kinyume na kifungu cha 2(a) cha mkataba huo.

Majogo alidai kuwa kitendo cha mdaiwa kujenga jengo hilo bila basement, kinyume na kifungu cha 2(a) cha mkataba huo, kimepunguza thamani ya kiuchumi ya jengo hilo ambalo ni mali yake mdai.

Pia, Majogo anadai kuwa mdaiwa (mpangaji) alivunja sharti la msingi la mkataba huo chini ya kifungu cha 1(b) kwa kushindwa kumlipa kodi ya pango kwa miaka 2023 na 2024.

Majogo anadai kuwa licha ya madai na maombi kadhaa kuhusu ujenzi wa basement na malipo ya kiasi kinachodaiwa kama ilivyoelezwa hapo juu, mdaiwa amekataa na/au amepuuza kuyatekeleza.

Kutokana na sababu hizo ndipo Majogo alipofungua kesi hiyo akiiomba mahakama hiyo imuamuru mdaiwa kumlipa fidia hiyo ya jumla ya Dola milioni 3 za Marekani.

Pia, anaiomba mahakama itoe amri ya kumtimua mdaiwa katika jengo hilo na yeye mdai arejeshewe umiliki wake, na pia aliomba mahakama imuamuru mdaiwa amlipe riba ya asilimia tano kwa mwaka ya kiasi cha jumla ya fidia anayoidai.

Vilevile Majogo anaiomba mahakama imuamuru mdaiwa alipe gharama za kesi hiyo na gharama nyinginezo zinazohusiana na pia itoe nafuu nyingine yoyote ambayo itaona inafaa kuitoa.