Tarura yabuni mkakati kuokoa gharama ujenzi wa barabara, madaraja

Muktasari:
- Matumizi ya mawe na matofali ya kuchoma yametajwa kuwa njia rafiki, inayotunza mazingira na kuokoa gharama kubwa za ujenzi wa miundombinu.
Dar es Salaam. Kukosekana kwa fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja kuliifanya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kuja na mbinu mpya ya utumiaji wa mawe na matofali katika kujenga miundombinu hiyo.
Utumiaji wa vifaa hivyo kumetajwa kupunguza gharama za ujenzi kwa takribani asilimia 50 ikilinganishwa na zile ambazo zingetumika ikiwa madaraja na barabara hizo zingejengwa kwa kutumia lami.
Takwimu za Tarura zinaonyesha kuwa katika barabara za urefu wa Kilomita 28.6 zilizojengwa kwa kutumia teknolojia ya mawe, jumla ya Sh10 bilioni zilitumika hadi kumalizika kwake ikiwa ni ndogo ukilinganisha na Sh16 bilioni ambazo zingetumika ikiwa lami nyepesi ingetumika katika ujenzi na Sh42 bilioni ikiwa ingetumika lami nzito.
Akizungumzia suala hili, Mhandisi Mshauri kutoka Tarura, Pharles Ngeleja amesema ujenzi wa kutumia mawe haupunguzi tu fedha ambazo zingeweza kutumika bali pia uchafuzi wa mazingira unapunguzwa kwa asilimia 75 kwani ujenzi wake haihitaji mitambo mikubwa.
“Ni rahisi pia kufanya matengenezo, kwa mfano ikitokea shimo sehemu wakala hauhitaji kubeba vifaa vingi ikiwemo magari kwenda kuziba shimo lililotokea na badala yake wanaweza kwenda watu wawili katika sehemu ambayo imepata changamoto na kazi kufanyika wakitumia malighafi zilizopo,” amesema Ngeleja.
Matumizi ya mawe pia yamesaidia kuiepusha Tarura na wizi wa vifaa vya ujenzi ambavyo hushuhudiwa katika baadhi ya maeneo kwani ni vigumu watu kuiba mawe makubwa.
Akizungumzia namna ambavyo gharama za ujenzi zinapungua Dk Makene alitolea mfano wa daraja la Mwanagati jijini hapa ambalo awali lilisanifiwa kwa Sh1.7 bilioni lakini baada ya kufanyika kwa usanifu wa ujenzi wa daraja hilo kwa kutumia mawe basi litakwenda kutumia Sh856 milioni.

“Hivyo utaona tofauti hapo zaidi ya Sh12 milioni zimeokolewa ni rahisi na hadi sasa tangu mwaka 2017 tulipoanza kutumia teknolojia hii madaraja 481 yamejengwa kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali ya kuchomwa,” amesema.
Akifafanua zaidi unafuu katika ujenzi, alitolea mfano wa Mwanza ambapo alisema wastani wa ujenzi wa Kilomita moja ya barabara ya mawe ni Sh390 milioni, ukitumia lami nyepesi ni Sh550 milioni na ikiwa utaamua kutumia lami nzito ni Sh1.3 bilioni.
Kwa upande wa Kigoma, ujenzi wa Kilomita moja ya barabara ya mawe ni Sh350 milioni, ukitumia lami nyepesi ni Sh550 milioni na ukitumia lami nzito ni Sh1 bilioni.
“Teknolojia hii iko maeneo mengi ikiwemo China wamekuwa wakiitumia, ujenzi huu ni imara, hata magari makubwa na mazito yanaweza kutumia madaraja haya huku uhai wake tangu kujengwa ukiwa ni miaka zaidi ya 100,” amesema Ngeleja.
Kaimu Mtendaji mkuu wa Tarura, Ismaily Mafita amesema matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya madaraja, huongeza ufanisi, huokoa muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu.
“Tarura imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi. Hata hivyo wakala unaendelea na matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi,’
“Pia tunatumia utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira,” amesema.
Akizungumzia utendaji wa Tarura amesema mkoa wa Dar es salaam katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 uliidhinishiwa Sh68 bilioni kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya Barabara Km 1,151.987 ambapo lami km 26.04 na madaraja na Kalavati 38.
Maendeleo ya utekelezaji kwa Mipango ya mwaka 2024/2025 yanahusisha utekelezaji wa kimaumbile na kifedha ambapo utekelezaji hadi kufikia Desemba 2024 wa kimaumbele ni asilimia 53