Uhaba matumizi ya teknolojia kilio sekta ya mifugo

Meneja Mkazi wa Kampuni ya URUS Tanzania, Edson Mfuru akizungumza katika kikao cha wadau wa sekta ya mifugo
Muktasari:
- Mfuru amesema kampuni hiyo inashiriki Maonyesho ya Nanenane ili kuonyesha teknalojia ya kisasa ya uhimilishaji kutoka Marekani na Brazil ambazo zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya mifugo kwa kuongeza uzalishaji.
Arusha. Wakati takwimu zikionyesha Tanzania ni ya pili Afrika kwa wingi wa mifugo, bado sekta hiyo inakumbwa na changamoto ya uhaba wa matumizi ya teknolojia.
Hayo yamesemwa leo Julai 29, 2024 na Meneja Mkazi wa Kampuni ya URUS Tanzania, Edson Mfuru akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Mfuru amesema kampuni hiyo inashiriki Maonyesho ya Nanenane ili kuonyesha teknolojia ya kisasa ya uhimilishaji kutoka Marekani na Brazil ambazo zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya mifugo kwa kuongeza uzalishaji.
“Lengo letu ni kusaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mifugo kama nyama na maziwa kupitia teknolojia rahisi, rafiki na yenye ufanisi ya uhimilishaji. Teknolojia tunayoitumia inawezesha kupatikana kwa ng’ombe chotara wa nyama na maziwa wenye uwezo wa kuzalisha maziwa zaidi pamoja na nyama kuliko ng’ombe wetu wa kienyeji.
“Mkakati wa mabadiliko wa kukuza sekta ya mifugo 2022/23-2026/27 unaonyesha kuwa sekta hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa na pamoja na matumizi ya mbegu za kienyeji zinazotoa uzalishaji mdogo wa maziwa na nyama,”amesema na kuongeza Mfuru.
Meneja huyo ameongeza kuwa teknolojia hiyo tayari imeshaanza kutumika nchini na kuongeza kuwa baadhi ya wafugaji wamenufaika nayo huku jitihada zaidi zikifanyika kuwafikia wafugaji wengi katika sehemu mbali mbali.
“Wafugaji watutembelee katika maonyesho ya Nanenane na tutakuwepo Morogoro, Dodoma, Mbeya, Arusha, Simiyu na Kagera ili waweze kujifunza zaidi kuhusu teknolojia hii pamoja na kupatiwa huduma,” amesema.
Pia, Mfuru amesema URUS Tanzania, ni kampuni tanzu ya URUS global inayojishughulisha na usambazaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa na nyama duniani.
Esther Mkani, miongoni mwa wadau wa sekta ya mifugo amesema kuna haja ya wadau wengi zaidi kutoa bunifu na teknolojia mpya ili kuongeza tija.
“Kwa tulipofikia sasa kuna umuhimu wadau wengine wasaidie katika kutoa teknolojia mpya na ubunifu utakaosaidia kuboresha thamani ya bidhaa za sekta ya mifugo,”amesema Esther.
Akizungumza jijini Arusha Jumatano Oktoba 25, 2023 wakati akifungua kongamano la 46 la chama cha wazalishaji na wataalamu wa mifugo na uvuvi Tanzania (TSAP), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega aliwataka wafugaji na wazalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kuwekeza katika teknolojia za kisasa na vitendea kazi sahihi vitakavyongeza uzalishaji wa mifugo na uvuvi.
Ulega alisema wizara itahakikisha inaweka mazingira bora ya kufuga, kusindika na kufanya biashara ya mazao yatokanayo na mifugo ma uvuvi na makundi yote katika mnyororo mzima wa thamani.
“Ni wakati muafaka wa kufanya mapinduzi katika mnyororo mzima wa thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe bora kwa wananchi na masoko yanayotuzunguka,” alisema Ulega