Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu mpya kudhibiti migogoro ya wakulima, wafugaji Tanzania

Waziri Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akimueleza jambo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN),  Earle Courtenay Rattray wakati walipotembelea Shamba la Serikali la Mbegu za malisho aina ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani.

Muktasari:

  • Umoja wa Mataifa umesema unaridhishwa na maendeleo ya matumizi ya teknolojia ya uzalishaji wa malisho aina ya Juncao, huku Serikali ikisema nyasi hizo zitakuwa mwarobaini wa changamoto za malisho.

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema teknolojia ya uzalishaji wa malisho aina ya Juncao iliyoanza kutumika nchini,  ni suluhisho la kumaliza changamoto za malisho ya mifugo inayowakabili wafugaji kwa nyakati tofauti.

Nyasi za Juncao zenye asili ya China zinaweza kutumiwa pia kuzalisha uyoga unaoweza kutumiwa pia kama chakula cha wanyama, mbolea, mafuta ya majani na nyenzo ya bidhaa za mafuta yanayokuwa katika ubora wa hali ya juu katika mazingira rafiki.

Waziri Ulega ameeleza hayo leo Ijumaa Agosti 9, 2024 alipotembelea shamba la Serikali la mbegu za malisho ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani.

Katika ziara hiyo, Ulega aliambatana na ugeni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) waliowakilishwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Earle Courtenay Rattray waliokwenda kujionea maendeleo ya teknolojia hiyo.

Waziri Ulega, amesema uwepo wa malisho yanayotokana na Juncao utawezesha kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima, huku akisema katika shamba hilo wamepanda majani ya Juncao ekari 21 kuanzia mwaka 2021 hadi 2024.

“Mbegu zilizozalishwa ni kilo 178,262, huku zaidi ya wakulima 957 wakishiriki kulima majani ya Juncao kwa hatua tofauti tofauti.

“Juncao ni sehemu katika programu ya tutunzane ‘Mvomero’ iliyozinduliwa na  Rais Samia Suluhu Hassan inayolenga kuhamasisha wafugaji kulima malisho katika maeneo yao, kuhifadhi mazingira na kupunguza migogoro kati yao na wakulima,” amesema Waziri Ulega

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa mchango wake wa kuwajengea uwezo wataalamu mbalimbali katika wizara yake ikiwemo kuifahamu vema teknolojia hiyo ya ulimaji majani ya Juncao.

“Teknolojia hii tumeichukua kama ni suluhu ya mahitaji ya malisho katika Taifa letu,” amesisitiza Waziri Ulega.

Naye, Balozi Rattray ameelezea kufurahishwa na maendeleo ya Juncao, akimpongeza Rais Samia kwa kuonesha utayari wa kuipokea teknolojia hiyo inayotarajiwa kuwa moja ya masuluhisho ya changamoto ya malisho na migogoro ya wakulima na wafugaji.