Tasaf, Tanroads zakalia mamilioni ya fedha za wananchi

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22, imebaini hundi zilizochacha zenye thamani ya Sh352.12 milioni zilitolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa waathirika wa miradi miwili mkoani Dodoma.
Hali kadhalika, CAG alibaini kuchelewa kulipa fidia kwa waathirika wa miradi ya Sh11.7 bilioni kwa waathirika wa miradi iliyoko chini ya Tanroads.
Mbali na hilo, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) haukupeleka Sh651.85 milioni zilizoidhinishwa kwenda kwenye miradi tisa katika Wilaya za Ludewa na Makete mkoani Njombe kwa watu 186 wanaoishi katika kaya hatarishi.
Katika ripoti ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa juzi bungeni, CAG Charles Kichere aliitaja miradi ambayo waathirika walipata hundi zilizochacha ni mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato na Barabara ya Mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma kwa Kiwango cha Lami (112.3 km).
Alisema kanuni za fedha za umma za mwaka 2001 (zilizorekebishwa 2004) zinahitaji kulinganishwa kwa taarifa za kibenki na daftari la fedha husika kila mwezi na kuwa hundi iliyochacha hutambuliwa ikiwa haijawasilishwa benki kwa malipo kwa siku zinazozidi 180 au miezi sita.
Alisema hivyo, hundi iliyochacha huwa haiwezi kulipwa na benki, lakini ukaguzi wake ulibaini hundi zilizochacha zilizotolewa kwa waathirika wa miradi zenye thamani ya Sh352.12 milioni.
Alisema hali hiyo, ilisababishwa na uwepo wa malalamiko na migogoro baina ya waathirika wa miradi ambayo ilisababisha kutochukua hundi hizo zili,zoandikwa kwao kwa ajili ya malipo.
“Ninapendekeza Wakala wa Barabara kuwasiliana na waathirika wa miradi na kuwapatia hundi zao kwa wakati bila kuchelewa zaidi,” alisema.
Ucheleweshaji wa fidia
Kichere alisema alibaini kuna ucheleweshaji wa kulipa fidia kwa waathirika wa miradi ambapo Sh11.37 bilioni zilizopaswa kulipwa katika miradi mitatu iliyochini ya Tanroads zimecheleweshwa.
Alibaini Sh512.34 milioni zilizokuwa zitolewe kwa waathirika wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kimataifa ya Bagamoyo – Horohoro /Lunga - Lunga Malindi unaotekelezwa na Tanroads hazikulipwa kwa waathirika wa mradi 422.
Alisema hali hiyo ilitokana na mchakato mrefu wa malipo ya fidia kwa waathirika wa miradi na hivyo kushindwa kulipa fidia kwa waathirika wa mradi ndani ya miezi sita.
Pia alibaini mradi wa miundombinu ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) awamu ya pili unaotekelezwa na Tanroads ulikuwa na madai ya fidia yenye thamani ya Sh4.63 bilioni kwa waathirika 15 wa mradi kwa zaidi ya miaka miwili.
Kichere alisema ulibaini madai ya fidia kwa waathirika 1,039 wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato yenye thamani ya Sh6.22 bilioni ikijumuisha madai halisi Sh3.92 bilioni na riba ya Sh2.3 bilioni hayajalipwa.
“Kuchelewesha malipo ya fidia kwa waathirika wa miradi kunasababisha Serikali kulipa riba isiyostahili ya ucheleweshaji ambayo ingeweza kuepukwa kwa kulipa fidia kwa wakati kulingana na ripoti ya tathmini ya mwaka 2011,” alisema.
Alipendekeza Tanroads kuharakisha malipo ya fidia kwa waathirika wa miradi yenye thamani ya Sh11.37 bilioni kwa waathirika wa miradi 1,476.
Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila aliyesema alikuwa safarini na kwamba hawezi kuzungumza chochote mpaka aelewe maeneo waliyoguswa.
“Nilikuwa nimewaambia watu wangu tupate hiyo ripoti tuone maeneo ambayo yanatuhusu na namna ya kuyajibu,” alisema.
Kaya hatarishi hazikulipwa
Kichere alibaini Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) haukupeleka Sh651.85 milioni zilizoidhinishwa kwenda kwenye miradi tisa katika Wilaya za Ludewa na Makete mkoani Njombe kwa watu 186 wanaoishi katika kaya hatarishi.
CAG alisema Tasaf inatekeleza mradi Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) kwa jumla ya wanufaika 186 wanaoishi kwenye kaya hatarishi katika wilaya hizo mbili.