TCRA kuja na katuni za watoto kulinda maadili

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari
Dar es Salaam. Katika jitihada za kukabiliana na maudhui yasiyofaa Mamlaka ya mawasiliano TCRA imesema inashirikiana na mzalishaji binafsi kutengeneza katuni za watoto.
Suala la kuwepo kwa katuni zisizoendana na maadili ya Kitanzania limekuwa likiibuka na kuzua minong'ono miongoni mwa watu huku TCRA ikirushiwa lawama kwa kutodhibiti maudhui hayo.
"Katika suala la katuni zisizofaa kwa watoto, TCRA kwa kushirikiana na mzalishaji binafsi ili kuzalisha katuni zenye viwango vya juu kwa ajili ya watoto, vilevile tunarekodi michezo ya kitamaduni ya makabila 120 ambayo nayo itakuwa katika ubora wa hali ya juu," alisema Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Jabiri Bakari katika taarifa ya mamlaka hiyo kwa vyombo vya habari.
Dk Jabiri alisema majukumu ya TCRA ni zaidi ya zaidi ya kuwezesha huduma za matangazo kwani mamlaka hiyo inajukumu la kuhakikisha maudhui yanayorushwa yanafuata maadili ya uandishi wa habari, yanazingatia sheria za nchi, kulinda maadili na urithi wa Taifa.
"Juhudi zetu za kupigia chapuo maudhui ya ndani zilo wazi kwani tumeanzisha ushirika na vituo 14 vya habari kuzalisha maudhui mahususi kwa ajili ya elimu ya familia na vijana," alisema Jabiri na kuongeza kuwa juhudi hizo na nyingine wanazifanya kwa kushirikiana na Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na watoto.
Dk Jabiri alisema zaidi wanaratibu vipindi vya maadili vinavyozalishwa na vituo vya habari vya wilaya 150 ili visaidie kutoa elimu na kujenga jamii yenye misingi, maadili na utamaduni wa Watanzania.