Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TCRA yatia neno Clubhouse kupotea, kurejea Tanzania

Muktasari:

  • Baada ya kutopatikana kwa takriban saa 12 hatimaye mtandao wa Clubhouse umerejea nchini Tanzania huku Mamlaka ya Mawasiliano ikitaja sababu ya kiufundi.

Dar es Salaam. Siku moja tangu utokee mkwamo wa upatikanaji wa mtandao wa Clubhouse nchini, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema haikuufungia bali kulikuwa na changamoto za kiufundi, lakini umesharejea.

Mtandao huo ambao watu huutumia kuwasiliana kwa sauti, kufanya mikutano na mijadala mbalimbali, ulianza kusuasua kupatikana jana na kuibua malalamiko mitandaoni.

Kutokana na kadhia hiyo, katika ukurasa wake wa twitter, Mwanasheria Bob Wangwe ameandika akimtaka Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye arudishe mtandao huo.

“Haya mambo ya enzi za giza hayapaswi kuendelea katika zama hizi tunazodhani ni zama nuru. Tanzania ni nchi huru acheni kuiongoza kama mnavyoongoza familia zenu,” ameandika.

Msemaji wa sekta ya mawasiliano, teknolojia na uchukuzi wa Chama cha ACT Wazalendo, Macheyeki Philbert amehusisha changamoto ya kupatikana kwa mtandao huo na hofu za baadhi ya watendaji wa Serikali.

Ameandika pamoja na dhamira njema ya Rais Samia Suluhu Hassan juu ya uhuru wa habari na kutoa maoni bado kuna watendaji wanahofu.

Katika ukurasa wake huo, ameandika hofu hizo zinatokana na maslahi binafsi akisisitiza: “Wanapata kigugumizi katika kulitekeleza hili kizalendo. Mheshimiwa Nnauye na Mmalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tushirikiane kuitoa nchi katika giza.”

Malalamiko dhidi ya kutopatikana kwa Clubhouse yamemuibua, Buberwa Kaiza, mtaalamu wa sheria, aliyeandika ni dhahiri Serikali itakuwa na nia mbaya, kwani uhuru wa kupata taarifa ni haki ya binadamu akihoji: “Tuanzishe mashtaka ya umma?”

Hata hivyo, watumiaji wa mtandao huo wamelazimika kuwa na program tumizi ya mfumo wa usalama wa mtandao ‘Virtual Private Network’ (VPN) kama kifaa kisaidizi cha kutumia Clubhouse.

Alipotafutwa na Mwananchi Digital leo Februari 16, 2023 kulizungumzia hilo, Mkurugenzi wa TCRA, Dk Jabir Bakari amesema si kwamba ulifungiwa bali kulikuwa na tatizo la kiufundi.

“Kulikuwa na tatizo la kiufundi. Limeisha na unapatikana,” amejibu mkurugenzi huyo bila kufafanua kwa kina tatizo hilo.

Ni kweli Mwananchi Digital ilipomaliza kuzungumza na Dk Bakari, mtandao huo ulirejea na ulipatikana bila msaada wa VPN.

Hii si mara ya kwanza kwa mitandao kupata tatizo nchini, iliwahi kutokea hivyo kwa mtandao wa Twitter, muda mchache kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2020.

Ingawa mamlaka hazikuweka wazi sababu za kufanya hivyo, kitendo hicho kilihusishwa na vuguvugu la kisiasa lililokuwepo wakati huo.

Kupitia tovuti yake twitter iliandika: “Tunashuhudia mtandao wetu kuminywa Tanzania” huku ikiongeza kufanya hivyo kuna madhara na uvunjaji wa haki za binadamu.