Tanzania kujifunza mbinu, teknolojia kimataifa kuwainua wavuvi wadogo

Muktasari:
- Mkutano wa Kimataifa wa nchi wanachama wa OACPS, unatarajiwa kufanyika kwa siku tano nchini, ukiwa na lengo la kujadili uchumi wa buluu na kuweka mkakati wa pamoja kuimarisha sekta ya uvuvi unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano JNICC jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Tanzania inatarajia kujifunza mbinu na teknolojia mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi kutoka nchi zilizoendelea, ili kuwainua wavuvi nchini ambao wengi wao ni wadogo.
Waziri Ulega amesema hayo leo Jumatatu Septemba 9, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kuufungua mkutano wa nane wa mawaziri wanaoshughulikia uvuvi, bahari na maji ya ndani kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) ambao unawawakilishi kutoka nchi 78 wanachama.
“Tunajadiliana jinsi tunavyosaidia wavuvi wadogo, ambao ni asilimia 95 ya wavuvi nchini. Tutatumia fursa hii kujifunza kuhusu teknolojia na kubadilishana maarifa na wenzetu waliopiga hatua katika sekta hii,” amesema Waziri Ulega.
Katika hilo, amesema wanaangalia namna ya kuwawezesha wavuvi hao kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea teknolojia na ukuaji wa idadi ya watu, amesisitiza lazima nchi iondoke kwenye uvuvi uliozoeleka na kwenda kwenye ule wa kisasa.
Amesema kwa sasa uharibifu wa mazingira upo katika kiwango kikubwa, jambo ambalo linaathiri hadi bahari mito na maziwa hivyo wanajadiliana namna ya kukabiliana na hali hiyo kwa manufaa ya wavuvi na nchi zote.
Hivyo, amesema majadiliano yatajikita katika kuboresha mbinu zao za uvuvi kwa njia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kupandisha mapato ya mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla.
“Mkutano huu unawakutanisha pamoja mawaziri, maofisa wa ngazi za juu na wadau muhimu kutoka nchi za OACPS, ili kujadili masuala muhimu ya sera za kimataifa na kanda, ikiwa ni pamoja na uvuvi na kilimo cha samaki, shughuli za baharini, na uchumi wa buluu.
“Kuna nchi ambazo uchumi wao unategemea sana baharini na ambazo zimewekeza katika teknolojia mbalimbali kama uvuvi mabwawa. Tutabadilishana uzoefu na nchi hizi, ili kujua mafanikio na vikwazo vyao, azma ni kuweza kushughulikia changamoto na kuimarisha uwezo wa Taifa letu,” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali itaanza kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani 'Drones' ili kupambana na uvuvi haramu. Amesema matumizi ya ndege hizo yataanza katika mwaka huu wa fedha wa 2024/2025 ili kuendelea kupambana na uharamia huo.
Amesema teknolojia ya dunia imekua na inazidi kutanuka kila kukicha, hivyo ni umuhimu wa matumizi ya ndege hizo utasaidia kuokoa gharama za matumizi ya doria kwa maofisa wanaopambana na aina hiyo ya uvuvi iliyokatazwa.
"Badala ya maofisa wetu kufanya doria muda wote kuzunguka huku wakitumia fedha za umma, kumbe tunaweza kupata taarifa kupitia Drones yenye kuchunguza maeneo ya uvuvi haramu," amesema.
Amesema wasimamizi watakuwa na taarifa za hakika hivyo watakuwa wanakwenda moja kwa moja eneo tajwa. Amesema kwa sasa zimekuwa zikitumika gharama na wakati mwingine wakienda hawakuti kile walichoelezwa.
'Dunia hii ni ya kisasa na ya kisayansi hatuwezi kwenda kwa njia ya kubahatisha hatuwezi kuwa na njia zilezile miaka yote. Teknolojia hii inakwenda kutusaidia kupambana na uvuvi haramu kama mataifa ya wenzetu ambao wameshapiga hatua kubwa," amesema.
Wakati Ulega akiyasema hayo, kumekuwa na juhudi mbalimbali za kupambana na uvuvi haramu ikiwemo boti maalumu iliyoletwa Jumapili, Aprili 21, 2024 pamoja na operesheni mbalimbali za kupambana na uvuvi huo.
Aidha, amesema kwa sasa mchango wa sekta ya uvuvi nchini ni asilimia 1.9 huku malengo yakiwa zaidi ya asilimia tatu hadi ifikapo mwaka 2030.
"Kwa miaka mitano mwenendo wa uuzaji nje mazao ya uvuvi tumekuwa tukienda vizuri, tumeuza Sh2.2 trilioni za samaki, huku ushuru wa Serikali ukiwa ni zaidi ya Sh98 bilioni kuanzia mwaka wa fedha 2019/23.
Kwa ujumla, akitaja faida za mkutano huo, amesema utasaidia kuchechemua uchumi kupitia wageni kula, kulala katika hoteli zilizopo hapa nchini pamoja na kupanda magari ya Tanzania.
"Pili, ni heshima kwa taifa letu kutokana na amani na usalama uliopo hapa lakini pia tunatangaza vivutio vyetu kama Mlima Kilimanjaro, Zanzibar, Ngorongoro, Serengeti ambavyo tunatamani watu wavijue zaidi," amesema.