Tanzania mbioni kutumia umeme wa jotoardhi

Muktasari:
- Lengo ni kuiwezesha Tanzania kufikia ajenda ya mwaka 2025 ya upatikani wa nishati ya umeme wa uhakika.
Mbeya. Tanzania iko mbioni kuondokana na changamoto ya kukatika kwa nishati ya umeme kufuatia kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ya Uendelezaji Jotoardhi Ardhi (TGDC) kuja na mpango wa kuviongezea nguvu vituo mbadala hasa 50 vilivyopo katika mikoa 16 nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba amebainisha hayo leo Machi 21, 2024 kwenye mkutano uliowakutanisha wanasayansi wabobevu kutoka mataifa mbalimbali wa Marekani, Newzland, Japan, Iceland, Kenya Rwanda na Ethiopia.
Lengo la mkutano huo ni kujadili na kupata mapendekezo ya namna ya bora ya kuanza uchimbaji wa nishati ya jotoardhi katika Mradi wa Ngozi uliopo Wilaya ya Mbeya ambao awamu ya kwanza utazalisha megawati 30 ifikapo mwaka 2025 huku lengo likiwa ni kuzalisha megawati 70.
“Kwa kushirikiana na wanasayansi wabobevu tumefanya tafiti za kisayansi na kubaini kuwepo kwa kiwango kikubwa cha jotoardhi katika mradi wa ngozi sambamba na uwepo wa vyanzo vingine 50 katika mikoa 16 nchini ambavyo vikiongezewa nguvu Tanzania itaondokana na adha ya upatikanaji wa nishati ya umeme iliyotokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameikumba dunia,” amesema Mwangomba.
Mhandisi Mwangomba amesema kutokana na ajenda ya Serikali ya mwaka 2025 kuhakikisha tatizo la umeme ni historia, TGDC imekuja na mwarobaini wa kuhakikisha vyanzo mbadala vinaongezewa nguvu na kuwepo na nishati bora na rafiki kwa mazingira.
“Tunakwenda kutekeleza agizo la Waziri Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko la kuanza uzalishaji katika Mradi wa Ngozi kuanzia Aprili Mosi, 2024 kwa sasa tupo katika hatua nzuri za kuandaa wataalamu, mtambo na taratibu za manunuzi,” amesema Mwangomba.
“Tafiti za kitaalamu za wanasayansi wabobevu tunapaswa kuanza kuchimba umbali wa mita 1,200 mpaka kukutana nyuzi joto 250 kwa teknolojia za kisasa,” amesema.
Mwangomba amesema uwepo wa nishati ya jotoardhi utakuwa chachu kubwa ya kuchochea pato la Taifa, ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi na upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Amesema mkutano huo wa pili kufanyika nchini unaokutanisha wanasayansi wabobevu, unatokana na upatikanaji wa matokeo mapya ya kisayansi katika Mradi wa Ngozi eneo la Magharibi na Kusini Mashariki.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara (TGDC) Mhandisi Shakiru Kapugus amesema kati ya megawati 70 za jotoardhi zinazokwenda kuzalisha, megawati 30 zitawashwa mapema mwaka 2025.
“Watanzania wajiandae kuingia kwenye matumIzi ya nishati mbadala ya jotoardhi ambayo ni rafiki wa mazingira na kwenda kuondoa kabisa tatizo la umeme sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na pato la Taifa,” amesema.
Amesema wanaishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa kwa Taifa unaokwenda kuandika historia ya kutatua tatizo la umeme ifikapo mwaka 2025.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batega amesema Tanzania imechelewa kuingia katika teknolojia ya matumizi ya nishati ya jotoardhi na kwamba uwepo wake ukawe chachu na fursa ya kiuchumi na ajira.
“Tanzania sasa ndio tunaanza safari ya kutengeneza nishati mchanganyiko, yako mataifa mengine yamewekeza zaidi ya matumizi ya umeme wa jotoardhi, hivyo ni matarajio ya Serikali kupitia TGDC tunakwenda kuondokana na adha ya umeme na ndiko dunia tunapaswa kwenda huko,” amesema.
Mfanyabishara Nassoro Mussa amesema ujio wa mradi wa jotoardhi ni fursa pekee itakayosaidia ongezeko la ajira, mapato kwa Serikali na kuwa mwarobaini wa tatizo la kukatika katika kwa umeme kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.